Hotuba ya kukubali tunzo

Hotuba ya kukubali tunzo

Pius B. Ngeze

New Member
Joined
May 30, 2011
Posts
2
Reaction score
3
Private Office

P.O. Box 1222, Bukoba, Tanzania
Tel/Fax 028 222083
E-mail: ngezep@yahoo.co.uk
Mob: Mob.0784 690277 & 0768 023019

HOTUBA YA KUKUBALI TUNZO (“THE SOKOINE UNIVERSITY OF AGRICULTURE AWARD FOR DISTINGUISHED CONTRIBUTION IN ADVANCEMENT OF AGRICULTURE IN TANZANIA” FOR THE YEAR 2011/2012)
Mhe. Mkuu wa Chuo,Mhe. Mwenyekiti wa Baraza la Chuo,Wahe. Wajumbe wa Baraza la Chuo,Wahe. Viongozi wa Chuo,Wanachuo na Wahitimu,Wahe. Wageni Waalikwa,Mabibi na Mabwana, Naomba nianze na shukrani. Kwanza, ninamshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ni muweza yote na ambaye bila yeye nisingeweza kufika hapa nilipo. Pili, nawashukuru Wazazi wangu, marehemu baba Michael Bujiji Ngeze na mama Fides Nankwene, kwa kunipeleka Shule ya Msingi mwaka 1954, kunilea, kunihimiza na kunisaidia kwa hali na mali mpaka kuhitimu elimu ya Chuo Kikuu, mwezi Machi 1970. Tatu, ninawashukuru sana Watanzania wote kwa kugharamia elimu yangu kuanzia elimu ya Sekondari hadi Chuo Kikuu, maana bila kodi yao nisingepata elimu hiyo. Nne, naishukuru sana familia yangu kwa kunitia moyo na kunisaidia kwa hali na mali: wake zangu marehemu Alice Mwakasaka na Rachel Wizeye na watoto wetu Katarina Balankunda, William Niyongoma, Fides Shimilimana, Flavia Niyikiza na Maria Niyimbona. Tano, nawashukuru sana watu wote walionisaidia kuandika vitabu nilivyoviandika. Hawa ni pamoja na wakulima, maofisa ugani, Vituo vya Utafiti wa Kilimo, watafiti, wasomaji wa miswada, wahariri, makampuni ya uchapishaji na mitandao mbalimbali ya intaneti.
Shukrani kwa Chuo Kikuu (SUA)
Mhe.Mkuu wa Chuo,Kwa namna ya pekee, ninakishukuru Chuo cha Sokoine cha Kilimo kwa kuniteua kupewa Tunzo hii kwa mwaka wa Chuo wa 2011/2012 kwa kutambua mchango wangu mahususi kwa maendeleo ya kilimo nchini. Nami naipokea kwa heshima na unyenyekevu mkubwa. Kwangu leo ni siku ya pekee na ya furaha kwa kuweza kupokea Tunzo hiii mwenyewe nikiwa hai. Katika maisha yangu, hii ni Tunzo ya pili, lakini, ndiyo kubwa. Tunzo ya kwanza nilipewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) mwaka 2005 ya "Mwandishi Bora wa Vitabu vya Taaluma Vilivyoandikwa kwa Kiswahili.” Ninafurahi na kushukuru kuwa Tunzo hizi mbili ni katika fani niliyoipenda tangu utotoni, nikaisomea na kupata Shahada ya Kwanza katika fani hiyohiyo – Digrii ya Sayansi ya Kilimo miaka 42 iliyopita.
Makala yangu ya kwanza kuchapishwa
