KILIO CHA MIFEREJI YA DAMU IENDAYO ETHIOPIA
RAI: Inapendeza zaidi na ni busara zaidi, uzi huu ukawa ni chanzo cha kuchochea mijadala ya kufikirisha na hoja mujaribu zenye kutufanya kukuna mbongo zetu na kuelimika. Si vyema kutumia uwanja huu kuleta malumbano ya kikabila au kitaifa na kutukanana.
Tunaweza kutofautiana kiitikadi na bado tukala meza moja, tunaweza kutofautiana kikabila na bado tukawa marafiki na tunaweza kutofautiana kwa hoja na bado tukaheshimiana.
Tuchochee udadisi, kufikiri na kushindanisha hoja. Si matusi.
Habibu.
SEHEMU YA 11
Kwenye sehemu ya kumi tulijadili namna ambavyo serikali ya rais Habyarimana walifikia makubaliano na RPF ya kusitisha mapigano lakini baadae mauaji ya watusi yaliendelea na kumfanya Kagame kuanza tena mashambulizi na kulishinda jeshi la serikalinkwa urahisi kabisa.
Tuliona namna ambavyo Habyarimana safari hii aliomba mazungumzo na Kagame ili kusitisha makubaliano.
Tuendeleeβ¦
Mazungumzo ya Uganda yalichukua siku mbili na kisha kurejea tena Arusha.
Nchi za Ulaya zilikuwa zinamtaka Kagame arejeshe nyuma vikosi vyake kurudi kwenye eneo ambalo walikuwa wanalishikilia kabla ya February.
Baada ya mabishano makali ya siku kadhaa huku Kagame akitishia kwamba ataanza tena mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali.
Ndipo hapa ambapo pande zote mbili walifikia makuabaliano.
Kwamba;
Kagame atarudisha nyuma vikosi vyake mpaka kwenye maeneo ambayo walikuwa wanayashikilia kabla ya mwezi February, 1993. Lakini maeneo hayo mapya ambayo RPF walikuwa wameyaweka kwenye himaya yao baada ya Febrary, pindi tu RPF wakirejesha nyuma vikosi vyao kutokana na makubaliano hayo basi maeneo hayo yatatengwa kama 'De-militarised zone'. Kwamba serikali haitaruhusiwa kuingiza wanajeshi wake kamwe kwenye maeneo hayo.
Makubaliano haya yalikuwa ya maana sana kwa Kagame, kwani hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa rais Habyarimana kukubali rasmi kushindwa. Japokuwa bado kuna makamanda ndani ya RPF walikuwa wanahisi kama Kagame amemwachia Habyarimana upenyo mkubwa zaidi wa kupumua, lakini Kagame mwenyewe alisimamia msimamo wake thabiti kabisa kwamba anataka kulinda taswira chanya ya RPF kwenye jumuiya ya kimataifa na kuwaonyesha kuwa RPF wako tayari pia kushughulikia migogoro kidiplomasia.
Lakini kipindi mazungumzo haya yanaendelea na makubaliani yanafikiwa, nyuma ya pazia Rais Juvenile Hibyarimana akishirikiana na serikali ya Ufaransa walikuwa wanaunganisha nguvu ya waunga mkono wao chini kwa chini ili kuipinga RPF. Katika mpango wao huu walienda mbali hata kiwajumuisha viongozi wa CDR.
Kadiri muda ulivyokuwa unaenda kukaanza kuibuka mkanganyiko. Kuna kundi la watu ndani ya MRND na CDR walitoa tamko kwamba hawakubaliani na jinsi ambavyo Ufaransa inajiingiza kwenye uratibu wa mkakati huo wa chini kwa chini. Waliona kama vile wanatwanga maji kwenye kinu. Yaani wanapambana kumuondoka "mkoloni mweusi" (watusi) na wakati huo huo viongozi wao wanaacha mwanya wa mkoloni mweupe kurudi (Ufaransa). Ndipo hapa kwa hasira wakaanza kushinikiza kwamba mkataba ulio sainiwa Arusha uheshimiwe.
Lakini pia bado walibakia lile kundi lenye msimamo ambalo walikuwa tayari lolote lifanyike (hata kama ikibidi kushirikiana na Ufaransa) kuhakikisha kwamba watusi wanaondoshwa ndani ya Rwanda.
Ndipo hapa kwenye kipindi hiki kulipamba moto vuguvugu la 'Hutu Power'.
Vyama vyote vya siasa ndani yake viligawanyika katika makundi mawili. Kulikuwa na kundi ambalo walikuwa na msimamo wa kati (moderate) ambao waliunga mkono mazungumzo ya Arusha. Alafu kulikuwa na kundi la wale wenye msimamo mkali, ndio hawa waliitwa 'Power Wing' (Hutu Power). Hawa wao walikuwa tayari kufanya lolote na kwa gharama yoyote ile kuhakikisha kwamba watusi hawawi sehemu ya uongozi wa nchi na hawaishi Rwanda kama raia mwingine.
Hiki ndicho ambacho kilitokea kwenye vyama vyote vya siasa nchini Rwanda katika kipindi hiki. Kila chama kilikuwa na hizi 'two wings'. Lakini wing ambayo ilikuwa na nguvu na ushawishi kwenye kila chama ilikuwa ni 'Hutu Power'.
Rais Juvenile Habyarimana na ujumbe wake kwenye mkutano Arusha
Hapa nchini kwetu Tanzania katika vyama vya siasa kwa miaka mingi tumekuwa na kasumba katika vyama vyetu vya siasa kwa kila chama kuwa na kikundi cha "ulinzi" cha chama. Pengine kuna walianzisha utaratibu huj walikuwa na sababu za msingi mpaka leo hii kuwa na 'Green Guard' ndani ya Chama Cha Mapinduzi na 'Red Brigade' ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo. Lakini kama tungekuwa tunaijua historia na kutumia mafunzo yake kujisahihisha si dhani kama tungelikumbatia kasumba hii ya vikundi vya ulinzi.
Kuibuka kwa Intarehamwe na Impuzamugambi
Intarahamwe na Impuzamugambi vilianza kama vikundi vya ulinzi katika vyama vya MRND na CDR kama ambavyo hapa kwetu Taznania tuna Green Guard na Red Brigade ndani ya CCM na Chadema.
Interahamwe
Maana halisi ya neno hilo ni "wanaopambana pamoja". Ni muunganiko wa maneno mawili ya kihutu, 'intera' ambayo ina maanisha 'kazi' na 'hamwe' ikimaanisha pamoja. Kwa nini sijasema "wanaofanyakazi pamoja" na badala yake nimesema "wanaopambana pamoja".
Hili neno 'kazi' (work) lilikuwa linatumika kama kauli mbiu katika radio za kibaguzi za kihutu wakimaanisha 'shughuli ya mauaji' kwa kutumia panga. Kwa hiyo lengo lao la kuchaganya neno hili halikiwa kwa ajili ya kumaanisha kazi ya uzalishaji bali ni kazi ya mauaji.
Kikundi hiki cha kihutu kilikuwa chini ya chama cha siasa cha MRND.
Ajabu ni kwamba kiongozi wa Kitaifa alikuwa ni muhutu aliyeitwa Robert Kajuga. Kajuga familia yake ilikuwa ni ya Kitusi lakini baba yake alifanikiwa kupata nyaraka za kiserikali ambazo ziliipa utambulisho familia yake yote kama wahutu. Kajuga mwenyewe alikuwa anafanya kazi kubwa sana kuficha ukweli wa mizizi ya familia yake ya Kitusi. Moja ya visa ambavyo vinasisimua sana ni namna ambavyo Kajuga alijitahidi kuificha familia yake HΓ΄tel des Mille Collines ndani ya Kigaki kipindi mauaji yalipoanza. Tutakirejea kisa hiki hapo baadae.
Impuzamugambi
Kikundi hiki nacho pia cha kihutu kilikuwa chini ya chama cha CDR. Japokuwa hakikuwa kikubwa au maarufu kama Interahamwe lakini vyote viliwi vilikuwa na lengo moja linalofanana.
Makamanda wa kikundi hiki walikuwa ni viongozi wakuu wa chama cha CDR, yaani Hassan Ngeze na Jean Bosco Barayagwiza.
Kipindi mauaji ya kimbari yalipoanza kikundi hiki kilifanya kazi bega kwa bega na Iterahamwe kama ambavyo tutaona hapo mbele kidogo.
Vikundi vyote hivi viwili vilijizolea umaarufu mkubwa ndani ya Rwanda na vijana wengi wa Kihutu waliojitafsiri kama 'wazalendo' wa nchi yao walijiunga navyo.
Wahutu wenye msimamo mkali ndani ya vyombo vya usalama ambao walikuwa na nyadhifa za juu kama vile mkui wa jeshi la polisi na mnadhimu mkuu wa jeshi la Rwanda walianza kuweka utaratibu ambapo wanachama wa vikundi hivi walikuwa wanapatiwa mafunzo ya awali ya kijeshi.
