Hotuba ya Mwalimu Nyerere Diamond Jubilee Hall 1985

Hotuba ya Mwalimu Nyerere Diamond Jubilee Hall 1985

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
HOTUBA YA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE UKUMBI WA DIAMOND 1985

''Kwa hiyo nilikuwa naijua Tanganyika African Association. Nilipokuwa ninaondoka kwenda Ulaya kusoma, nilikuwa nimeishaonja shughuli za TAA. Sasa niliporudi, baada ya kukaa Pugu siku chache, nikaja mjini Dar es Salaam. Nikauliza nani wanaongoza TAA?Nikaambiwa kuna jamaa mmoja anaitwa Abdul Sykes. Sasa ni marehemu. Abdul ndiye alikuwa katibu wakati huo.

Nilipelekwa na Kasela Bantu - ambaye naye aliteleza-teleza na hatunaye hapa (kwenye mkutano). Kasela Bantu alikuwa mwalimu mwenzangu. Tulifundisha pamoja Milambo. Nilipokuja Dar es Salaam, nikakuta anafanya kazi Redio (Tanganyika Broadcasting Corporation). Ni Kasela Bantu aliyenipeleka kwa Sykes.

Wakati huo mambo yalikuwa yanasinzia kidogo. Kwa muda mfupi mwaka ule, tukafufua-fufua, hasa kutoka Januari. Kufika Aprili, TAA ikafufuka. Tukafanya mkutano hapo Anautouglou. Kwenye mkutano huu wakanichagua kuwa Rais wao – wa TAA.

Ninasema yote haya kwa shukrani kwa wazee. Jamaa hawa walikuwa watu wazima wa Dar es Salaam, na mimi kijana mdogo Mzanaki, na Kiswahili changu si kizuri sana – cha matatizo.

Nimekuja, natoka Ulaya, tena masomoni. Muda mfupi tu jamaa hawa wakaniamini haraka sana – katika muda wa miezi mitatu. Wakanichagua Rais wa TAA. Hapo ndipo nilianza shughuli mpya ya kuandika katiba ya TAA na kuipa madhumuni hasa ya shabaha ya kuleta uhuru.

Baada ya miezi 13, hapo 1954, tukaanzisha TANU. Jina hili lilipendekezwa na akina Abdul Sykes. Walikuwa wamelifikiria tangu zamani, walipokuwa askari vitani huko Burma (Vita vya Pili).

Miezi minne baada ya kuanza kazi Pugu nikawa ninakuja Dar es Salaam, kwa mguu; kila Jumamosi. Baadaye wazee wakanipa baiskeli nikawa ninakuja mjini kukutana na wenzangu; kufanya mikutano.

Hivyo ndivyo tulivyofanya. Wazee wakaniamini upesi sana. Tukawa na uhusiano mkubwa sana. Wadogo wenzangu wengine walikuwa Abdul Sykes, Abass Sykes (mdogo wake), Dosa Aziz – waliokuwa wengi ni wazee.

Katika kuhutubia mikutano yangu, nilikuwa nikisema: Wazee na Ndugu zangu! Wazee hasa ndio walikuwa na mikutano ya awali ya TAA na TANU. Walikuwa na msimamo wa hali ya juu kabisa! Hawakuyumba hata kidogo! Vijana walikuwa na mashaka. Wengine walikuwa na vikazi vyao, waliogopa kuvipoteza.

Nalo jambo lenyewe ni la hatari – la kuzungumzia uhuru! Unaweza ukakosa kazi; na wapo waliopoteza kazi; wengine wakaacha kazi. Akina Rashid (Kawawa) waliona watoke kwenye shughuli hizo tuje tuungane katika chama.

Wazee wa Dar es Salaam, na baadaye wa nchi nzima, wakatuunga mkono, na kila nilipokwenda, watu wa kwanza walionielewa, walikuwa wazee.

Nilikwenda Songea mwaka 1955 mara baada ya kujiuzulu. Huko wazee walinipokea na kunielewa. Nilianza safari za kuitembelea Tanganyika nzima. Nilikwenda Mbeya. Mkutano wangu niliufanya na wazee; kikundi kidogo cha wazee, ndani ya nyumba ya mtu.

Kwa mkutano huu wa Mbeya, wazee wakauliza: Unatafuta nini? Nikawaambia natafuta uhuru. Wale wazee, kwa sababu ya vita vya Maji Maji, na wanakumbuka, kabisa, wakaona mimi ninatafuta jambo la hatari. Tulifanya mkutano wa makini kweli. Wakauliza: Wewe unawezaje kuleta uhuru? Wewe una njia gani kudai uhuru na usitiwe kitanzi na Waingereza?