Mhe. Mkuu wa Chuo,Makala yangu ya kwanza kuchapwa tangu kuzaliwa kwangu, katika Jarida la The East Africa Reporter mwaka 1969, ilihusu kilimo. Wakati huo nilikuwa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Makerere, Uganda, kikiwa ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki. Makala yenyewe ilihusu “Ndizi: Chakula Kikuu cha Wahaya (kabila kubwa na wala ndizi katika Mkoa wa Kagera).” Makala hiyo ilipochapishwa nilifurahi sana.
Miaka 42 ya uandishi wa vitabu 54 vya kilimo
Mhe. Mkuu wa Chuo,Baada ya kuhitimu Shahada hiyo ya Kwanza, mwezi Machi 1970, nilijiuliza, “Watanzania waliogharamia elimu yangu ya Chuo Kikuu wataifaidi vipi?” Katika kujibu swali hilo, nikaamua kuwaandikia vitabu vya kilimo katika Kiswahili, ingawa ninakielewa vizuri Kiingereza, ili wakulima na Watanzania wengi waweze kufaidi elimu yangu waliyoigharamia, kwa kusoma vitabu vya kilimo vilivyoandikwa kwa lugha wanayoijua, Kiswahili. Mhe. Mkuu wa Chuo,Mara baada ya kurudi nchini kutoka Uganda, mwezi Machi 1970, na kuajiriwa na Wizara ya Kilimo, Makao Makuu, nikaanza kuandaa miswada miwili ya vitabu. Muswada wa kwanza niliuita Ushirika Tanzania. Nikaupeleka Tanzania Publishing House. Wakaona unafaa kuchapishwa kitabu na kikatoka mwaka 1975. Kitabu hiki, kikiwa na kurasa 166, kikawa cha kwanza nchini kuandikwa katika eneo hili kwa Kiswahili na kuchapishwa. Kitabu hiki ni utafiti wa Historia ya Ushirika nchini tangu miaka ya 1920 hadi 1976: kuanzishwa kwake, aina, kukua, maendeleo na matatizo ya ushirika nchini. Toleo la pili lilitoka mwaka 2010. Kitabu changu cha pili kiliitwa Misingi ya Kilimo Bora, nacho kilichapishwa pia, na Tanzania Publishing House mwaka 1976, kikiwa na kurasa 184. Kitabu hiki kilipokelewa vizuri na Watanzania na Wizara ya Elimu ikakipatia Ithibati na kuanza kutumika katika Shule za Msingi na Vyuo vya Ualimu, kama kitabu cha ziada na marejeo. Mhe. Mkuu wa Chuo, Kuchapishwa kwa vitabu hivi viwili kulinitia moyo na hamasa ya kuandika vitabu juu ya kilimo kwa kutumia Kiswahili. Leo hii ninapopokea TUNZO hii, nimeandika vitabu 54 juu kilimo na vingine vinane (8) visivyo juu ya kilimo moja kwa moja. Jumla ni 62 na nimeviandika ndani ya miaka 42 (yaani, 1970 – 2012). Vitabu hivyo vipo na vinapatikana kutoka kwa Wachapishaji na Maduka ya Vitabu. Baadhi ya Wachapishaji katika nchi jirani, hususan Kenya, wameanza kuvitafsiri kwa Kiingereza kwa ajili ya watu wao. Swali tunalojiuliza ni iwapo Watanzania, na hasa wakulima, wengi nchini wameviona na wanasoma vitabu hivyo 54 juu ya kilimo bora cha mazao, ufugaji, ushirika, uhasibu, mazingira n.k. Jibu ni hapana, na sababu nitazieleza hapa chini.
Baadhi ya vikwazo kwa mapinduzi ya kijani nchini

