Hotuba ya mgombea binafsi kutangaza nia ya urais wa jamhuri ya muungano wa tanzania

Hotuba ya mgombea binafsi kutangaza nia ya urais wa jamhuri ya muungano wa tanzania

IsangulaKG

JF-Expert Member
Joined
Oct 14, 2010
Posts
706
Reaction score
386
Hotuba kwa walalahoi wenzangu kutangaza nia ya kugombea urais wa Tanzania

Ndugu Walalahoi wenzangu,

Kwanza nimshukuru mwenyezi Mungu ambaye kwa uwezo wake usiomithilika tumepata pumzi na nguvu ya kuweza kufika hapa. Natambua kuwa wengi wenu mmeiminya mifuko yenu ili kuweza kupata japo nauli ya kubanana kwenye vifodi na vikirikuu ili tupate nafasi ya kujumuika hapa, na kwa sababu hiyo nasema asanteni sana (makofi).

Kwanza kabla ya kuongelea fursa za kimaendeleo tutakazotengeza pamoja mtakapo nipa ridhaa ya kuwaongoza, nieleze kwa ufupi nini tafsiri ya kiongozi, tafsiri ambayo watangaza nia wenzangu ama wameifumbia macho ama hawaifahamu. Neno kiongozi limetokana na harakati za kivita miaka ya nyuma sana ambapo ‘kiongozi’ ni mtu ambaye alikuwa akisimama mstari wa mbele katika vita, mfano, mshika alama ya kutoa ishara kwa wenzake ili waanze mashambulizi. Kwa bahati mbaya, mtu huyu mara nyingi alikuwa wa kwanza kupata madhara yatokanayo na mashambulizi ya maadui mfano kifo.
Sisemi kuwa kila kiongozi lazima afariki katika kipindi chake cha uongozi bali hoja yangu ni kuwa uongozi ni UTAYARI wa KUBEBA DHAMANA YA MATARAJIO YA WALIO WENGI ambao , wewe kama kiongozi unatoa ishara ya wapi muelekeze harakati zenu na kwa pamoja, ili mzikabili changamoto mnazokumbana nazo. Hapa namaanisha kiongozi ni mtu aliyjitoa mhanga kwa gharama yoyote ile kuleta mafanikio ya wenzake na nchi yake na si kwa manufaa yake binafsi.

Ndugu walalahoi wenzangu,
Nchi yetu imegubigwa na wingu la usifadi. Tena, mafisadi wenyewe wana nguvu kubwa ya kifedha na kisiasa. Hapa ndipo kujitoa MHANGA kunapohitajika. Kiongozi anayefaa katika nchi hii ni yule ambaye yuko tayari kulifumua wingu hili AKISUKUMWA na nia ya kuleta ulinganifu wa kipato kwa wote hata kuhatarisha maisha yake kutokana na nguvu za mafisadi. Ni kwa sababu hii nimeamua kufanya kikao hiki hapa uwanja wa wazi wa jamii ili kuepuka kupewa misaada ya kifedha na wanaojiita marafiki zangu ambao matarajio yao yaliyojificha ni kutumia urafiki huo katika kufanikisha ajenda zao za kujinufaisha. (makofi)

Japo kuna mambo mengi sana ya msingi katika nchi hii ambayo naweza nisiongelee yote leo, utajiuliza kwa nini nimeanzia na nia ya kupambana na ufisadi. Matatizo mengi tuliyonayo ni kutokana na mikataba mibovu inayowanufaisha wachache, rushwa na usimamizi mbovu wa rasilimali za taifa katika ngazi zote. Kuna watu ambao wamejilimbikizia mifedha ambayo ingeweza kujenga mji wa kisasa, wakati ambao watoto wanazaliwa na kukua katika mazingira yaliyojaa ufukara vijijini, kiasi kwamba hawana ndoto ya kujiondoa katika umasikini toka wakiwa wadogo. Watangaza nia wenzangu wameligusia suala hili, lakini jiulize toka lini mafuta yakatumika kuzima moto uliosababishwa na kuwaka kwa mafuta? Watu hawa wanajisifu kwa 'uzoefu' walioupata katika kuitumikia serikali. Serikali ambayo ndiyo imetufikisha hapa tulipo na walikuwa na nafasi ya kuleta mabadiliko wakiwa ndani ya serikali. Sasa wanajifanya kama si sehemu ya serikali iliyotufikisha hapa. Wanataka kuturubuni kuwa ukipanda mbegu ya mahindi utavuna mpunga....
Pili, Serikali imekuwa ikilia kwa uhaba wa fedha lakini wapo viongozi ambao wana fedha kuliko hata bajeti za wizara. Ni kutokana na sababu hii, japo kuna mambo mengi ya kushughulikia katika nchi hii, vipaumbele vyangu ni mageuzi katika utawala, mageuzi katika elimu, sayansi na teknolojia, na mageuzi katika miundombinu.

