Historia ya kusisimua kuhusu Peter Tosh na kifo chake

Historia ya kusisimua kuhusu Peter Tosh na kifo chake

Joined
Feb 6, 2021
Posts
12
Reaction score
34
2787662_164340169_4058950797471932_5451852098395649003_n.jpg

PETER TOSH, ALIKUWA MTU WA KUUAWA TU(a man who must be killed), KWA SABABU ALIKUWA MTU NA NUSU, HAKUWA MTU WA KAWAIDA

Bunny Wailer amnyooshea kidole mjane wa Bob Marley, Rita Marley.

Ulikuwa ni usiku wa joto jingi katika mji wa Kingston nchini Jamaica. Usiku ambao haukukomaa saana tangu jua lizame. Usiku wa ijumaa ya tarehe 11 Septemba, 1987. Ambapo gwiji wa muziki reggae duniani, Peter Tosh, damu yake ilipomwagwa kinyama nyumbani kwake. Na kwa hakika walifanikiwa kuufumba "mdomo mkubwa! Hatimaye wakapumua, walimaliza kazi. Ndiyo, Peter Tosh aliuawa usiku huo, akimfuata mwenzake, Bob Marley.

Ni siku ambayo, punde tu, alikuwa nyumbani kwake akipumzika baada ya safari ya kutoka Marekani katika ziara yake ya kimuziki. Na wakati huo ndani ya nyumba yake alikuwa na mkewe Marlene Brown - mke mwingine mdogo aliyekuwa anaishi naye kwa kipindi hicho. Pia walikuwemo watu wengine watano, 'memba' wa bendi yake na wengine waliokuja kumsalimu mara baada ya ziara. Na watano hao, ni Wilton 'Doc' Brown, Michael Robison, Jeff 'Free I' Dixon ambaye alikuwa Dj wa mtaani pamoja na mkewe Joy Dixon, pia alikuwepo Carlton 'Santa' Davis; mpiga "drum" matata katika bendi ya Peter Tosh. Wote walikuwemo nyumbani kwake usiku huo.

Haikupita kitambo sana, Peter Tosh alisikia kama kuna jambo nje. Kama vile mtu anagonga mlango. "Mikey, nenda kaangalie getini", Tosh alimwambia mmoja kati ya watu waliokuwemo ndani humo. Hakujua ulikuwa ni usiku wa mwisho kwake. Usiku ambao muziki wa reggae uliuawa.

Punde tu, mara Michael alipofungua geti, watu watatu wenye bunduki waliingia ndani. "Tulieni! Na hili linatokea kwa sababu yako wewe", alisema mmoja kati ya wauaji hao watatu akimuoneshea mke wa Tosh, Marlene Brown. Anaikumbuka sana siku hiyo Carlton 'Santa' Daivis, mmoja kati ya manusura aliyekuwa anatoa ushuhuda huu hivi karibuni. Na wakati huo wa tukio yeye alikuwa bado hajaonwa na wauaji hawa, kwa kuwa likuwa ameketi katikati ya mapazia yaliyokuwa yamemziba asionekane vizuri.

Na nyuma yake, 'Santa', kulikuwa na mlango wa kioo, hakudhani kama wamemuona. Alimgundua mmoja kati ya wauaji hao, Leppo Lobban, mtu aliyekuwa ameachiwa kutoka jela mwaka mmoja tu upite, na ambaye alikuwa akipewa msaada na Peter Tosh sanjari na kutafutiwa kazi mara baada ya kutoka jela. Walikuwa hawajavaa vinyago, na hawakujali hata kama wangejulikana. Lakini haikuchukua muda, walimuona 'Santa' aliyekuwa amezibwa na mapazia. "we rasta, lala chini!", alisema mmoja kati ya wauaji akimwambia 'Santa'. Wakati huo, wote walikuwa wamelala chini. Wamelalia matumbo na sura zikitazama kiupandae - yaani zimelalia sikio.

Hapo ndipo Leppo alipoanza kumuuliza Peter Tosh kwamba ameweka wapi pesa. Tosh alisistiza kwamba hakuwa na pesa yoyote ndani kwa wakati huo, labda angekwenda Benki siku ya jumatatu. "Nitakwenda Benki jumatatu". Walimpiga na kitako cha bunduki tena na tena. 'Santa' aliyekuwa amelala pembezoni mwa Tosh, alimsikia Tosh kwa namna alivyokuwa akigugumia kwa maumivu makali. "kwa kweli inaumiza, sikuwa na uwezo wa kufanya lolote kumuokoa kaka yangu", alisema 'Santa'.