Tulielezana. Nikawaambia ninyi wazee, Waingereza wanawadanganya, Waingereza wametumwa na ule Umoja wa Mataifa uliokufa (League of Nations), waje kuishika Tanganyika kwa muda tu; watusaidie, na wakati tutakapokuwa tayari, watuachie tukajitawale.

Waingereza wanafanya ujanja; hawasemi. Vita vimekwisha (vya Pili) na Umoja wa Mataifa mwingine – mpya (United Nations Organisation – UNO) umewakabidhi Tanganyika kwa shabaha ileile. Sisi siyo koloni lao.

Wamepewa dhamana tu.''
---

Katika hotuba hii Mwalimu anasema ‘’anadhani’’ Abdul Sykes alikuwa Secretary wa TAA.

(Katika hotuba iliyoko katika maandishi neno, ''nadhani,'' limeondolewa lakini ukisikiliza audio utalisikia amelitamka).

Mwalimu hana hakika na hili.

Kuanzia mwaka wa 1953 alipokuwa President wa TAA hadi mwaka wa 1985 Mwalimu bado hajui Abdul Sykes alikuwa na nafasi gani katika TAA.

Anasema mambo yalikuwa ‘’yamesinzia.’’

Ukweli ni kuwa TAA kuanzia mwaka wa 1950 uongozi ulipochukuiwa na Dr. Vedasto Kyaruzi kama President na Abdul Sykes Secretary TAA ilifanya mengi kuanzia kuunda TAA Political Subcommittee na kumleta Earle Seaton kama mshauri wa TAA katika masula ya sheria katika mambo ya Mandate Territories, yaani Nchi Chini ya Udhamini kama ilivyopitishwa na UNO.

TAA ilifanya mazungumzo ya siri na Jomo Kenyatta, Nairobi pia mazungumzo na Chief David Kidaha Makwaia kumwingiza TAA achaguliwe President kwa nia ya kuunda TANU mbali na kumwajiri Alexander Tobia kama kama mtumishi wa TAA.

Yapo mengi sana.

Mwalimu anasema kwa muda mfupi kufika April TAA ‘’ikafufuka.’’

Lakini April 1953 ndiyo Mwalimu anaingia madarakani kama President wa TAA Abdul Sykes akiwa Vice President baada ya uchaguzi wa Arnautoglo.

Ikiwa Mwalimu kaifufua TAA ndiyo kusema kaifufua TAA mwezi ule alipochaguliwa kuwa President.

Ukweli ni kuwa yeye alipochukua uongozi wa TAA April 1953 chama kilisinzia.

Mwalimu anaeleza mkutano wa Arnautoglo ambao alichaguliwa kuwa President, ‘’wao,’’ lakini hasemi nafasi hiyo aligombea na nani.

Mwalimu anasema ‘’akaandika,’’ katiba mpya.
Hapakuwa na ‘’uandikaji’’ wa katiba mpya.

Kilichofanyika ni kuwa ilinakiliwa katiba ya Convention People's Party (CPP) ya Kwame Nkrumah wa Ghana na sehemu ya CPP waliweka TANU.

Mwalimu anazungumza mkutano wa Songea na Mbeya mwaka wa 1955.

Safari ya kwanza ya Mwalimu ilikuwa Morogoro akiongozana na Zuberi Mtemvu na walifanya mkutano wa ndani ambao haukuwa na mafanikio.

Hii ilikuwa August, 1955.
Baada ya Morogoro Mwalimu, Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani walikwenda Lindi.

Yapo mengi sana.
Mwalimu kaichukua TAA ikiwa ina mipango madhubuti na fedha za kutosha.

Picha: Abdul na Ally Sykes Burma Infantry/Waasisi wa TANU/Baraza la Wazee wa TANU.

Screenshot_20211211-081823_Facebook.jpg
 
Reg...
Soma kitabu cha Abdul Sykes yako mengi.
Niko kwenye mchakato wa kukipata, Nitakisoma iwe iwavyo.
Vitabu kwangu ni hazina, Vitabu kwangu ni dutu za thamani sana na isitoshe ni lazima mashujaa hawa wote wa kihistoria walioikomboa nchini yetu na kuipatia uhuru lazima niwe na historia zao kwa kumbukizi ya kizazi hata kizazi.
 
Niko kwenye mchakato wa kukipata, Nitakisoma iwe iwavyo.
Vitabu kwangu ni hazina, Vitabu kwangu ni dutu za thamani sana na isitoshe ni lazima mashujaa hawa wote wa kihistoria walioikomboa nchini yetu na kuipatia uhuru lazima niwe na historia zao kwa kumbukizi ya kizazi hata kizazi.
Regi...
Ingia hapo chini:
mohamedsaidsalum.blogspot.com
 
Back
Top Bottom