Mageuzi katika utawala

Watangaza nia wenzangu wameongelea vipaumbele kama elimu, kilimo na kadhalika. Kwa imani yangu, huwezi kutekeleza vipaumbele vyovyote iwapo huna viongozi wenye maadili,wenye nia thabiti na waliojitoa mhanga kuwaondoa watanzania katika nchi ya kero na mahangaiko kwenda katika nchi ya ahadi.
Ni kwa sababu hii, lazima kwanza tufumue na kujenga upya mfumo wa utawala, badala ya kuimba tu utawala bora majukwaan. Kuboresha utawala si suala la kuwepo na sera tu nyingine hata hazitekelezi, bali kwa kuufumua na kuusuka upya mfumo wa uwajibikaji wa watwala. Ni lazima tuweke mfumo ambao utawezesha viongozi walioteuliwa au kuchaguliwa kupimwa utendaji wao siyo tu na waliowateua ama kuwachagua bali pia na watumiaji wa huduma wanazozitoa.

Ndugu walalahoi,
Mfumo wa kisiasa na kiutawala wa nchi hii umewapora mamlaka wananchi katika kuwawajibisha viongozi wao na kubaki na fursa moja tu ya uchaguzi wa kila baada ya miaka mitano. Hii ni hatari kwa taifa linalohitaji uwajibikaji yakini ili kusonga mbele. Ni kwa sababu ya kukosekana uwajibikaji thabiti na maendeleo ya kweli, wananchi hawaoni faida hata ya kulipa kodi.Ni kwa sababu hii kazi yangu ya kwanza si tu kuboresha mfumo wa uwajibikaji bali kutengeneza mfu wa kuwawajibisha watawala wasio wajibika.

Ili kuleta uhalali wa mifumo hii ni lazima kuboresha upya katiba kwa kupitia upya mchakato mzima wa katiba iliyopendekezwa. Kwa Imani yangu, katiba ya Tume ya Warioba ililenga kufumua mfumo wa kitawala na kuwarejeshea wananchi mamlaka ya kuwawajibisha viongozi wao. Hilo ndilo linalotakikana katika nchi hii. Asiwadanganyeni mgombea yeyote kuwa atawaletea maendeleo kwa mfumo huu uliopo wa kisiasa na kiuchumi.

Tunataka viongozi wawe na hofu ya wananchi, si hofu ya kufanyiwa jambo baya bali hofu ya kuondolewa katika nafasi zao iwapo wananchi hawajaridhika na utendaji wao. Kwa wale walioteuliwa, lazima kiwepo chombo kipya kabisa cha kikatiba kinachojitengemea chenye mchanganyiko wa wajumbe cha kupima uwajibikaji wa viongozi na watendaji wote wa serikali wote walioteuliwa au kuajiriwa. Kwa viongozi wakuu wa vitengo, chombo hiki kitawajibika kuwasilisha matokeo ya upimaji wa ufanisi kwa wananchi, bunge na mimi mwenyewe. Wananchi na bunge litatoa maoni yake na lazima hatua zichukuliwa stahiki zitakuchuliwa. Kwa viongozi wa ngazi za chini, wanachi watakuwa na nguvu ya moja kwa moja kuwawajibisha watendaji wa serikali na kisiasa.

Pili, nitahimiza uundwaji wa kikatiba wa chombo cha kibunge chenye kutathmini utendaji, michango na uwajibijaki wa wabunge. Chombo hiki kitapima ufanisi wa mbunge mmoja mmoja bungeni kutokana na michango yenye manufaa anayoitoa na utendaji katika jimbo lake na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni ni pamoja na kutoa nafasi ya kura ya kutokuwa na Imani na mbunge katika jimbo lake na kutoa mapendekezo stahiki. Wabunge watakaoonyesha ufanisi wa kuridhisha, pasipo kujali chama chao,ndiyo watakuwa na nafasi katika utendaji wa serikali. Ili haya yafanyike, lazima tuwe na katiba mpya inayohimiza uwajibikaji.


Mapinduzi ya Elimu, sayansi na teknolojia


Ndugu walalahoi wenzangu,
Mfumo wa elimu wa watanzania kwa sasa unatengeza 'wategemezi' wa ajira yaani waajiriwa na si waajiri. Jambo hili ni hatari kama kweli tunataka kupambana na suala la ajira.Ni lazima tuufumue mfumo huu ili kuwa na elimu inayohimiza ubunifu toka katika ngazi za awali. Tutanziaha mfuko wa mashindano ya kibunifu utakaowezesha ushindani wa wanafunzi katika ngazi za awali hadi chuo kikuu. Washindi wa ubunifu watapewa mikopo ya kukuza vipaji vyao katika maeneo husika. Kwa hali hii tutahimiza ufikiri wa wanafunzi na kuwezesha kuwa na akili ya kutatua matatizo ya kijamii kuliko tu kufikiria ajira. Pia, tutaweka mfumo na mitaala inayoruhusu wanafunzi kuwapa changamoto walimu wao katika mfumo wa kufundisha kwa mijadala badala ya kuwa kama waumini wa kupokea mahubiri bila kuuliza maswali. Kwa mfumo huu walimu watalazimika kujisomea mara kwa mara kujibu kwa ufasaha changamoto wanazopewa na wanafunzi wao.

Ndugu walalahoi wenzangu,

Hakuna nchi yoytote duniani iliyoendelea KIUCHUMI bila kuwa na uthamini NA UTHUBUTU wa mapinduzi ya sayansi na teknolojia. Tutaisuka upya tume ya sayansi na teknolojia ili kusimamia tafiti katika masuala ya kijamii na kuwezesha matumizi ya tafiti hizo katika mipango ya serikali. Chombo kitakachoundwa cha ubunifu kitashirikiana na tume ya sayansi na teknolojia kuendeleza ubunifu uliotambuliwa ili uweze kutumika kutatua changamoto za wananchi.
Ni jambo la kusikitisha kuwa katika karne hii bado wanachi wanatembea bila viatu. Ni lengo langu kuhimiza ubunifu na kutengeza tatuzi nafuu kwa changamoto za wananchi. Matumizi ya sayansi na teknolojia yataanzia katika ngazi za vijiji ambapo wananchi watahimizwa kuwa wabunifu katika kutatua changamoto zao. Kazi ya mfuko wa mashindano ya kibunifu si tu katika mashule bali pia katika ngazi za vijiji, kata, wilaya hadi taifa. Kila wilaya italazimika kutenga fungu la kuhimiza ubunifu na kushirikiana na chombo cha ushindani wa kibunifu kuhimiza ubinifu katika wilaya hiyo na kuweka mikakati ya kupanua ubunifu huo kwa manufaa ya wilaya na taifa kwa ujumla

Ndugu walalahoi wenzangu,
Kazi kubwa ya serikali ni kuweka mifumo ya kimiundo mbinu ili kuwawezesha wananchi kutimiza adhma zao za kimaendeleo. Lazima tuhimize matumizi ya komputa mashuleni na katika huduma zote za serikali pamoja na kuwezesha na kusimamia huduma bora za mawasiliano ya intaneti na simu ya uhakika kwa wananchi. Serikali iliyo pita ilijenga mkonga wa mawasiliano ambao faida zake kwa wananchi hazionekani. Tunataka wananchi waunganishwe na dunia ili waone wenzao wanavyokabiliana na changamoto na kujifunza jinsi ya kutatua changamoto zao badala ya kuwaficha mambo haya. Tunataka kuwa na mfumo wa kuunganisha nyumba na mtandao wa internet na simu. Ni kwa mfumo huu tutaberesha mawasiliano kati ya wananchi na vyombo vya serikali. Tunataka huduma za serikali zinazowezekana zitolewe kwa mitandao badala ya wananchi kusafiri umbali mrefu.