Baada ya kipigo kizito kwa Tosh, na wakati huo hana pesa, mmoja wao alisikika akisema, "unakufa usiku huu". Kulikuwa kimya kidogo. Na kwa mara ya kwanza mtu mgumu na jasiri, Tosh alionekana kuogopa, alijua kifo kimefika, ila hakuwa na namna. Baada ya sekunde kadhaa risasi zilipigwa. Ni Peter Tosh, alikiwa amelala sakafuni kimya na rasta zake ndefu, risasi zimefumua nyuma ya kichwa chake. Walifuatia wengine na wao wakamiminiwa risasi.

'Santa' alikuwa wa mwisho, alijua ni zamu yake imefika. Alipgwa risasi sehemu ya bega upande wa kushoto. Baada ya muda kukawa kimya. Akasikia kwa nje mlio wa gari iliyowashwa na kutokomea.

'Santa' alikuwa anapumua kwa shida wakati huo, alimwambia Marlene aliyekuwa pia hajiwezi, kuwa pumzi ina mbana. Alikimbilia haraka haraka na kwenda kwenye gari lake aina ya "Jeep". Aliiwasha ambapo upande mmoja tu, wa kulia wa mwili wake ndio uliokuwa na uzima, na mwingine ukifa ganzi. Aliendesha hadi hospitali ya chuo cha West Indies. Baada ya dakika kumi alikuwa akipiga honi kwa nguvu nje ya geti. Alipokuja kuchukuliwa na kukimbizwa chumba cha dharura, alipoteza fahamu kwa muda.

Baada ya kuzinduka, upande mmoja alikuwa Jeff 'Free I' Dixon akiunguruma kwa taabu, na upande mwingine alikuwa Peter Tosh ambaye madaktari walimzigira wakihaha huku na kule. Hapa ndipo 'Santa' aliposikia daktari mmoja akisema, "Nina mashaka kuwa bwana Tosh ametutoka". Licha ya kuwa hajiwezi, kauli hiyo ilimuumiza sana 'Santa'.

Peter Tosh alikuwa amefariki, katika umri wa miaka 42. Jeff 'Free I', Dj wa mtaa, alifariki kwa majeraha mabaya. Wilton 'Doc' Brown pia alifariki. Wengine wakasalimika roho zao, ila wakiwa na majeraha makubwa.

Baada ya polisi kuwahoji waliosalimika, walimtaja Leppo Lobban. Baadaye alikamatwa na kufunguliwa mashitaka. Naada ya hukumu iliyochukua dakika 11 tu, alihukumiwa kunyongwa hadi kufa, lakini baadaye adhabu ikatenguliwa na kuwa ya kifungo cha maisha. Leppo ambaye amekuwa akikanusha hadi sasa kuwa hausiki na mauaji hayo. Na kwamba usiku wa tukio alikuwa katika kioski akipata kinywaji na ndipo aliposikia tukio hilo la kuuawa kwa Tosh kupitia kwa watu.

Dennis 'Leppo' Loban, mtukutu aliyetumia maisha yake kwa kiasi kikubwa akiwa jela. Hata baada ya kutoka tu, Octoba 1986, mwaka uliofuata, Septemba 1987, akaondoa uhai wa Peter Tosh, mtu ambaye alijitolea kumsaidia kwa kila hali kwa sababu alimfahamu, na wamekuwa wote mitaa ya Trench Town. Na sasa ndio huyu aliyerudi kuuondoa uhai wa Tosh.

Kweli Tosh aliwahi kuimba katika wimbo wake mmoja unaoitwa "Maga dog" akisema "Sorry fi maga dog. Him turn around bite you". Akiwa na maana ambayo si ya moja kwa moja, kwamba unaweza kuumpa chakula mbwa mwenye njaa na aliyekonda ili anawili, lakini baadaye akageuka na kuuma mkono uleule unaompea chakula. Na ndivyo alivyofanya Leppo Lobban kwa Peter Tosh.

