Kuna wakati unaamka na kuhisi hofu isiyoelezeka. Hofu ya kuona watu waliokuwa sauti ya jamii wakitoweka taratibu kwenye macho ya umma, halafu maisha yanaendelea kana kwamba hakuna kilichotokea. Hiyo ndiyo hisia ninayopata kila ninaposikia kuhusu watu tunaoweza kuwapoteza kimya kimya, halafu tukalia kwa wiki moja mitandaoni na baadaye tukawasahau.
Tumeshuhudia mara nyingi namna Watanzania wanavyoguswa na jambo kwa muda mfupi. Mitandao huwaka moto, watu huandika “haki itendeke”, video husambazwa kila kona, majina hutrend kwa siku kadhaa. Lakini kadiri muda unavyopita, ukimya huanza kutawala. Watu hurudi kwenye maisha yao ya kawaida, mada mpya huibuka, na waliokuwa wakizungumziwa hubaki historia ya muda mfupi.
Hali hii inanipa maumivu hasa ninapofikiria kuhusu watu kama Polepole, Mdude, na wengine ambao leo hawajulikani walipo au hali zao zimezungukwa na sintofahamu. Kinachoumiza zaidi si tu kutoweka kwao kwenye mjadala wa umma, bali ni namna jamii inavyozoea haraka kusahau.
Taifa lisipojifunza kukumbuka, linaanza kupoteza utu wake. Kwa sababu ukimya wa leo unaweza kuwa kilio cha kesho kwa mtu mwingine. Leo tunamtazama mwingine akiwa kwenye sintofahamu, kesho inaweza kuwa ndugu yetu, rafiki yetu, au hata sisi wenyewe.
Mitandao ya kijamii imekuwa sehemu ya kuonyesha hisia kwa haraka, lakini mara nyingi hisia hizo hazidumu. Tunaandika kwa hasira, tunalalamika kwa uchungu, lakini baada ya muda tunachoka. Hapo ndipo nguvu ya mifumo inayotaka watu wasahau inaposhinda. Kwa sababu jambo likisahaulika, hata haki yake hupoteza uzito.
Kuna umuhimu mkubwa kwa jamii kujenga utamaduni wa kufuatilia mambo hadi mwisho badala ya kuhamasika kwa muda mfupi. Haki haipaswi kuwa trend ya siku mbili. Maisha ya watu na usalama wao si mada za kuburudisha hadhira mtandaoni.
Ninaposema sina amani, si kwa sababu ya hofu binafsi pekee, bali ni kwa sababu ya kuona jamii inayoweza kuumia leo, kulia kesho, na kusahau kesho kutwa. Hilo ni jambo la kujiuliza kwa kina: Je, tunawathamini watu wetu kwa dhati, au tunaguswa kwa muda tu kabla ya kuendelea na maisha?
Taifa imara si lile lisilopitia changamoto, bali ni lile lisiloruhusu sauti za watu wake zipotee gizani bila majibu. Tunahitaji kujifunza kukumbuka, kuuliza, kufuatilia, na kusimama pamoja hata pale kelele za mitandaoni zinapopungua.
Kwa sababu jamii inayosahau haraka, hujenga mazingira ya kila mmoja kuishi kwa hofu ya kusahaulika kesho.