Kwa hiyo ndani ya muda mfupi sana vikundi hivi nguvu yake na ushawishi wake ukawa mkubwa kuzidi hata namna ambavyo watu walitegemea.
Japokuwa alikaa kimya na kufumbia macho lakini hii haikuwa dalili nzuri kwa uongozi wa Rais Habyarimana. Kwa sababu aliona fukuto ambalo lilikuwepo chini kwa chini. Kwamba kadiri ambavyo alikuwa anaviacha vikundi hivyo vikue na kuwa na nguvu zaidi, siku vikilipuka kwa ghasia kubwa nchi hiyo haitakuwa salama tena. Na si kama alijali zaidi usalama wa nchi bali aliogopa zaidi kupoteza madaraka kutokana na presha ambayo atapewa na jumuiya ya Kimataifa.
Wanachama wa Interahamwe na Impuzamugambi
Lakini pia nilieleza huko nyuma kwamba vuguvugu hili la Hutu Power lilikuwa linaratibiwa na 'inner cirlce' ya Akazu ambayo ilikuwa inafahamika kama 'le clan de madame'.
Hawa walikuwa ni maswahiba na ndugu wa karibu kabisa wa Agathe Hibyarimana, mkewe Rais.
Kwa upande mwingine pia kitendo cha Rais Hibyarimana kuendelea na mzungumzo ya Arusha kulikuwa kunazidi kuwachukiza wahutu wenye msimamo mkali na Habyarimana alihisi kabisa hasira hizi zinaweza kufikia kilele cha wahutu hao wakamuondoa madarakani kwa nguvu.
Hivyo basi Habyarimana tegemeo lake pekee katika kipindi hiki cha sintofahamu kubwa lilikuwa ni jumuiya ya kimataifa na RPF.
Habyarimana alikata shauri sasa kuingia kwa miguu yote miwili kwenye mazungumzo ta Arusha. Lengo lake lilikuwa ni kwanza kupata huruma na kuaminika na jamii ya kimataifa na pili aliamini kuwa kama RPF wangekuwa sehemu ya uongozi wa nchi basi ilikuwa ni njia nzuri ya kuwadhibiti wahutu wenye msimamo mkalai.
Safari hii kwenye mazungumzo alikubaliana karibia na kila sharti la RPF. Kwa mfano alikubali 40% ya jeshi jipya la nchi ambalo litaundwa liwe na wanajeshi wa RPF. Alikubali pia uongozi wa juu wa jeshi 50% wawe ni RPF na masuala mengine mengi zaidi ambayo yalikuwa ni ushindi mkubwa kwa Kagame na RPF.
Mkataba wa makubaliano haya ulisainiwa tarehe 4 August 1993.
Pia waliweka makubaliano kwamba katika kipindi hiki cha mpito lazima amani ya nchi isimamiwe na jeshi la kimataifa ili kuepuka upande wowote, wa serikali au RPF kutumia mwanya huo vibaya kujiongezea madaraka au ushaiwishi.
Ndipo hapa mwezi octoba jeshi maalumu la Umoja wa Mataifa vikosi vilivyopewa jina la UNAMIR (United Nations Assistance Mission for Rwanda) likiongozwa na Jenerali RomΓ©o Dallaire raia wa Canada liliingia nchini Rwanda kwa ajili ya kulinda amani.
Kipengele kingine ambacho Kagame alikitaka kilikuwa ni kutaka uwakilishi wa RPF ndani ya Bunge la Rwanda katika kipindi hiki cha mpito.
Bunge la Rwanda muundo wake uko hivi; kuna 'Uper Chamber' (au Sena kwa kinyarwanda (senate kwa umombo ) na kuna 'Lower Chamber' (au Umutwe w'Abadepite (chamber of deputies kwa umombo).
Muundo na mfumo wa ufanyaji kazi wa Chamber hizi mbili ni kama vile Congress ya Marekani (House of Representatives na Senate).
Rais Hibyarimana alikubali kutoa nafasi za uwakilishi kwa RPF katika Chamber of Deputies.
Uhalisia ni kwamba Kagame hakuwa na haja sana na nafasi hizo za uwakilishi bali alikuwa ametumia akili ya mbali sana ambayo kwa kipindi hiki hawakumshitukia.