'Santa', anamnyooshea kidole mke wa Peter Tosh, Marlene Brown kwamba ndio chanzo cha Tosh kuuawa. Kwamba siku chache kabla ya tukio. Marlene alikwaruzana na Leppo, alimtukana na kumwita Leppo jina ambalo ni matusi kwa Jamaica, "batty man", kwa maana ya mtu anayeshiriki mapenzi ya jinsia moja. Leppo alilaani na kusema Tosh ameshindwa kumchunga mkewe aliyemtawala, hiyo yeye atamfundisha.

Kuna baadhi ya vyanzo vinadai kuwa, aliyekuwa mwanakundi wa "The Wailers", Bunny Wailer, amemshutumu mke wa Bob Marley, Rita Marley kuhusika na mauaji ya Peter Tosh akimtumia Leppo Lobban. Pia Bunny Wailer akinukuliwa na vyanzo hivyo, anaenda mbali na kudai pia Rita ndiye aliyepanga mauaji ya mumewe, Bob Marley kwa kumpa vumbi la mlipuko wa nyuklia(Radioactive Ash) alilopewa na aliyekuwa mmiliki na 'prodyuza' wa lebo ya "Island Record", Christopher Blackwell ambaye Bob Marley alikuwa chini yake. Au kwa kuwa Bunny Wailer na Rita Marley wanaugomvi wa muda mrefu? Hatujui. Lakini ukweli unabaki kuwa Peter Tosh alitakiwa afe tu. Kwanini?

'Mdomo mkubwa' na msimamo ulimuua Tosh. Leppo alikuwa ni kama 'kisu' tu. Lakini kuna mkono ulioshika 'kisu' hiki, ndio ulioangamiza maisha ya gwiji huyu wa reggae duniani. Kujua kwanini Peter Tosh aliuawa, ni lazima kujua falsafa ya maisha yake kwa ujumla.

Naam, Peter Tosh alizaliwa mnamo tarehe 19 Octoba, 1944 mji wa Westmoreland Jamaica. Alizaliwa kwa jina la Winston Hubert McIntosh. Alizaliwa kutoka kwa wazazi wawili waliokuwa watu wa kanisa. Baba yake, James McIntosh aliyekuwa mchungaji wa kanisa katika mtaa wa Savanna-la-Mar, ambako alikutana na mama yake Peter Tosh, Alvera ambaye alikuwa muumini wa kanisa hilo.

Kwa nyakati hizo za makuzi ya udogoni akitumia jina la ubatizo la Winston Hubert McIntosh, hakupata bahati ya kulelewa na wazazi wake. Hasa kwa baba yake ambaye alikuwa na watoto wengi, hivyo na kuwasahau wengine. Maisha yake kwa kiasi kikubwa amelelewa na Shangazi yake. Lakini, tunaweza kisema, amejilea mwenyewe.

Amekuwa ni mtu wa kujitegemea sana tangu akiwa mdogo. Aliwahi kuulizwa kama shangazi yake ndiye aliyemkuza na kama alikuwa na mchango wa kufanya maisha yake yawe kama yalivyokuwa. "Hapana. Hapana. Unajua, nilikuwa na miaka mitatu kwa umri, lakini ni kama nilikuwa na miaka hamsini kifikra"

Akiwa katika umri wa mdogo kabisa, alianza kujifunza kupiga gitaa. Hasa ni baada ya kupita mtaani na kumuona mtu aliyekuwa analicharaza. Tosh alivutiwa sana. Alisogea na kumtazama kwa karibu mtu huyo, ambaye aliamua kumfundisha kwa muda mfupi. Baadaye alipopata la kwake, alifanya mazoezi na kuwa mpigaji hodari wa gitaa. Kutokana na ubishi, udadisi na ung'ang'anizi wa kutaka kujua jambo, ndivyo vilivyomsaidia baadaye ukubwani kujua kupiga karibia ala nyingi za muziki na kuwa mwalimu mzuri wa Bob Marley katika gitaa mara walipokutana.

Baada ya kuishi katika mji wa Savanna-la-mar kwa zaidi ya muongo mmoja, Tosh na shangazi yake mwaka 1956 walihamia mtaa wa Denham, Kingston. Ambapo miaka mitatu mbele, Tosh akiwa na miaka 15, shangazi yake alifariki na kumuacha na mjomba wake. Ambapo ni kama alikuwa anajilea mwenyewe.

