JK ageuka mbogo
Shadrack Sagati
Daily News; Wednesday,December 31, 2008 @20:19
Rais Jakaya Kikwete ameagiza mtumishi yeyote wa serikali ambaye atahusika na wizi au ubadhirifu wa fedha za umma kufikishwa katika vyombo vya sheria. Katika salamu zake za mwaka mpya kwa taifa, Rais alisema bado hali si ya kuridhisha katika matumizi ya fedha za umma kumfanya afurahi na akaahidi kuwa mwaka huu utakuwa wa kubanana katika jambo hilo ili ufanisi uweze kufikiwa.
Alisema amewataka viongozi wenzake na watumishi wa serikali kusoma na kuzingatia maoni na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yaliyomo katika taarifa zake za kila mwaka.
Kuanzia mwaka ujao nitawaomba wakaguzi wa mahesabu ya serikali kumkabidhi kwenye vyombo vya sheria mtumishi wa serikali aliyehusika na wizi au ubadhirifu mara watakapougundua, alisema Rais.
Aliongeza kuwa kwa sasa utaratibu hauko hivyo lakini akataka ofisi ya CAG itazame upya utaratibu wa sasa ili isaidie kujenga nidhamu hata kama ni ya woga wa kufungwa.
Itasaidia kunusuru fedha nyingi za umma zinazotumiwa isivyo. Rais pia alimtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuendeleza kwa kasi na nguvu zaidi kazi waliyoianza ya ukaguzi wa thamani ya fedha zilizotumiwa na kulinganisha na kazi iliyofanyika (value for money audit).
Alisema ukaguzi wa asili umekuwa unahusu uandishi wa vitabu kwa mujibu wa kanuni za fedha. Lakini, inawezekana kabisa vitabu vya hesabu vikaandikwa vizuri lakini pesa zikatumika vibaya au hata kuibiwa.
Tunataka ulinganifu sawia wa fedha zilizotumika na kazi iliyofanywa. Pia Rais ameielekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kufanya kazi kwa karibu na ofisi ya CAG kusaidia kupambana na wasiozingatia nidhamu ya matumizi ya fedha na mali za umma hususan wezi na wabadhirifu wa fedha za umma kwa kutumia sheria ya mwaka 2007 iliyounda Takukuru.
Nimewataka wawe wakali kwa wala rushwa kama wafanyavyo sasa, lakini pia wawe wakali kwa wale wote wanaokiuka kanuni za fedha za serikali, alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa vitendo hivyo siyo tu vinaitia hasara serikali bali pia vinapunguza uwezo wa serikali kuwahudumia wananchi walioiweka madarakani.
Nimewataka waitumie vyema sheria mpya na fursa waliyonayo ya kuwaongezea uwezo wa rasilimali tuliyowapa kwa kutimiza ipasavyo wajibu wao. Nimewasihi pia kwamba katika kufanya hivyo wasionee wala kupendelea watu bali watende haki.
Kuhusu mauaji ya albino, Rais alisema mapema mwaka ujao itaendeshwa kura ya maoni nchi nzima na amewataka wananchi wawataje watu wanaowajua kuwa wanajihusisha na mauaji au kukata viungo vya albino. Alisema watu wawataje waganga wanaohusika, wauaji wa albino, wauzaji wa viungo vya albino na wafanyabiashara wanaotumia viungo hivyo.
Rais Kikwete alisema taarifa hizo zitasaidia kuwafuatilia na kuwakamata watu hawa waovu. Pia alisema utaratibu kama huu ulitusaidia katika mapambano dhidi ya ujambazi nchini. Naamini utasaidia kwa hili... tunafanya matayarisho ya zoezi hilo na wakati utakapowadia watu wataarifiwa namna ya kushiriki.
Katika hotuba hiyo Rais alisema serikali imeunda kikosi-kazi kinachojumuisha Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa cha kuendesha mapambano haya. Aliongeza kuwa hivi sasa wanaendelea na uchunguzi wa kina nchi nzima kuwatambua wahalifu na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria. Mpaka sasa watu 91 wamekamatwa na kufikishwa mahakamani na mapambano yanaendelea.