Mhe. Mkuu wa Chuo,
Hapa nchini, kilimo kitaendelea kuwa tasnia muhimu sana kwa miaka mingi ijayo kama chanzo kikuu cha chakula, mapato na ajira kwa Watanzania zaidi ya milioni 45 waishio mijini na vijijini. Wakati uchumi wa taifa ukiongezeka kwa asilimia 6.5 – 7.0 kwa mwaka, ongezeko la uzalishaji wa kilimo uko chini sana. Hali iko hivyo licha ya nia njema ya serikali zote tangu tupate Uhuru. Walio wengi tunakumbuka matamshi na kaulimbiu kadhaa za kisiasa, kama vile Siasa ni Kilimo, Kilimo cha Kufa na Kupona na programu kabambe kadhaa kama vile ASDP, MKUKUTA, MKURUBITA, SAGGOT n.k., lakini, zote hazijaleta mapinduzi ya kijani haraka yaliyokusudiwa. Kwa sasa tuna Kilimo Kwanza, yenye lengo lilelile la kuleta mapinduzi ya kijani nchini. Kilimo Kwanza imetambua vikwazo kadhaa vya kilimo nchini na kubainisha nguzo 10 ambazo zikitekelezwa barabara tutashuhudia mapinduzi ya kijani nchini. Pamoja na nia nzuri ya serikali ya kuona uzalishaji wa kilimo nchini ukiongezeka mara kumi na zaidi na jitihada za SUA kuzalisha wahitimu wengi kila mwaka katika fani ya kilimo, naona vikwazo vingine vitano kwa ukuaji wa kilimo chetu. Kikwazo cha kwanza, ni uharibifu wa mazingira na mbadiliko ya tabianchi, mapacha yanayotegemeana. Watu wengi hapa nchini bado hawalioni kuwa tishio kubwa la kutuletea njaa, umaskini, janga na hata vifo. Tembelea mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, kama mfano, ushuhudie athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi kwenye kilimo. Barafu kwenye mlima Kilimanjaro inatoweka haraka na wakulima wadogo wa mikoa hiyo wanashuhudia athari mbaya sana kwenye kilimo chao ambazo hawajawahi kuziona maishani mwao. Mito ambayo huko nyuma haikuwahi kukauka, sasa inakauka. Katika baadhi ya wilaya za mikoa hiyo, kama vile Monduli, mvua hukosekana hata kwa miaka miwili mfululizo na maziwa, kama vile Ziwa Manyara, yanaendelea kukauka. Hali iko hivyo hivyo katika mikoa mingine mingi nchini, na hata iliyosalia inanyemelewa. Natoa mwito kwa serikali, taasisi na asasi mbalimbali kuongeza kasi katika kuwaelimisha wananchi juu ya suala hili na kuchukua hatua za kupunguza athari na kukabiliana na hali hiyo.Kikwazo cha pili, ni wahitimu wa kozi za kilimo nchini kutokuwa na utamaduni wa kujisomea vitabu vyenye elimu ya kilimo bora. Maofisa hawa ni wahitimu wa Vyuo Vikuu, SUA ikiwamo, na Vyuo vya kilimo nchini. Kutosoma vitabu ni kansa kwa Watanzania walio wengi sana. Hatimaye taifa ambalo wananchi wake hawana utamaduni wa kusoma litakuwa taifa la wajinga na mwisho wake siyo mzuri. Mwito wangu kwa Vyuo Vikuu vyote (SUA ikiwamo), vyuo vya aina mbalimbali, shule za sekondari na shule za msingi, ni kuwa lazima mkazanie kuanzisha "somo la kupenda kujisomea” ili wahitimu wenu wathamini kusoma, muwajengee mazoea na utamaduni wa kujisomea, maana elimu kubwa na inayokwenda na wakati hupatikana nje ya vipindi vya kuwa vyuoni na shuleni. Kuthibitisha rai hii, pamoja na kuzitumia orodha ya vitabu vya kilimo tulivyonavyo Halmashauri, kati Halmashauri za Miji/Manispaa/Majiji 156 ni 22 tu ambazo zimewahi kuagiza vitabu vya kilimo kwa ajili ya Vituo vya Elimu vya Kata, maofisa ugani, viongozi wao na wakulima. Je, hizo zilizobaki hazina maofisa wa kilimo ambao wanatambua umuhimu wa vitabu hivyo kama nyenzo ya kufanikisha Kilimo Kwanza katika maeneo yao? Aidha, tusisahau kuwa nchi hii ina watu wengi vijijini na mijini ambao wanajua kusoma na