Mwaka anaouawa, 1987, alitoa albamu yake ya mwisho kwa jina la "No Nuclear War". Ambapo mwaka 1988, baada ya kufariki, ilichukua tuzo ya "Grammy" kama albamu bora ya reggae ya mwaka. Ni katika albamu hii, Tosh amepinga matumizi ya silaha za nyuklia, na kupinga ubaguzi wa makaburu Afrika Kusini, katika nyimbo za "No Nuclear War" na "Fight Apartheid".

Na hii ndiyo ilikuwa falsafa yake, ambayo watu waliifananisha na ile ya Malcolm X katika kidai haki. Hakupenda kuimba nyimbo za kuhamasisha upendo kama Bob Marley wakati wengine wanakandamizwa. Falsafa yake ilitofautiana na ya Bob Marley aliyefananishwa na Martin Luther King Jr, ya kudai haki kwa kuhimiza upendo na mshikamano.

Tosh hakuwahi kuwa mnafiki, aliongea kile kilichopo katika fikra zake. Aliwahi kuulizwa kama kifo cha cha Bob Marley atakuwa amepoteza kitu. "Hapana, hakuna nilichopoteza. Kama mke wangu akifa, hakuna nitakachopoteza. Hivyo, hata kaka yangu alivyofariki, hakuna nilichopoteza. Sijali kuhusu hilo". Kuna wakati pia aliwahi kuulizwa kama atamkuta Bob Marley peponi badala yake alijibu kuwa amekwisha kuwepo huko mara kadhaa.

Peter Tosh, mwembamba na mrefu wa futi 6 na inci 4. Alikuwa hajibu kwanza kabla hajafikiria. Kwa matendo yake, alikuwa kama mtume aliyetumwa kupitia muziki wa reggae kufikisha ujumbe. Alikuwa mtu wa watu ambaye hakuwahi kuwa mbinafsi. Mtu aliyewafanya Lucky Dube na Senzo kuanza kuimba muziki wa reggae.

Lakini huyu Peter Tosh, alikuwa mtu wa kuuawa(a man who must be killed) kwa aliyoyasimamia na kuyafanya. Ndiyo mawazo ya wakubwa yalivyokuwa yanawaza. Hakika mawazo yake hayakupendwa na mfumo ouvu aliouita "Babylon System". Alikuwa zaidi ya mwanajeshi aliyepigana vita kwa kutumia silaha za moto. Alitumia kalamu na maiki kupandikiza fikra za kimageuzi kwa watu waliokandamizwahususani watu weusi na Afrika kwa ujumla. Alipigana kipindi kigumu, kipindi ambacho wanaharakati wengi waliuawa. Tosh aliipigania Afrika kuliko mwanamiziki yeyote wa ulimwengu huu kupata kutokea.

Hadi aliamua kutoa albamu na kuiita jina la "Mama Afrika", hakujali kama wazungu walioshikilia mfumo kwamba wataitangaza ama kuinunua, alijali utu. Alikuwa mmajumui(Pan Africanst) kweli kweli kuliko hata waafrika wenyewe. Kabla ya kuuawa, alikuwa na ndoto ya kujenga shule kwao Jamaica ili watoto wasome. Kifo kilichokuwa kinamnyemelea, hatimaye kikamchukua akiwa na umri wa miaka 42 tu kabla ya ndoto yake kutimia.

Hadi sasa, wakubwa wa Jamaica wanaonekana kutompenda Peter Tosh zaidi ya Bob Marley, wala nyimbo zake hawazipendi. Ni msumari wa moto unaochoma kidondani.

Dennis Leppo Lobban, mtu aliyetumika kama kama kisu, alimuua. Je, ni nani aliyekuwa nyuma yake? Basi kwa kazi za Tosh na maisha yake kwa ujumla, muuaji umekwisha mtambua fikrani mwako.

Peter Tosh ameacha mke na watoto sita wengine wakiwa wanamuziki wa reggae kama baba yao. Wanajitahidi kulitangaza jina la baba yao, na wananuia kufungua jumba la makumbusho kwa ajili ya baba yao.

#Sky_videos_production_tz
#Mr_camera_man

Jah bless!
 
Mkuu binafsi namkubali sana Peter Tosh na pia sipingani na opinio yako, lakini ni ukweli usiopingika kuwa Bob Marley ni namba nyingine katika historia ya reggie. Hajawahi kutokea na hatotokea mwimba reggie wa aina ya Bob Marley dunia nzima, na hasa bara la Africa tunalifahamu hili.
 
Back
Top Bottom