Udhibiti wa mali ni muhimu katika biashara kwani husaidia kufahamu ni wakati gani, vipi na kwanini unahakikisha huishiwi na mali ili usiwakere wateja wako. Pia itakusaidia kupunguza hasara inayoweza kusababishwa na wizi, uharibifu au uchakavu. Ili kuepuka matatizo katika biashara yako na hasa kufilisika, yafaa kuwa na malengo ya biashara yako. Jiulize kwanini unafanya hicho unachokifanya? Usijiingize kwenye biashara bila kuwa na malengo maalum. Je una malengo gani na unachofanya?Pamoja na kukosa malengo ya biashara, watu wengi wamekuwa wakianzisha biashara bila mpango wa biashara (Business Plan). Mpango wa biashara ni tathmini ya mwelekeo wa biashara kwa ujumla wake, ni ramani katika kiganja cha mkono wako, ili ufike unakotaka.
Mpango wa biashara hutoa mwelekeo kwa mjasiriamali, kujua bidhaa anazouza, soko lake, gharama, mahitaji, pamoja na fedha zitakazohitajika katika biashara husika, matokeo tarajiwa ya biashara nakadhalika. Yafaa kuwa na kitu kitakachokupa mwelekeo mzuri.
Bila mpango wa biashara, unaweza kujikuta unafanya biashara ambayo haina mwelekeo wowote, zaidi ya kununua mali kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu, wakati kuna gharama mbalimbali za kuzingatia katika biashara yako.
Biashara yoyote ili ipate mafanikio yafaa kuwa na mpango wa biashara, ambao utatoa mwelekeo wa wapi biashara ielekee na kutoa matokeo gani na kutofanya, hivyo kunaweza kusababisha usipate matokeo mazuri katika biashara yako na kuwa endelevu.
Pia kuna Kumbukumbu za biashara ambazo ni muhimu sana hata ukizingatia msemo wa wahenga kuwa mali bila daftari hupotea bila taarifa. Hivyo biashara bila kumbukumbu ni sawa na bure. Kumbukumbu zina umuhimu na fadia zake ni kama zifuatazo;
Mmiliki kujua faida halisi ya biashara
Faida ya biashara inatokana na mapato baada ya kutoa matumizi, hivyo ni dhahili ili kupata faida halisi mfanyabiashara anapaswa kuweka taarifa zake za mapato na matumizi kwa usahihi na kweli.
Kulipi kodi halali
Kipengele 80 cha sheria ya kodi ya mapato kinatoa nafuu kwa mlipa kodi anayetunza kumbukumbu zake za biashara. Mfanyabiashara asiyekuwa na kumbukumbu za biashara yake anaweza kudaiwa kodi kubwa kuliko stahili yako. Hivyo kumbukumbu za biashara zinasaidia kulipa kodi stahiki na sahihi.
Husaidia kufuatilia mtiririko wa biashara na mapato
Mtiririko wa biashara unahusisha mambo mengi ikiwemo ununuzi wa bidhaa, gharama za biashara, mauzo, wadeni na wadai na hata mali za biashara. Kwa hiyo, kwa mfanyabiashara kuweka kumbukumbu za biashara zitakuwezesha kujua hali na thamani ya mali, madeni na mtaji wa biashara. Hali kadhalika, mtiririko wa fedha. Kwa ujumla utajua thamani ya biashara yako.
Husaidia kuthibitisha au kutoa ushuhuda wa miamala ya biashara
Mwendelezo wa utunzaji kumbukumbu za biashara hufikia hatua ya kufanya ukaguzi wa mahesabu ambapo wakaguzi wa mahesabu hukagua taarifa hizo ili kutoa ripoti ya taarifa za fedha. Nyaraka zilizotunzwa vizuri mfano, stakabadhi, vocha za malipo na risiti zake ndizo zitathibitisha kuwa kweli muamala ulifanyika na malipo au maingizo ni sahihi.
Mamlaka ya Kodi nchini – TRA na hata benki huhitaji kuona nyaraka hizo hizo za biashara ili kujiridhisha wakati wa kukadiria kodi ya biashara yako hiyo.
