KILIO CHA MIFEREJI YA DAMU IENDAYO ETHIOPIA
SEHEMU YA NANE
Kama ambavyo nilieleza kwenye sehemu iliyopita kwamba Kagame alichagua mji wa Ruhengeri kuwa mji wa kwanza kuushambulia kutokana na sababu tatu… kwanza ulikuwa ni mji wa Ukanda ambao anatoka Rais Habyarimana na mkewe, pili mji ulikuwa chini ya milima ya Virunga ambayo RPF walikuwa wameweka kambi kwa kipindi cha miezi mitatu lakini pia walichagua mji huu kutokana na uwepo wa Gereza kuu la Ruhengeri ambalo ndilo lilikuwa gereza kubwa kushinda magereza yote nchini Rwanda.
Mkuu wa Gereza mara ya kwanza alipiga simu Kigali na kuongea na Kanali Elie Sagatwa ambaye alikuwa ni moja ya wale 'akazu' ambao niliwaongolea huko nyuma (inner circle ya Rais Habyarimana ambayo ilijengwa na ndugu wa mkewe na familia yake).
Kanali Sagatwa alimuamurj kwamba ashirikiane na askari wenzake awapige risasi wafungwa wote.
Mkuu wa gereza Bw. Charles Uwihoreye kwa kiasi fulani kuna chembe za busara zilimjia kichwani… mji wote wa Ruhengeri ulikuwa chini ya RPF kwa hiyo hakukuwa na uwezekano wa wao kutoka mahala hapo na kukimbia salama. Kwa hiyo kama anahitaji kuishi ni vyema awe na kitu fulani cha kuwafurahissha RPF.
Uwihoreye alikataa kutekeleza agizo hilo la kanali Sagatwa la kuua wafungwa wote.
Ilibidi Sagatwa awasiliane na Rais Habyarimana kumueleza kuhusu kinachoendelea gereza la Ruhengeri. Rais Habyarimana akatoa ruhusa kwamba wafungwa wote wapigwe risasi.
Kanali Sagatwa akapiga simu tena kwenda kwa mkuu wa gereza Ruhengeri kumtaka atekeleze agizo hilo na kumsisitiza kwamba agizo limethibitishwa na amri kutoka kwa Rais.
Kwa mara nyingine tena Mkuu wa gereza alikataa katakata kutekeleza agizo hilo.
Dakika chache baadae wapiganaji wa RPF walivamia gereza la Ruhengeri na kuliweka mikononi mwao. Kutokana na kitendo cha mkuu wa gereza kuweka msimamo na kukataa kutekeleza agizo la Rais Habyarimana na kanali Sagatwa kuua wafungwa wote, RPF walimsamehe mkuu wa gereza na kumuacha aishi japokuwa isingekuwa hivyo ni lazima wangempiga risasi kutokana na mafungamano yake na Rais Habyarimana.
Wafungwa wote wa gereza la Ruhengeri waliachiwa huru huku Bw. Théoneste Lizinde ambaye alikuwa ni moja wa wafungwa kwenye gereza hilo na rafiki mkubwa wa zamani wa Rais Habayarimana kabla ya kumsaliti na kutaka kumpindua, alishawishiwa na kujiunga na RPF kutoka na taarifa adhimu ambazo alikuwa nazo kuhusu serikali nzima na Habyarimana mwenyewe binafsi.
Wapiganaji wa RPF waliushikilia mji mpaka mida ya alasiri kabla ya kuondoka na kurejea msituni kwenye milima ya Virunga. Tayari walikuwa wamefanikiwa kutuma ujumbe waliotaka kwamba, RPF bado iko na iko imara na pia walikuwa wamemdhalilisha Rais Habyarimana na kuonyesha udhaifu wa jeshi lake.
Ilipita siku moja nyinginendipo serikali ilitangaza hali ya hatari nchi nzima na kutuma vikosi vingine vya jeshi kwenda mji wa Ruhengeri.
Wapiganaji wa RPF waliendelea kuuvamia mji wa Ruhengeri kila siku usiku na kupambana na vikosi vya serikali. RPF hawakuwa na ya kuushikilia huu mji. Walikuwa wanafanya hivi (kuvamia usiku na kuondoka) ili kuwachosha tu vikosi vya serikali. Hii ni moja ya mbinu adhimu ya kisaikolojia ambayo kagame aliitumia sana kwenye vita. Kumchosha kwanza adui vya kutosha na kisha kufanta shambulio kubwa madhubuti.
Kwa hiyo hatimaye nchi ya Rwanda ikarejea vitani tena baada ya kutulia kwa karibia miezi minne.
Vita iliendelea kupamba moto. Majeshi ya serikali yalizunguka sehemu zote muhimu za milima ya Virunga. Ubaya ni kwamba RPF ndio ambao walikuwa wako sehemu ya kimkakati (juu ya milima) kwa hiyo vikosi vya serikali walikuwa hawawezi kufanya "all out assault" kwenda juu mlimani.
Kagame aliendelea kuwaongoza wapiganaji wa RPF kufanya mashambulizi makali na kisha kurudi kujificha milimani. Walikuwa wanafanya hivi mara kwa mara na kwa umahiri mkubwa.
Kuna wakati kagame alikuwa anawaongoza wapiganaji wake kushambulia maeneo kumi tofauti kwa pamoja ili kuwachanganya vikosi vya serikali wasijue ni wapi hasa ambako walipaswa kuelekeza nguvu zao.
Mashambulizi ya namna hii yaliendelea kwa miezi kadhaa huku taratibu RPF wakipata kile ambacho walikuwa wanakitaka. Walifanikiwa kuwachosha vikosi vya serikali na hatimaye kuanza kuweka maeneo muhimu kwenye himaya yao. Moja ya maeneo ya kimkakati kabisa ambayo RPF walifanikiwa kuyaweka chini yao ilikuwa ni mji wa Gatuna ulioko mpakani.
Mji huu ndipo ambapo mizigo yote kutoka bandari ya Mombasa inapitia hapa na kuingia ndani ya Rwanda.
Hii iliifa ya serikali ya Rwanda kubadili route na kuanza kutumia bandari ya Dar es Salaam kwa kiwango kikubwa ambapo route hii gharama yake ni kubwa mno kulinganisha na gharama ya kutoka bandari ya Mombasa kuingilia mji wa Gatuna.
Kutokea hapa kwenye mji huu taratibu vikosi vya RPF vilianza kusonga mbele. Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 1991 vikosi vya RPF vilikuwa vimeweka chini ya himaya yao karibia 5% ya nchi ya Rwanda.
Wakahamisha makao makuu yao kutoka kwenye milima ya Virunga mpaka jimbo la Byumba karibu na mji wa Mukindi ambako kulikuwa na kiwanda cha chai kilichotelekezwa kutokana na vita hiyo na wakafanya hizi kama ofisi zao na makao makuu yao.
Katika kipindi hiki ndipo ambapo Wahutu nao labda kwa kiasi fulani waliweza kuhisi yale maumivu ambayo Watusi waligapitia kwa miongo kadhaa ya kuishi kama wakimbizi. Miji mingi hii ambayo RPF waliiteka ilikuwa na idadi kubwa ya wakazi wa kabila la Kihutu. Kwa hiyo baada ya miji kutekwa na RPF ilibidi wakimbie miji hiyo, lakini hawakuweza kukimbilia Uganda kwa kuwa RPF walikuwa wanamiliki eneo kubwa la mpakani. Hivyo kwenye kipindi hiki Rwanda ilishuhudiwa ikiwa na idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani (internally displaced).
Japokuwa kuibuka tena huku kwa vita kulikuwa na manufaa makubwa kwa RPF ambao walionekana kuchanja mbuga siku baada ya siku lakini kulikuwa na athari kubwa kwa watusi ambao walikuwa ndani ya Rwanda. Mateso yalianza tena upya kwa kiwango cha juj zaidi.