Kagame aliwaeleza kwamba, wanadiplomasia wake hao ambao wataiwakilisha RPF kwenye Bunge ni lazima wapewe ulinzi na wanajeshi wake wa RPF na si jeshi la serikali au UNAMIR ya umoja wa mataifa. Na alipendekeza kwamba itawapasa RPF kuingiza wanajeshi 1000 kwenye mji mkuu wa Kigali kwa ajili ya ulinzi wa wanadiplomasia wao.
Mwezi December 1993, kupitia mpango wa vikosi vya umoja wa Mataifa vya UNAMIR uliokuwa unaitwa 'operation Clean Corridor', wanajeshi 1000 wa weledi (special forces) kutoka RPF ya Kagame waliruhusiwa kuingia kwenye mji mkuu wa Kigali na kuweka makazi yao kwenye majengo ya Bunge.
Hii ndio moja ya akili adhimu ambayo Kagame amejaaliwa (psychological warfare)β¦ alikuwa amefanikiwa kuingiza special forces wake elfu moja ndani ya Kigali tena kwa ruhusa ya serikali bila kumwaga hata tone la damu au kufyatua hata risasi moja.
Wanajeshi hawa 1000 aliowaingiza ndani ya Kigali walikuja kuwa nguzo ya ushindi wake dhidi ya wahutu na kuingia madarakani kama ambavyo tutaona hapo mbeleni.
Wahutu wenye msimamo mkali hili lilikuwa ni tishio kubwa sana kwao. Waliona kila dalili ya 'adui' yao kurejea kwenye kiti cha enzi.
Mbaya zaidi, nchini Burundi ambako nako kwa miongo mingi serikali ilikuwa inaendeshwa na Watusi mwezi october kwa mara ya kwanza wananchi walimchagua Melchior Ndadaye kuwa rais wa kwanza wa Burundi mwenye asili ya Kihutu.
Ndadaye alikuwa ni msomi na mwanazuoni, mtu wa fikra pevu. Huyu hakuwa mtu wa itikadi ya 'Hutu Power' bali alikuwa amelenga kumaliza utengano wa kikabila ndani ya Burundi.
Alitaka nchi hiyo iongozwe kwa pamoja. Akaanza kufanya mabadiliko kwenye jeshi ambalo lilitawaliwa na watusi pekee na kuanza kuwajumuisha wahutu.
Wanasema kwamba uking'atwa na nyoka hata ukikanyaga jani unashituka, ndicho ambacho watusi wa Burundi kilichiwashitua. Japokuwa Ndadaye alikuwa najaribu kuiunganisha nchi lakini watusi wa Burindi walimuona kama tishio na anataka kuwaletea maswahibu kama yale ambayo yanatokea Rwanda.
Kwa hiyo wanajeshi wa Kitusi wenye msimamo mkali walimtandika risasi Rais Melchoir Ndadaye mwishoni mwa mwezi octoba na kuzua vita kubwa ya kikabila nchini Burundi.
Wahutu wa nchini Rwanda walitumia kitendo cha muhutu mwenzao kupigwa risasi nchini Burundi kuhalalisha propaganda yao ya siku nyingi kwamba Watusi kamwe hawawezi kukubali kutawaliwa na Wahutu na watafanya chochote wawezacho ili kuitawala Rwanda na kuwafanya wahutu raia wa daraja la pili.
Propaganda hii safari hii ilikuwa na msisimko kwa wapokeaji huko mtaani hasa baada ya kushuhudia Kagame ameingiza wanadiplomasia wake ndani ya Bunge la Rwanda na wanajeshi elfu moja wa RPF ndani ya Kigali.
Kwenye jumuiya ya kimataifa Kagame na Habyarimana walikuwa wanapongezwa kwa hatua hiyo ya makubaliano. Lakini mtaani ilikuwa kana kwamba petroli imemwagwa ardhini na njiti ya kiberiti imeshikwa kiganjani tayari kufanya mlipuko.
Habyarimana alijua. Na Kagame alijua. Kwamba wakati ulikuwa uko karibu. Wakati ambao hakuna mtu aliombea ifikie. Wakati ambao utautikisa ulimwengu kwa mauaji ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwenye historia ya karibu. Wakati wa jino kwa jino, msumari kwa msumari⦠wakati wa panga na shingo za watu.
Rais wa zamani wa Burundi marehemu Melchoir Ndadaye
Nikirejea tutajadili kuuwawa kwa Rais Habyarimana na Kuanza kwa mauaji yenyewe ya Kimbari.
Stay here.
Habibu B. Anga 'The Bold'- 0719 096 811
To Infinity and Beyond
Please Follow, subscribe and WhatsApp