Mahitaji ya wawekezaji
Wakati mwingine unaweza kuhitaji kuongeza nguvu/mtaji wa biashara kwa kupitia njia ya kutafuta mwekezaji au mbia, hivyo kumbukumbu ulizonazo ndizo zitakazomfanya mwekezaji au mbia kutoa maamuzi. Na wakati mwingine unaweza kutaka kuuza biashara yako, ili kujua bei au thamani ya biashara hiyo kumbukumbu lazima ziwe zimetunzwa vizuri.
Kuongeza mtaji kupitia mikopo
Watu wengi hutumia njia ya mikopo toka benki au taasisi za fedha kuongeza mtaji wa biashara. Kamwe huwezi hata kusogelea taasisi hizo kama huna kumbukumbu za biashara yako. Ili utembee kifua mbele au taasisi za fedha zikufuate zenyewe kukuomba ukope kwao, ni vyema utunze vizuri kumbukumbu za biashara yako.
Aina ya kumbukumbu za biashara
Cash book – hurekodi taarifa zinazohusiana na fedha taslimu au fedha iliyo benki kuingia (kupokea) au kutoka(kulipa)
Chati ya Cash Book ina sehemu kuu mbili yaani mweke na mtoe. Mweke ni sehemu ambayo maangizo yote ya fedha taslimu na benki huandikwa. Mtoe ni sehemu ambayo malipo au fedha iliyotoka huandikwa. Hali kadhalika, kama fedha taslimu imepelekwa benki ni lazima pande zote mbili ziandikwe, upande wa mweke na mtoe.
Mwisho wa kila siku lazima ufunge kitabu chako kwa kupata jumla ya taslimu na benki upande wa mweke na jumla ya taslimu na benki upande wa mtoe. Kisha kupata balansi fungia kwa kuchukua jumla ya upande wa mweke kutoa jumla ya upande wa mtoe. Salio fungia huandikwa upande wa mweke. Na mwisho unafungua mstari wa chini ili kurekodi miamala ya siku inayofuata, chukua salio fungia kuwa salio anzia, kisha mtiririko unaendelea(kama hapo juu).
Petty cash – hurekodi matumizi madogo madogo ya fedha taslimu katika uendeshaji wa kila siku wa biashara.
Debit and Credit note – hurekodi taarifa zisizohusu fedha taslimu. Debit note hutumika kuandika taarifa ambazo unategemea kupokea fedha (mali) na Credit note hutumika kuandika taarifa ambazo unategemea kulipa fedha (deni).
VAT Account – kwa biashara za kuuza bidhaa huwa zinakuwa na namba ya usajili ya ongezeko la kodi - VRN, hivyo lazima uwe na akaunti maalum kwa ajili ya kodi za VAT.
Purchase day book – hurekodi taarifa za manunuzi ya bidhaa au malighafi kila siku.
Sales day book – hurekodi taarifa za mauzo
Production records – hurekodi taarifa za uzalishaji wa kila siku kwa wenye biashara za viwanda.
Bank statement – hii ni taarifa kutoka benki inayoonesha mtiririko wa miamala ya biashara yako kwa fedha zinazotoka au kuingia kwenye akaunti hiyo. Pia hurekodi makato mbalimbali kama gharama za benki. Ni lazima kila biashara kuchukua taarifa hii toka benki walau mara moja kila mwezi.
Mikataba – biashara nyingi huwa zina mikataba mfano pango, kuleta bidhaa au kuuza bidhaa au huduma. Mikataba hii ni muhimu sana kuwa kumbukumbu za biashara.
Rekodi za kompyuta – biashara zingine hutumia mfumo wa komputa hasa kupunguza kazi za makaratasi. Pia ni muhimu kuhakikisha taarifa zinaingizwa vizuri na kutunzwa sehemu mbalimbali (back up).
Inashauriwa ili uwe na kumbukumbu sahihi ni bora kuhakikisha fedha yote inaingia kwenye akaunti ya benki na matumizi yote hutoka kwenye akaunti ya benki. Hii itasaidi kudhibiti matumizi na kuleta nidhamu ya fedha.