Hongera Simbu; Lakini riadha Tanzania tunakwama wapi?

Hongera Simbu; Lakini riadha Tanzania tunakwama wapi?

MamaSamia2025

JF-Expert Member
Joined
Mar 29, 2012
Posts
14,588
Reaction score
32,361
HONGERA SIMBU. TAIFA TUJITAFAKARI UPYA KWENYE RIADHA

Nawasalimu kwa jina la Chama Cha Mapinduzi.

Leo nina furaha kiasi na huzuni pia. Ninaandika kwa furaha baada ya kijana wetu Alphonce Simbu kushika nafasi ya 7 kwenye mbio za marathon za olimpiki huko Tokyo, Japan, akimaliza kwa muda wa masaa 2:11:35. Pia mwanadada Failuna Abdi akishika nafasi ya 24 kwa muda wa masaa 2:33:58 huku Gabriel Geay akishindwa kumaliza. Kwangu mimi nimeona vijana wamepambana hivyo nawapongeza nikiwa na furaha. Kiukweli hizi mbio zilikuwa ni ngumu. Nitafafanua zaidi kwenye aya zinazofuatia.

Pia nimehuzunika kuona nchi yetu ikiwakilishwa na wanariadha watatu tu wakati riadha ina mambo mengi mno. Kuna mbio za mita 100, 200, 400, 800, 1500, 3000, 5k, 10k, 21k na 42k. Kuna kuruka viunzi, tufe, mkuki nk. Kiukweli hii ni huzuni. Lakini hata ingekuwa ni wachache basi tungekuwa na washiriki angalau wa 5k, 10k, 21k na 42k. Hizo mbio nne zimetawaliwa sana na waafrika wakiwemo ndugu zetu wakenya na waganda. Hakika hili suala la washiriki watatu limeniuma sana. Ila nawapongeza sana shirikisho la riadha kwa kutokuwa na mambo ya ajabu ya kupeleka viongozi wengi olimpiki kuliko wachezaji. Kuna wakati jumuiya ya madola walienda viongozi 20 halafu wachezaji 10. Usishangae ndo bongo yetu hii.

Baada ya kurasa mbalimbali mitandaoni kuanza kuripoti matokeo haya ya watanzania wenzetu nikakutana na maoni mbalimbali kuhusu matokeo, olimpiki na riadha kwa ujumla. Comments chache zilikuwa za kisomi na chanya. Maoni mengi sana yalikuwa toka kwa akili ndogo yaliyojaa hisia kali zisizo na kichwa wala miguu. Kiufupi wengi walitoa maoni ya kisiasa bila kuwa na uelewa wowote kuhusu riadha wala olimpiki.

Nilisikitika kuona watu wana uelewa mdogo halafu wanakazana kulaumu serikali ya chama pendwa bila facts. Wengine wakalaumu wanariadha, shirikisho la riadha, BMT hadi waziri husika. Mimi nikaona kuna haja ya kuandika jambo na kuelimisha watu. Hizi akili nyingi nilizojaliwa bora nizitumie kwa manufaa ya taifa wakati huu nikiwa hai. Hivyo nawasihi wote msome kwa makini huu uzi na kama mna maswali mtauliza nitajibu kwenye comments.

Baadhi ya watu wamewatupia lawama wanariadha kwamba wamezidisha visingizio vya kutoleta medali. Wengine wakaenda mbali na kutamka kwamba ni bora kusimama na komredi Simba Dangote kuliko kushabikia mambo mengine. Hawa huenda wana hoja kiasi chake ila bahati mbaya hili ni kundi kubwa lisilojua chochote kuhusu riadha. Kiufundi hakuna sababu ya kumlaumu mwanariadha anayeweza kumaliza mbio. Wawakilishi wetu wawili walimaliza na mwingine mmoja hakuweza. Nafasi walizopata Alphonce na Failuna ni za juu mno kwa sababu ya uzito wa mbio zenyewe.

Kiufundi marathon ya kwenye olimpiki mwaka huu ilikuwa ni ngumu kwa washiriki wote. Mshindi wa mbio hizo kwa muda wa masaa 2:08:38 ambaye pia ni mwenye rekodi ya dunia kwa mbio za marathon, Mkenya Eliud Kipchoge hakuweza kuisogelea rekodi yake dunia. Ikumbukwe Eliud Kipchoge aliweka rekodi ya masaa 2:01:39 huko Berlin tarehe 16 September 2018. Utaona tofauti ya dakika 5 nzima kwa bingwa huyo. Hata kwa upande wa wanawake hakukuwa na urahisi. Mdogo wetu Failuna alikuwa akipambana na manguli wa marathon kidunia. Mshindi wa pili kwa muda wa masaa 2:27:36 upande wa wanawake mwanadada wa kikenya Brigid Kosgei ambaye pia anashikilia rekodi ya dunia ya mwaka 2019 huko Chicago kwa muda wa masaa 2:14:04 hakuweza kuisogelea kabisa rekodi yake. Huo ni ushahidi mmoja kuashiria mambo hayakuwa marahisi.

