Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Ahmed Rashad Ali
Nadhani katika niandikayo mara kwa mara mmekuwa mkisoma jina la Ahmed Rashad Ali.
Ahmed Rashad wakati wa WWII yeye alikuwa mwanafunzi India. Rashad ni katika Royal Family Zanzibar na alikuwa rafiki ya Abdul Sykes toka wadogo 1939 walipojuana kwa mara ya kwanza.
Mama yake Rashad Bi. Ruzuna bint Tamim aliolewa na Sultan Sayyid Ali bin Hamoud (1902 - 1911) na babu yake Muhammad Bakashmar alikuwa Waziri Mkuu katika miaka ya 1800.
Nilikuwa nastarehe sana ninapozungumza na Mzee Rashad. Rashad alikwenda Kalieni Camp kuwatembelea Abdul na Ally Sykes ambako askari kutoka makoloni ya Afrika baada ya vita kumalizika walipokusanywa kurudishwa makwao.
Rashad alinisomesha mengi sana katika maisha ya Abdul Sykes wakati wa utafiti wa kitabu.
Kila siku nikimbembeleza Mzee Rashad tuandike kumbukumbu zake lakini akinikatalia akisisitiza kuwa hana la maana la kuandikwa.
Baada ya kumbembeleza sana alikuwa na tukaanza.
Hatukuandika kitu baada ya pale ila nilipokea simu ya kifo chake.
Lakini kutokana na kikao kile kimoja nimeweza kuandika historia yake, ''Ahmed Rashad Ali Radio Afrika Huru, 1952,'' ambayo niliitia katika tafsiri ya Kiswahili ya kitabu cha Abdul Sykes rafiki yake toka utotoni.
Hii Radio Afrika Huru (Radio Free Africa) ilikuwa radio aliyoanzisha Abdel Nasser kwa ajili ya kusaidia ukombozi wa Afrika.
Ahmed Rashad alikuwa mmoja wa watangazaji wa radio hii.
Mzee Rashad alikuwa haishi kusikitika kuwa juu ya msaada wa Nasser kwa Tanganyika na Zanzibar wakati wa kupigani uhuru, Nasser hajapewa hata barabara moja si Dar es Salaam wala Zanzibar.
Rashad alimsindikiza Abdul siku alipokwenda kufanya mkutano na Jomo Kenyatta 1950 Nairobi.
Wakati ule Abdul alikuwa katibu wa TAA.
Rashad alikuwa na Abdul Cairo 1964 na baadae wakawa pamoja Dar es Salaam hadi Abdul alipofarika mwaka wa 1968.
Maelezo muhimu katika maziko ya Abdul niliyapata kutoka kwa Mzee Rashad.
Mzee Rashad alikaa jamvi moja na Mwalimu Nyerere katika maziko ya Abdul na walikula pilau sinia moja.
Mwalimu alipeleka ng'ombe mzima kama kitoweo katika msiba ule.
Picha ya kwanza ni Ahmed Rashad Ali, ya pili kushoto ni Ahmed Rashad Ali, Abdallah Jabir na Balozi Ahmed Uwanja wa Ndege Dar es Salaam 1998, ya tatu akimpokea Sidney Poitier Uwanja wa Ndege Dar es Salaam miaka ya 1970s picha ya nne kushoto Ahmed Rashad, Dr. Harith Ghassany na Mwandishi nyumbani kwa Mzee Rashad Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Upanga ya tano Ahmed Rashad wa pili kushoto na anaefuatia ni Ally Sykes Zanzibar 1950s.