Kwanza yalianza kama tukio dogo tu... ambapo wafugaji wapatao 60 wa Kitusi katika wao pamoja na mifugo yao walikatwakatwa mapanga kwenye eneo la Kinigi. Baadae mauaji haya dhidi ya Watusi yalianza kuenea kuelekea mikoa ya kusini mpaka maeneo ya Ruhengeri na Gisenyi.
Ndani ya muda mchache tu Rwanda ilishuhudia mauajibya zaidi ya Watusi 1000. Mwezi June, 1991 vikosi vya RPF na vikosi vya serikali viliweka makubaliano kwamba pande zote mbili ziruhusu waathiriwa wa vita hiyo kukimbia na kwenda kujificha sehemu salama. Kwa kiasi fulani ilipunguza kasi ya raia wasio na hatia kuuwawa. Lakini rohonu bado kila pande ilikiwa imejawa na vihoro wakitaka kutimiza lengo ambalo walikuwa nalo mioyoni mwao.
Agathe Habyarimana
Kwenye sehemu zilizopita huko nyuma nilieleza kidogo juu ya uwepo wa 'Akazu' mara baada ya Rais Juvenile Habyarimana kushika madaraka.
Nilieleza pia kuwa moja ya vitu muhimu ambavyo vilimsaidia Habyarimana kubaki madarakani ilikuwa ni ushawishi na nguvu ya familia ya mkewe Agathe Habyarimana. Sasa basi hawa 'Akazu' walikuwa ni ndugu wa Agthe Habyarimana pamoja na ndugu wachache wa Habyarinama mwenyewe na watu wake wa karibu. Watu hawa walikuwa wamejipa jikumu la kuamua hatma ya nchi ya Rwanda, kwamba hawataki uwepo wa Watusi kwenye 'nchi yao'.
Hivyo basi kikundi hiki ambacho kilikuwa na nguvu kubwa mno, kilikuwa kinaratibu matukio mengi ovu dhidi ya watusi.
Jina lingine ambalo walijipachika lilikuwa ni "Zero Network" wakimaamisha kwamba lengo lao kuu lilikuwa ni kuwa na Rwanda yenye idadi sifuri ya Watusi.
Akazu ndio ambao walichochea kuibuka kwa itikadi ya "Hutu Power". Itikadi ya msimamo mkali dhidi ya Watusi na hata Wahutu wenye kuwakumbatia Watusi. Akazu walikuwa na kikundi chao cha wapiganaji kilichoitwa 'Impuzamugambi' na miezi michache baadae walichangia pia kuratibu kuibuka kwa kikundi cha 'intarahamwe' ambavyo tutavijadili zaidi hapo mbele kidogo.
Akazu walianzisha propaganda ya hali ya juu dhidi ya Watusi. Walifika mbali mpaka kufungua vituo vya redio na kuchapisha majarida kueneza ujunbe wao wa propaganda.
Ujumbe wao ulikuwa ni mmoja tu, kwamba Watusi si Wanyarwanda na hawana haki ya kuwepo hapo.
Propaganda hizi zilienda mbali zaidi na kufikia hatua ya wanachama wa Akazu wenye nguzu wakiongozwa na mwanahabari nguli n mmiliki wa gazeti maarufu kipindi hicho lililoitwa 'Kangura' kukaa chini na kuyengeneza "AMRI KUMI ZA WAHUTU" ambazo walizichapa kwenye gazeti la Kangura na majarida yote yanayoendeshwa na Akazu.
Amri hizi kumi ulikuwa ni muongozo ambao Wahutu wote walikuwa wanapaswa kuufuata kuanzia muda huo katika maisha yao.
Amri zenyewe ni hizi;
1. Kila mhutu anapaswa kujua kwamba kila mwanamke wa Kitusi, haijalishi ni nani, anatetea maslahi ya Watusi wenzake.
Hivyo basi Mhutu yeyote atakayefanya yafuatayi tutamuhesabu ni msaliti:
- anaye muoa mwanamke wa Kitusi
- anafanaye urafiki na mwanamke wa Kitusi
- anayemuajiri mwanamke wa kitusi kama sekretari au muhudumu wa ndani
2. Kila Muhutu anapaswa kujua kwamba mabinti zetu wa Kihutu wanafaa zaidi na wenye kuwajibika kama wanawake, wake na mama wa familia. Je sio wazuri, kufaa kuwa masekretari na waaminifu zaidi?
3. Wanawake wa Kihutu muwe hodari, washaurini waume zenu na watoto wenu wa kiume wajielewe.
4. Kila Muhutu anapaswa kujua kwamba Watusi wote sio waaminifu kwenye biashara. Malengo yao pekee ni yeye na kabila lao kutawala. Hivyo basi Muhuti ambaye atafanya chochote kati ya hivi atahesabika ni msaliti;
- atakayefanya ubia wa kibiashara na Mtusi.
- atakayewekeza fedha zake au za serikali kwenye kampuni ya Mtusi.
- kukopa au kumkopesha Mtusi
- atakayefanya fadhila ya kibiashara kwa Mtusi (kupata kibali cha kuagiza bidhaa nje, mkopo wa benki, ujenzi, masoko ya umma n.k.)
5. Nyadhifa zote za kimkakati za kisiasa, kiutawala, kiuchumi, kijeshi na kiusalama zinapaswa kuaminiwa kwa Wahutu pekee.
6. Sekta ya elimu (wanafunzi na walimu) inatakiwa kujazwa na Watusi kwa idadi kubwa zaidi.
7. Wanajeshi wote wa Rwandan Armed Forces wanapaswa kuwa Wahutu. Vita ya mwaka 1990 imetupa somo. Na hakuna mwanajeshi ambaye anaruhusiwa kuoa Mtusi.
8. Wahutu wanatakiwa kuacha kuwaburumja Watusi.
9. Wahutu, popte walipo, wanatakiwa kuungana na kushikamana na kutafakari hatma ya ndugu zao wahutu
- Wahutu walio ndani na nje ya Rwanda lazima muda wote wawatunze ndugu zao wahutu.
- wanapaswa kupinga propaganda za Watusi bila woga.
- wahutu lazima wawe shupavu na wakali dhidi ya adui yetu Watusi.
10. Mapinduzi ya mwaka 1959, Mabadiliko ya katiba ya mwaka 1961 na itikadi ya Kihutu inapaswa kufundishwa kwa Wahutu wote katika ngazi zote.
Itikadi hii pia inapaswa kusambazwa kwa kasi na Muhutu popte ulipo. Mhutu yeyote mwenye kumkataza au kumsema Muhutu mwenzake kwa kusambaza itikadi hii atahesabika ni msaliti.
Amri hizi kumi zilisomwa kwenye vituo vya redio, kuchapwa kwenye magazeti na majarida na kusambazwa kwenye vipeperushi mitaani.
Itikadi ilienea kwa kasi kama moto wa kifuu.
Kagame kwa kuona hatari iliyo mbele naye alifungua kituo cha redio jijini kampala kilichoitwa Radio Muhabura kwa ajili ya kueneza propaganda za kupinga itikadi ya "Hutu power" na amri kumi.. lakini haikufua dafu.
Bundi alikuwa ametua mlangoni na hakukuwa na wakumfanya aruke kwenda mtini.
Harufu ya damu zaidi ilinukia.
Kurasa ya mbele ya gazeti la Kangura tolea la November 1991... hayo maandishi makubwa ya kichwa cha habari tafsiri yake ni "Watusi: Wana wa Mungu"
Tamaza hayo maandishi pembeni ya picha ya Panga... maana yake "Silaga gani tutumie kuwaua hawa mende?"
Alafu pembeni hiyo picha kubwa ni Rais wa zamani Gregoire Kayibanda aliyeongoza mapinduzi na umwagaji damu wa mwaka 1959 na kuwafanya Wahutu kabila tawala.
Itaendelea...
The Bold
To Infinity and Beyond - 0718 096 811
Pls: follow, subscribe and WhatsApp