Katika salamu hizo za mwaka mpya, Rais Kikwete alisema mwaka umeisha nchi ikiwa tulivu. Alisema hiyo inathibitisha kuwa nchi inaweza kuwa tulivu isipokuwa pale ambapo baadhi ya watu watakapokuwa wameamua kuwa isiwe hivyo.
Naomba mwaka 2009 uwe tofauti. Tuache vitendo vya kuchochea ghasia kwa kisingizio chochote kile. Vitendo hivyo havitavumiliwa hata kidogo. Ni vizuri tukaambiana mapema tusije tukalaumiana, alisema Rais Kikwete na kuwaomba wanasiasa wayatambue hayo na tujiepushe nayo.
Pia aliomba makundi ya kijamii yatambue ukweli huo na waache kuwaendekeza wanasiasa hasidi. Alitoa onyo baada ya kueleza kuwa katika mwaka huu unaomalizika baadhi ya wanasiasa wamekuwa wanafanya vitendo au kutoa kauli ambazo zilikuwa zinalielekeza taifa kubaya.
Alisema walifanya hivyo kwa ajili ya kuendeleza manufaa binafsi ya kisiasa. Ni matumaini yangu kuwa tutajiepusha na mambo hayo katika mwaka 2009. Nawasihi viongozi wenzangu wa kisiasa na wa kijamii tubadilike, tuweke mbele maslahi ya taifa ili tuiepushe nchi yetu na mabalaa ambayo baadhi ya wenzetu yaliwakuta.
Kuhusu hali ya chakula, Rais aliwahakikishia wananchi kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni nzuri kwa miaka miwili mfululizo sasa, yaani 2007 na 2008, na nchi imekuwa inapata ziada ingawaje ni kidogo.
Napenda kuwahakikishia kuwa hakuna tishio la njaa nchini. Rais pia alizungumzia tsunami ya uchumi wa dunia na kueleza kuwa tatizo hilo litafanya malengo ya taifa ya kukua kwa uchumi mwaka 2008 na hata mwaka huu wa 2009. alisema uchumi utakua kwa asilimia 7.7 badala ya 7.8 mwaka 2008 na mwakani 2009 utakua kwa asilimia 7.3 badala ya asilimia 8 iliyokadiriwa.
Kiongozi huyo alisema kudorora kwa uchumi wa dunia kunafanya idadi ya watalii kupungua na mapato yake kushuka kwa kati ya asilimia 7 na 18. Alisema pia kuwa mauzo ya mazao kama pamba na kahawa kwenye masoko ya nje nayo yameshuka.
Rais alisema kupungua kwa mauzo nje na bei ya bidhaa zetu pamoja na kupungua kwa watalii kuna athari kwa uchumi wa nchi kwani mapato ya fedha za kigeni yatapungua jambo ambalo litapunguza akiba ya fedha za kigeni, hivyo kuathiri uwezo wetu wa kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje.
Aidha alisema mapato ya serikali kwa kodi zitokanazo na mauzo hayo yatapungua, hivyo kuathiri uwezo wa serikali wa kutimiza majukumu yake ya kiutawala na kiuchumi. Isitoshe ajira chache zilizopo katika sekta husika zitapungua na kusababisha watu hao kuwa na hali mbaya kiuchumi.
Kuhusu kupanda kwa gharama za bidhaa mbalimbali ikiwamo chakula, Rais alisema hali imeanza kuonyesha kushuka kwa mfumuko wa bei lakini akasema wakati mwingine hali huwa hivyo kwa sababu ya ukaidi na tamaa ya wafanyabiashara.
Aliongeza kuwa amekwishawaagiza mawaziri wahusika kuzibana mamlaka husika kutimiza ipasavyo wajibu wao kwa mujibu wa mamlaka waliyopewa kisheria kuwalinda wananchi dhidi ya wafanyabiashara wa aina hiyo.
Pia alitaka wafanyabiashara watoe ushirikiano unaostahili kwa maslahi ya wateja wao na taifa. Aidha, nazitaka mamlaka husika kutochelewa wala kuchelea kuchukua hatua zipasazo kwa wafanyabiashara wakaidi