SoC01 Hoja tano (5) za kinabii zitakazosaidia kukemea pepo la rushwa nchini Tanzania

SoC01 Hoja tano (5) za kinabii zitakazosaidia kukemea pepo la rushwa nchini Tanzania

Stories of Change - 2021 Competition
Joined
Sep 6, 2021
Posts
24
Reaction score
111
Na Elivius Athanas.
0745937016.

Neno "Rushwa" linaweza kuelezwa na kufafanuliwa kwa tafsiri tofauti tofauti, lakini tafsiri rahisi na nyepesi ya neno rushwa, ni kitu au fedha inayotolewa kwa mtu mwenye mamlaka fulani ili kufanikisha jambo fulani la mtu.
Kwa mantiki hiyo, rushwa ni njia ya mkato katika kutimiza jambo fulani baina ya mhitaji na mtu mwenye mamlaka fulani. Rushwa ni kosa kwa mjibu wa Sheria zetu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mtoa rushwa au mpokea rushwa wote ni wakosaji kwa mjibu wa sheria zetu za kupambana na rushwa. Hivyo, watakuwa hatarini kutozwa faini au kutumikia kifungo kwa mda fulani kulingana na kosa husika.

Rushwa imekuwa ni tatizo kubwa sana katika Mataifa mengi Duniani, hasa Nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Chimbuko la kushamiri kwa vitendo vya rushwa katika Nchi nyingi hasa Tanzania, linachagizwa na mambo kadha wa kadha kama vile umasikini, tamaa, mishahara midogo, wahitaji kutokidhi vigezo vya kazi, ugumu wa kupata ajira na kadhalika.
Sababu zote hizo huchochea moto ukuni wa rushwa kushamiri sehemu mbalimbali za kazi, maofisini, viwandani, majumbani na sehemu zingine za riziki.

Rushwa ya ngono katika sehemu za kazi umekuwa ni ugonjwa sugu ambao unawakumba vijana wengi hasa wa kike, wanapoenda maofisini na sehemu zingine za kazi kutafuta riziki.
Wasichana wengi wamekuwa wakikutana na kadhia hii wanapoenda kutafuta kazi maofisini na viwandani.

UFANYEJE UNAPOOMBWA RUSHWA YA NGONO?

Mtu yeyote anayekutana na kadhia ya kuombwa rushwa ya ngono ili afanikishiwe jambo fulani, anatakiwa kupeleka taarifa kwenye Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) ili hatua na uchunguzi ufanyike. "Kifungu namba 39(1) cha Sheria ya kupambana na Rushwa kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2007.

ADHABU YA MTU ALIYETHIBITISHWA KUOMBA RUSHWA YA NGONO NI IPI?

Adhabu ya mtu aliyefanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa kuomba rushwa ya ngono ni faini ya shilingi milioni tano (5) au kwenda miaka mitatu (3) jela au vyote kwa pamoja.

Baada ya utangulizi huo mfupi kuhusu maana ya rushwa na elimu kidogo kuhusu rushwa ya ngono, nijikite sasa katika kufafanua kichwa chetu cha habari kinachonitaka kufafanua hoja tano zitakazosaidia kupunguza tatizo la rushwa Nchini Tanzania.
Kwa kifupi, ninaenda kuyaangaza mambo ambayo yakifanyika au kurekebishwa, yatasaidia sana kupunguza tatizo la rushwa Tanzania.

Moja, tumkunje samaki angali mbichi. Mafunzo na elimu ianze kutolewa kwa watoto wadogo ili kuufanya ubongo na akili ya mtoto kukua akijua kuwa, rushwa ni dhambi kama zilivyo dhambi zingine.
Tunataka mtoto akifika umri fulani wa kuombwa rushwa aseme kuwa baba alinikataza au mwalimu alinikataza.
Elimu ianze kutolewa kuanzia shule za Awali, Misingi na Sekondari ili kujenga kitu kwenye akili ya mtoto kuogopa rushwa.
Kutoa elimu ya rushwa ukubwani ni sawa na kumuelimisha msichana mwenye ujauzito (mimba) kuwa asifanye ngono atapata mimba. Unakuwa ushachelewa kwani tayari ni mjamzito.
Vikundi vya rushwa viundwe na kuimarishwa toka ngazi ya chini. Walimu wetu wawakanye wanafunzi kuhusu rushwa na madhara yake kwa uzito.
Wazazi majumbani pia watoe elimu ya kutosha kwa watoto wao kuhusu rushwa na madhara yake. Wawaeleze madhara ya rushwa kwa staili ambayo mtoto ataiona rushwa kama laana.
Elimu yote hiyo ya shuleni na majumbani kwa watoto kuhusu rushwa, itasaidia sana kupunguza tatizo la rushwa.
Uimara wa nyumba ni msingi, tujenge msingi mzuri kuanzia kwa watoto.