kuandika, na hivi sasa kila mwaka maelfu ya wahitimu wa shule za sekondari na shule za msingi hubaki vijijini na mijini bila ajira tofauti na kilimo au wasioendelea na elimu ya juu. Hawa wangekuwa na utamaduni wa kusoma vitabu vya kilimo na wakavipata, wangevutiwa kuanzisha kilimo, hivyo, kuchangia mapinduzi ya kijani nchini. Kikwazo cha nne, ni uwezo mdogo wa kifedha wa wakulima wetu, maofisa watendaji wa vijiji na kata, viongozi wao na hata maofisa ugani wa kununua vitabu vya kilimo. Hata kama wengependa kuvisoma, hawawezi kuvinunua! Natoa mwito kwa serikali, taasisi na asasi mbalimbali kubuni miradi itakayowawezesha kupata na kusambaza vitabu hivyo kwa wakulima, Vituo vya Elimu vya Kata na Maktaba za Vijiji/Kata kwa kupitia Halmashauri zao za Wilaya/Miji/Majiji. Kwa hakika, haina maana wala faida yoyote kuwapo nchini vitabu vya kilimo, lakini, walengwa haviwafikii ili wafaidike navyo. Kikwazo cha tano, ni serikali kutosaidia tasnia ya uchapishaji nchini. Miaka minne hadi sita iliyopita, hadi sasa, imeshuhudia kudorora kwa uchapishaji na biashara ya vitabu nchini. Hii ni kwa sababu soko kubwa la vitabu ni serikali. Isiponunua vitabu vya kupelekwa mashuleni, vyuoni, vijijini na taasisi nyingine, kama ilivyotokea katika kipindi hicho, matokeo yake ni wachapishaji kukwama na kujiondoa katika biashara hiyo. Inapokuwa hivyo na maduka mengi ya vitabu nchini hufungwa, na ndivyo imetokea. Hali hii ni tofauti na ilivyo katika nchi nyingine za Jumuia ya Afrika Mashariki, Jumuia ya SADC n.k. Hatari inayotukabiri Watanzania na taifa, ni kuwa tunaelekea kuwa soko la vitabu kutoka nchi jirani ambavyo viliandaliwa maalumu kwa ajili ya watu wao na si Watanzania! Natoa mwito kwa serikali kukabili haraka hali hii na kuokoa tasnia ya uchapishaji nchini. Tusipofanya hivyo, taifa litaangamia kielimu.
Huduma za Ugani katika kufanikisha Kilimo Kwanza
Mhe. Mkuu wa Chuo,Ili kuleta mapinduzi ya kijani nchini yaliyolengwa na Kilimo Kwanza, huduma za ugani ni za muhimu sana. Mpaka sasa tunaendelea kusikia matamshi ya kisiasa yanayolenga kuwashutumu maofisa ugani kuwa wanapenda kukaa maofisini badala ya kuwaendea wakulima ili kufikisha kwao teknolojia mpya ya kilimo. Kwa baadhi ya maofisa hao, shutuma hizo wanazistahili, lakini, kwa baadhi ni kuwaonea, maana ziko sababu kadhaa zinazowakwamisha. Ingefaa wasikilizwe kwanza, baada ya hapo hatua zinazofaa zichukuliwe dhidi ya wahusika. Kwa mfano, watafikaje huko bila kuwezeshwa kwa kupewa nyenzo za kutendea kazi, ikiwa ni pamoja na usafiri?
Mwito kwa wasomi nchini kuandika vitabu
Mhe. Mkuu wa Chuo Kikuu, Mbali na vitabu vya kitaaluma ambavyo ninaamini vyuo vinavyo, Watanzania wanahitaji na wanastahili kusoma vitabu vya aina mbalimbali vilivyoandikwa na Watanzania wasomi na vilivyoandikwa kwa Kiswahili sanifu. Vitabu vya aina hiyo si vingi kwa sasa. Kwa sababu hii, natoa mwito kwa wasomi wetu nchini kuviandika. Vitabu hivyo ni pamoja na vile vya kilimo. Kwa upande wangu, ninawaahidi Watanzania kuwa kazi niliyoianza miaka 42 iliyopita, nitaiendeleza ili niendelee kuchangia maendeleo ya nchi yangu kwa kuwarithisha sehemu ya elimu yangu waliyoigharamia na uzoefu walionipatia. Asanteni kwa kunisikiliza.

Pius B.NgezeMTUNUKIWA TUNZO

Hotuba hii imetolewa tarehe 23 Novemba, 2012 SUA Morogoro, Tanzania
 

Attachments

Ok tumeisoma, next........... Tuichallenge, tukubaliane nayo au ..........................
 
Back
Top Bottom