Pia, tutaanzisha mifuko ya barabara,mawasiliano, maji, afya,elimu na kilimo katika kila wilaya ili kusimamia ujenzi wa miundoombinu muhimu kama vile barabara, maji,vituo bora vya kutolea huduma za afya, madarasa na madawati na zana bora za kilimo.Ni jambo la kusikitisha kuwa kwa Zaidi ya miaka hamsini ya uhuru hakuna huduma yoyote ya uhakika katika nchi hii. Umeme si wa uhakika, maji hadi katikati ya jiji ni shida tupu na vijijini ndiyo usiseme.Tutaikarabati Tanroads ili kuleta mapinduzi ya barabara katika majiji na barabara zinazounganisha mikoa na wilaya zote. Tutaboresha miundo mbinu ya maji hasa kwa kutumia utajiri wetu wa maziwa na mito kutatua tatizo la maji. Tutaboresha huduma za afya kwa kubadili mfumo wa utoaji huduma za afya ili kuleata ushindani. Tutahimiza ushiriki wa vijana katika kilimo bora na cha kisasa, usindikaji na usafirishaji na uuzaji mazao.
Kwa ujumla,tutaongeza ushindani katika utoaji wa huduma zote za msingi kama vile umeme, maji na afya.

Pia, tutaweza taratibu kuwezesha makampuni na watu binafsi , kwa kuwapa upendeleo maalumu, kuwekeza katika nishati mbadala za umeme kama vile umeme upepo, umeme jua na kipaumbele kitatolewa kwa makampuni yanayolenga maeneo ya vijijini.

Tutafumua mfumo wa afya ili kuleta ushindani wa kihuduma, kufanya afya na elimu kuwa haki ya kila mtanzania, kutengeneza mifumo bora ya bima ya afya kwa watu wote, kuweka mfumo wa kupima ufanisi wa utendaji wa watumishi wa afya na elimu, utaratibu thabiti na bora wa kuwatunza wazee, ulinzi kwa watu waishio na ulemavu na kadhalika.

Kimsingi, Kila sekta, chombo, kampuni au mtu anayepokea ruzuku ya serikali ili kutoa huduma kwa wananchi atapimwa ufanisi na wananchi wenyewe na kuwajibishwa na serikali.

Ndugu walalhoi wenzangu,

Ni lazima tufanye mapinduzi ya vyombo vyetu vya usalama ili kuvifanya viwe na ufanisi wa kiutendaji na kuzuia uonevu uliopo sasa. Tutaweka mfumo imara wa wananchi kutoa maoni kuhusu ufanisi wa maaskari wetu na hatua stahiki kuchukulia. Nchi hii ni yetu sote na hakuna mtu mwenye haki ya kuwanyanyasa wengine. Hatutarushusu askari yeyote amnyanyase raia kwa asababu yeyote. Tutaweka utaratibu wa kupokea malalamiko ya raia kuhusu uonevu au unyanyasaji na hatua kuchukuliwa bila kumuathiri raia mwenyewe. Pia, ni imani yangu kuwa, ukuaji wa huduma wa intanet utawezesha wananchi kufichua maovu ya maaskari na watendaji wetu na maovu haya yatafanyiwa kazi maramoja. Kwa aina hii kila mtu atakuwa askari wa mwenzake. Kwa ufupi, tutaweka utaratibu wa kila mtumishi wa serikali anayetoa huduma kwa wananchi kutathminiwa na wananchi wenyewe na hatua stahiki kuchukuliwa na chombo maalumu cha kusimamia utendaji wa watumishi wa umma katika taifa.

Ili kuyafanya yote haya katika mazingira ya Amani na utulivu, lazima tuwe na mihimili mikuu minne inayojitegemea yaani wananchi, Bunge, mahakama na mahakama. Wananchi watakuwa na uwezo wa kuwawajibisha watendaji wa mihimili hii mingine kwani wao ndiyo kitovu cha mamlaka. Kuwezesha haya kunahitaji katiba mpya inayotoa usawa katika muungano na nguvu kwa wananchi kusimamia serikali yao.

Ndugu walalahoi wenzangu,

Kama umesikiliza kwa makini, sehemu nyingi ya hotuba yangu nimetuimia wingi wa nafsi mfano tutaweka, tutafanya n.k. Hii ni kwa sababu natambua kuwa mimi mwenyewe sitaweza kufanya mambo yote haya bila kuwa na timu imara yenye malengo thabiti. Mtakaponichagua, nitaweka mfumo wa kuwarushusu wananchi kupendekeza majina ya watu wenye sifa na uadilifu thabitiwa wa kuwa sehemu ya serikali. Maoni ya wananchi yatazingatiwa katika uteuzi wa mawaziri na watendaji wa wizara bila kujali anatooka katika chama gani. Ni kwa mfumo huu, sote tutwawawajibisha maana tumeshiriki kuwateua.


Naombeni kura zenu na asanteni kwa kunisikilaza

Mtangaza nia

Mlosi Mtulutumbi

Chama Binafsi
 
Back
Top Bottom