Pili, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), itengewe bajeti (fedha) za kutosha. Fedha zinazokuwa zinatengwa kwa ajili ya chombo hiki muhimu cha kutokomeza rushwa, hazikidhi mahitaji ya chombo hiki kwa asilimia miamoja (100%).
Takukuru kama Taasisi, inahitaji kupewa fedha zinazokidhi mahitaji ya chombo hicho kwa asilimia zote. Kutoa pesa zisizokidhi mahitaji ya Takukuru kwa asilimia miamoja, kunafanya baadhi ya mipango na mahitaji ya chombo hiki kutokamilika.
Takukuru inahitaji kujenga ofisi zake kila Wilaya, inahitaji kuendesha mikutano, vikao na kadhalika. Bajeti ya kutosha itasaidia kutimiza mahitaji hayo hivyo kufanya Takukuru kufanya kazi zake kwa ufanisi na matokeo.

Tatu, Serikali na Taasisi binafsi zitoe mishahara inayokidhi mahitaji muhimu ya wafanyakazi ili kuepusha njaa ndogondogo zinazosababisha rushwa.
Japo binadamu hariziki lakini mishahara inayokidhi mahitaji muhimu ya wafanyakazi, itasaidia kupunguza njaa ndogondogo zinazowashawishi wafanyakazi kuomba rushwa.
Mfanyakazi anayekuomba rushwa ndogo kama vile elfu tano (5000) bila shaka huyo anahitaji hela ya kula au nauli. Huwezi kuomba rushwa ya elfu tano ili ukanunue gari. Hivyo, kuwapa wafanyakazi pesa inayokidhi mahitaji yao muhimu, kutapunguza tamaa ya wao kuomba rushwa.

Nne, wananchi watoe taarifa wanapokutana na kadhia ya kuombwa rushwa kwani ukimya unachochea rushwa.
Wananchi wengi hawana utamaduni wa kuripoti matukio ya kuombwa rushwa hivyo kupelekea matukio haya kushamiri.
Ukimya umekuwa ni sababu ya tatizo la rushwa kupamba moto.
Watoto wa kike wanaombwa rushwa kila uchao na wanakaa kimya.
Wazazi wengi wanaombwa rushwa na hawasemi.
Wagonjwa na watu wengine wanaombwa rushwa lakini hawasemi.
Tukiendelea kutotoa taarifa, TAKUKURU watajuaje?
Nina mfano wa kiwanda kimoja hapa Temeke, ilikuwa kila binti anayekuja kuomba kazi pale wanamuomba rushwa ya ngono. Siku moja binti mmoja akaenda kutoa taarifa, TAKUKURU wakafika pale kumchukua mhalifu kwa ajili ya uchunguzi na mahojiano. Kuanzia hapo, tabia hiyo ikakoma pale kiwandani.
Tuache ukimya.

Tano, Mahakama ya wala rushwa na mafisadi iwe "Mahakama Vitendo" isiwe "Mahakama Jina". Tunataka kuona wala rushwa wanakamatwa, kuchunguzwa na kufungwa.
Wala rushwa wakifungwa, watafanya watu wengine kuogopa kula rushwa.
Mafisadi wakifungwa, itasaidia watu wengine kuogopa ufisadi.
TAKUKURU iongeze makali. Viongozi wanaosema mafisadi tunawajua, wahojiwe ili wataje mafisadi hao.
Na wahakikishe wala rushwa wanachukuliwa hatua kali kwa mjibu wa sheria.
Jambo hili litasaidia watu kuogopa kujihusisha na rushwa.

MWISHO, HOJA YA KINABII.

Makanisa na Misikiti kupitia Wachungaji, Manabii na Mashekhe, wajitahidi kukemea rushwa kwa kuwahubiri waumini wao kutojihusisha na vitendo vya rushwa.

Amina.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom