esther mashiker
JF-Expert Member
- May 29, 2018
- 616
- 552
TIMU ya Soka ya Taifa ya Vijana ya umri chini ya miaka 17 maarufu Serengeti Boys itakuwa mwenyeji wa Fainali za Afrika kwa umri huo zitakazofanyika hapa nchini kwa mara ya kwanza .
Fainali hizo zinazosimamiwa na kuandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinatarajiwa kuchezwa kuanzia Aprili 14 hadi 28 mwaka huu. Hii ni mara ya pili kwa Serengeti Boys kushiriki fainali hizo, mara ya kwanza ilikuwa mwaka juzi huko nchini Gabon.
Kwa sasa kikosi hicho cha Serengeti Boys kiko jijini Kigali kikishiriki mashindano maalumu ambayo yanajumuisha timu za nchi tatu ambazo ni pamoja na wenyeji Rwanda na Cameroon. Katika kuhakikisha kuwa Serengeti Boys inaingia katika mashindano hayo ikiwa imara, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ametangaza kuwapatia kiasi cha Sh. bilioni moja.
Kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na Rais Magufuli, ni maalumu kwa ajili ya kukiandaa kikosi cha timu hiyo ili kiweze kufanya vema katika fainali hizo. Rais Magufuli anataka kuona wenyeji wanakuwa imara na kupata matokeo mazuri katika mechi zote watakazocheza kwenye fainali hizo na si kuwa wasindikizaji.
Huo ni mwanzo, timu hiyo ambayo inahitaji kuweka kambi Ulaya, vifaa vya michezo na posho za wachezaji pamoja na viongozi, inahitaji fedha zaidi ili iweze kutimiza malengo yake.
Inafahamika wazi kuwa mbali ya heshima ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, timu nne zitakazofanya vema zitakuwa zimekata tiketi ya kushiriki katika Fainali za Dunia za Vijana zijazo ambazo zitafanyika Peru.
Katika mpira hakuna miujiza, timu itakayojiandaa vema, wachezaji watakaojituma na watakaoshinda mechi zao, ndio wana nafasi kubwa ya kutimiza malengo ya kucheza fainali hizo za dunia. Rais Magufuli ameanzisha safari, huu ni wakati kwa kampuni, taasisi na wadau wengine wa ndani na nje ya Tanzania kujitokeza kuichangia Serengeti Boys ili iweze kutimiza ndoto zake.
Kwa pamoja hakuna kisichowezekana, Serengeti Boys inahitaji mchango wa kila Mtanzania ili iweze kutekeleza malengo yake na kikubwa ni kuitangaza nchi. Nipashe inaamini kuwa, kufanya vema kwa Serengeti Boys ndio kutasaidia kulitangaza jina la Tanzania katika medani mbalimbali za kimataifa na kutaongeza pato la uchumi kwa wageni watakaokuja nchini.
Huu ndio wakati sahihi wa kushiriki katika kuiimarisha timu hiyo na si kusubiri baadaye kuanza kuikosoa au kuiponda endapo itapata matokeo yasiyofurahisha. Kama nguvu ziliweza kuunganishwa na hatimaye Timu ya Taifa (Taifa Stars) kufanikiwa kukata tiketi ya kucheza Fainali za Afrika zitakazofanyika Juni, mwaka huu (AFCON 2019), pia inawezekana kuhakikisha ndoto za Tanzania zinatimia kwa kucheza Fainali za Dunia za Vijana kwa mara ya kwanza.
Umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, Watanzania huu ni wakati wa kujitoa kuhakikisha timu zetu zote za Taifa ikiwamo ye wanawake (Twiga Stars) zinafanya vema katika mashindano mbalimbali ambayo zitashiriki.
SOURCE NIPASHE