SoC02 Hivi ndivyo jinsi visingizio vilivyohitimisha ndoto za watu wengi

SoC02 Hivi ndivyo jinsi visingizio vilivyohitimisha ndoto za watu wengi

Stories of Change - 2022 Competition
Joined
Jun 27, 2020
Posts
6
Reaction score
4
Na; Mashaka Siwingwa

Visingizio ni tabia ambayo wengi wetu sana tumejijengea na tunaendelea kujijengea siku hadi siku. Visingizio ni ile hali ya kutaka kutafuta pingamizi linalokufanya usifanye jambo fulani na mara nyingi hutolewa kwa njia ya kauli zetu mbalimbali.

Binadamu tumekuwa wenye kujijengea kauli mbalimbali ambazo huwa tunazitoa kama sababu za kutokufanikiwa kwetu na pindi tutowapo sababu hizi sisi hujiona kama watu ambao tunastahili na sababu hizi huwa tunataka ziaminiwe. Lakini mimi nataka kukuambia hapa kuwa unajidanganya na hizo sababu unazo zitoa sio sababu za msingi na sio sababu za maana bali ni visingizio ambavyo havikusaidii kitu.

Hapa nakuletea kauli kadhaa ambazo ni visingizio ili ujue kama unazitumia ujue kabisa wewe ni mmoja wapo kati ya wale watu ambao wanatoa visingizio kadha wa kadha ambavyo kimsingi vinahitimisha na kuua kabisa ndoto zako.

Nina umri mkubwa/ nimezeeka; watu wengi hutoa kauli hii wakiamini kuwa sababu ya wao kutokufanya jambo fulani ni kwa sababu ya umri wao kuwa mkubwa na kwamba hawawezi kupambana ili kukamilisha jambo fulani. Je? Kuna umri ambao umeandikwa kuwa ni umri wa kufanikiwa. Unaweza kufanikiwa katika umri wowote ule, hivyo basi acha kutumia kigezo cha umri kama ruksa au tiketi ya kushindwa kwako.

Sina kipaji; nani aliyekuambia kufanikiwa lazima uwe na kipaji. Nani aliyekuambia watu wenye kufanikiwa ni wale wenye vipaji pekee. Kwa taarifa yako watu wanaotumia vipaji na wakafanikiwa kutumia vipaji hivyo kama vile uandishi, kusakata kabumbu na vingine ni asilimia 1% tu duniani hivyo basi achana na hii kauli mara moja. Tambua kuwa unaweza kupata mafanikio makubwa sana maishani hata kama hautambui kipaji chako lakini kama hukifahamu kipaji chako tafuta ili ukijue.

Sikuzaliwa sehemu sahihi; wapi uliambiwa ndiyo sehemu sahihi ambayo ukizaliwa lazima uwe mwenye mafanikio? Nakusikia tu unajidanganya eti bora kuzaliwa mbwa ulaya kuliko mtu Afrika.

Huo ni upuuzi kwani ulaya hakuna watu masikini kama huku Afrika? Marekani kwenyewe masikini na omba omba wapo pia sasa unataka ukafanikiwe sehemu gani. Tafuta fursa hapo hapo ulipo uzitumie siyo kuleta kauli za ajabu eti sikuzaliwa sehemu sahihi, acha mara moja.

Ninatokea katika historia ya watu masikini; historia ya wapi ulikotokea haina cha kufanya na maisha yako ikiwa hautoikubali, kama ukikubali na kuamini kuwa utakuwa masikini kwa kuwa wazazi wako walikuwa masikini una matatizo makubwa sana.

Usitumie hii kama tiketi ya kutofanikiwa kwako wewe jua tu umeamua kuwa masikini basi na sio eti kisa umezaliwa katika historia ya watu masikini. Ni watu wangapi wanazaliwa sehemu ambazo hawana hata ndugu mmoja ambaye ni tajiri lakini wakafanikiwa. Hii kauli nayo imehitimisha ndoto na malengo ya watu wengi sana.