Tukiachana na waliotoa lawama kwa wachezaji kuna hawa ambao wako kisiasa na kudai kwamba kina Alphonce walipewa nafasi kimagumashi na wanaostahili kuachwa. Hawa pia ni kundi kubwa lisilojua chochote kuhusu riadha. Huenda kama hata olimpiki ijayo pale Paris hawahawa kina Simbu wakaendelea kutuwakilisha. Nitaeleza kwanini. Kwa wasiojua ni kwamba ili uweze kushiriki mbio za olimpiki lazima uwe na vigezo na sio kujuana. Kigezo kikuu ni kuwahi kushiriki mashindano yanayotambuliwa na shirikisho la riadha la dunia na kuweza kufikisha muda uliowekwa kama kigezo cha kushiriki olimpiki. Kwa mfano ili ushiriki Olympic marathon lazima uwe umekimbia kwa muda usiozidi masaa 2:11:30 kwa wanaume na masaa 2:29:30 kwa wanawake. Na huo muda uwe umepatikana kwenye mbio zinazotambuliwa na shirikisho la riadha la dunia. Muda bora kabisa wa Simbu kabla ya olimpiki ni masaa 2:08:27 kwenye Lake Biwa Marathon, Japan tarehe 10 March 2019. Kwa upande wa Failuna muda wake bora kabla ya olimpiki ni masaa 2:27:55 kwenye Haspa Marathon, Hamburg tarehe 28 April 2019. Kwa ushahidi huo utaona kabisa hawa washiriki walikuwa wana vigezo na walikuwa hawakwepeki kwenye kushiriki olimpiki. Kuwaacha hawa ingekuwa ni kashfa kwa viongozi wa riadha Tanzania. Na pia wale waliohoji kwanini washiriki wawe wachache ni kwamba hakukuwa na wanariadha wengine walioweza kufikia muda uliowekwa kwenye mashindano yanayotambulika na shirikisho la riadha la dunia.


Wale wanaolaumu serikali kwamba haikujihusisha na maandalizi ya wanariadha ni wa kupuuzwa. Serikali ya Chama Cha Mapinduzi iliwezesha kambi ya olimpiki huko Arusha kwa kuhudumia kila kitu na vilevile kulipa safari kwenda na kurudi. Pia serikali ya CCM ilihakikisha wanariadha na viongozi wanashonewa suti kali. Pamoja na huduma za serikali lakini pia waandaaji wa mashindano ya olimpiki hutoa fungu kupitia kamati ya olimpiki kugharamia maandalizi ya timu. Miaka iliyopita hizi pesa zilileta mgogoro kati ya komredi Gidabuday na Mzee Filbert Bayi.

Baada ya kujibu baadhi ya sintofahamu zilizojitokeza sasa tujiulize nini kifanyike ili kufanya vizuri zaidi? Aya kadhaa chini zitaelezea maoni yangu. Hakuna mtanzania anayeridhika kuona nchi yenye watu zaidi ya milioni 50 ikiwakilishwa na watu watatu wakati olimpiki imesheni michezo mingi sana. Kwa upande wangu naona jambo la kwanza ni serikali kuamua kuwekeza zaidi mashuleni ili kupata vipaji fresh vya kudumu. Hawa wanamichezo wa kuwachukulia mitaani huwa wanakuwa na tatizo la umri. Hata kama akidanganya umri bado hataweza kulazimisha kuendelea na mapambano.. umri ukifika mwili unagoma. Faida ni nyingi mno za kukuza vipaji. Wengine mtaelezea.

Chama Cha Mapinduzi kiboreshe viwanja vyake vya michezo. Hii iko wazi kwasababu CCM ndo mmiliki wa karibu viwanja vyote vikubwa nchini. Kama haina fungu itafute mwekezaji ili tupate viwanja vyenye ubora na vinavyoweza kutumika kwa michezo yote. Nashangaa UVCCM kutoweza kulifanyia kazi hili suala. Hii ni aibu kwa jumuiya ya vijana. Hatutaweza kukuza vipaji kwenye miundombinu mibovu.

Chama cha riadha kifanye jitihada kuboresha hizi marathon zilizofanyika sehemu mbalimbali nchini ili ziweze kutambulika na shirikisho la riadha duniani. Utitiri wa Marathon zisizo na manufaa kiufundi inakuwa haina maana. Majuzi hapa nimeshangazwa na marathon za kuwania ng'ombe. Siasa ziepukwe kwenye riadha. Sijui kama kuna mbio zingine hapa nchini zinazotambuliwa na shirikisho la dunia ukitoa Kilimanjaro Marathon.

Wanariadha nao waweke juhudi zaidi kwenye kazi yao. Muda wa mwanariadha kuwa vizuri huwa ni mfupi lakini unaweza kurefushwa endapo mwanariadha mwenyewe na kocha wake watakuwa na nidhamu kwenye kazi yao. Wanariadha wawekeze hela nyingi kwenye miili yao ili kuepusha injuries na mambo mengine ya kuharibu mwili.

Nina mengi ya kuandika ila naishia hapa na kukaribisha maoni.

NB: Mwandishi ni kada wa CCM anayeunga mkono fikra za mwenyekiti.
 
Sahv wasani wa bngofleva ndiyo wanaonekana
Watu wa muhimu,mondi,kba,knde,nndy etseteraa

Ova
 
Sahv wasani wa bngofleva ndiyo wanaonekana
Watu wa muhimu,mondi,kba,knde,nndy etseteraa

Ova
Yaani Mzee wa Kinondoni hawa watu wa riadha wana mawe hatari sema wako Low Profile kupindukia. Hawa kina Simbu karibu airports kubwa zote duniani wamepita. Mtu kama Simbu baada ya kuwa wa saba kwenye olimpiki atapata mikataba minono ya makampuni kama Nike, Adidas na wengine. Tatizo ni kama hawaeleweki hivi.
 
Uwekezaji kwenye michezo ni lazima ili tulete matokeo chanya.
Hii Marathon ya kugombea ng'ombe ni kubwa kuliko😂😂😂
Hongera kwa waliotuwakilisha
Nalog off
 
Inapendeza na kila la kheri kwa team Tanzania...
 
Back
Top Bottom