Dkt. Gwajima D
Minister
- Nov 28, 2015
- 966
- 6,019
Wapendwa wazee wetu, sote tunaikumbuka historia ya Disemba 14 mwaka 1990, ambapo, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa kupitia Azimio Namba 45/106 ulitenga siku ya Oktoba 1 kuwa Siku ya Kimataifa ya Wazee. Vilevile, sote tunakumbuka kuwa, tangu kuanza kwa maadhimisho haya mnamo mwaka 1991, nchi yetu Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuadhimisha siku hii lengo likiwa ni kuhakikisha jamii inajengewa uelewa na kutiwa hamasa kuhusu kulinda haki, ustawi na maslahi ya Wazee hapa nchini.
Wapendwa Wazee wetu, kama mnavyofahamu, maadhimisho ya kesho tarehe 1 Oktoba, 2024 yatafanyika kimikoa ambapo, viongozi wa mikoa yote watapata fursa ya kuzungumza nanyi na kufanya tathmini ya maendeleo na ustawi wa wazee kwenye maeneo yao.
Baada ya maadhimisho haya, wizara itaendelea kufanyia kazi utekelezaji wa yote yatokanayo na tathmini ya kila mkoa yanayohitaji utekelezaji wa kitaifa.
Kwa upande mwingine, nachukua fursa hii kuiasa jamii yote hususan wale wote ambao hawajafikia umri rasmi wa uzee kutambua na kukumbuka kuwa, uzee na kuzeeka hauepukiki na kila anayeomba umri mrefu anaombea kufikia uzee na hakika, anaombea afikie uzee mwema na kwa hali hiyo, hana budi kumpenda na kumheshimu mzee wa leo.
Hivyo, katika kuthamini maendeleo na ustawi wa wazee wa leo sambamba na kutazama mbele kwenye hatma za ustawi na maendeleo ya wazee wa kizazi kijacho, Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Mwaka 2024 inasema “Tuimarishe Huduma kwa Wazee, Wazeeke kwa Heshima” ikiwa na maana ya wazee wanastahili heshima kwa kuboreshewa mifumo yao mbalimbali ya upatikanaji wa huduma zote za kijamii na ulinzi kwa usalama wao.
Wapendwa Wazee wetu, katika kuboresha mifumo mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wazee nchini, Serikali iko kwenye hatua za mwisho kukamilisha kuhuisha Sera ya Wazee kama ambavyo mmekuwa mkitaarifiwa kupitia Baraza la Ushauri la Wazee ambapo, kuhuishwa kwa Sera hii ni hatua kuelekea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali za kundi hili ambalo ni tunu ya Taifa letu.
Wapendwa Wazee wetu, kwa heshima, narudia tena kuwatakia kila heri kwenye kuadhimisha siku yenu adhimu ya wazee duniani tarehe 1 Oktoba, 2024.
Picha hapa chini tarehe 13 Septemba 2024 ilikuwa uzinduzi wa Help Age Tanzania (NGO) inayojishughulisha na maendeleo na ustawi wa Wazee.