Sina akili sana; huna akili katika eneo gani labda, na umejuaje kama hauna akili. Kila binadamu ana akili ila tunatofautiana tu katika ile hali ya kuzitumia akili zetu hivyo ni muhimu ufute hiyo kauli na badala yake ujiulize ni kwa namna gani unaweza kuichezesha akili yako na ikulete mafanikio makubwa.

Sina wa kunisaidia; kwani uliambiwa kusaidiwa ni lazima! Acha kutegemea msaada wakati wewe mwenyewe una uwezo wa kujisaidia. Watu watapata hamasa na hali ya kutaka kukusaidia pindi wewe utakapo onyesha hali ya kujitutumua.

Chukulia udhamini wa wasanii, hakuna mtu anayetoka kwake na kumkuta mtu barabarani na kusema njoo nitakudhamini wakati hajui kipaji wala shughuli yake, bali msaani ili apate kudhaminiwa ni lazima aimbe aonekane kwa kazi zake yaani kazi zake zimtambulishe ndipo anapoweza kupata wa kumdhamini.

Yaani wewe ukae ndani kwako utegemee msaada unafikiri kuna mtu anayekuja kujipendekeza na kujikuta anakusaidia wewe. Acha hicho kisingizio mara moja.

Sijui kama nitafanikiwa; hii tunaita kujipinga mwenyewe, kwanini uamini kuwa hauwezi kufanikiwa maishani! Nakuambia leo unaweza unaweza tena sana zaidi ya unavyoweza kudhani kuwa unaweza kufanikiwa hivyo basi acha kauli hiyo ya kuwa sijui kama nitafanikiwa.

Sina mwalimu sahihi; ni kweli ili ufanikiwe lazima uwe na mwalimu ambae atakuwa akikushauri na kukuongoza katika mengi na kukuonyesha njia. Katika maisha ya sasa hutakiwi kuwa na mwalimu mmoja yaani labda mwalimu wa kukushauri katika biashara tu hapana inabidi uwe na mwalimu wa biashara, familia na ndoa, mwalimu wa kipato n.k. Ni kweli bila mwalimu huwezi kusonga mbele. Lakini shida inakuja kuwa mwalimu anatafutwa, mwalimu haji hivi hivi.

Pengine huna mwalimu sahihi kwa sababu unafanya mambo yasiyo sahihi, nani atakuwa tayari kukufundisha ikiwa unafanya mambo ya ajabu ajabu! Hivyo basi, usisingizie kuwa huna mwalimu mzuri mwalimu yupo au walimu wapo sema shida ni kuwa wewe ndiye mwenye mambo yasiyoweza kukufanya upate mwalimu.

Sina elimu ya kutosha; ni kweli hauna elimu ya kutosha pengine umeishia darasa la saba. Au haukupata bahati ya kuweza kusoma kabisa. Sasa nataka nikuulize ni wapi ambapo ulisoma au kuona au nani aliyekwambia kuwa mafanikio yanaendana na kiwango fulani cha elimu?

Hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya elimu unayoisema wewe ambayo ni ya darasani na mafanikio. Kama ingekuwa hivyo basi maprofesa na wenye digrii wote wangekuwa na mafanikio lakini mambo yako tofauti hawana mafanikio na hii inamaanisha kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya elimu hiyo unayoisema na mafanikio. Hivyo basi elimu sio kigezo cha wewe kutokufanikiwa.

Nitaanza kesho; kwanini hutaki kuanza leo! Kesho ni lini? Kuna watu huwa wanasema kesho huwa haifiki, wengine husema liwezekanalo leo usingoje kesho. Hivyo basi jijengee mazoea ya kutaka kufanya leo na siyo kesho.

Nitafanya kesho huwa ni kisingizio kikubwa sana miongoni mwetu na ambacho kinaturudisha nyuma kila siku. Achana na kauli ya nitafanya kesho mara moja kama unataka kufanikiwa kiuchumi.

Kama kuna kauli ulikuwa unatumia na ukiamini kuwa ni njia sahihi na ni halali wewe kuzitumia kama kinga yako pale ambapo unakuwa hujatekeleza jambo fulani au umeshindwa kufanya jambo fulani ni wakati sasa wa wewe kubadilika na kuziacha kauli hizo mara moja.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom