The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 747
- 2,112
Intaneti imefungua ulimwengu mpya kwa watu wengi duniani kote. Fursa nyingi zinapatikana hapa. Teknolojia hii inatoa fursa ya watu kuboresha maisha yao kwa kuwapa ajira na kurahisisha shughuli zao binafsi ikiwemo za kibiashara.
Intaneti inafungua ufikiaji wa vitu vilivyokuwa si rahisi kufikiwa hapo awali. Ikiwa na mamilioni ya watumiaji, intaneti imekuwa mojawapo ya zana muhimu zaidi za mawasiliano katika enzi hizi.
Kwa kuzingatia jukumu muhimu la intaneti kama njia muhimu ya mawasiliano, Umoja wa Mataifa ulipendekeza kwamba ufikiaji wa huduma hii unapaswa kuwa sehemu ya haki za binadamu. Hii ni kwakuwa umegusa karibu kila nyanja ya maisha ya mwanadamu, sio tu maisha ya kibinafsi bali pia huduma za umma.
Kwa upande mwingine, intaneti pia inaruhusu umma kujua nini serikali inafanya. Sasa hivi hata watu wanaoishi katika maeneo ya mbali na miji wanajua kinachoendelea miongoni mwa vyama vya siasa na viongozi wa serikali. Lakini pia, inaruhusu makampuni kujifunza mbinu za ushindani na kuruhusu umma kukosoa bidhaa au huduma wanazozitoa.
Pamoja na majukumu yake yanayozidi kuwa muhimu, mtandaoni kunatarajiwa kuwa jukwaa linaloweza kufikiwa na watu wote, ambalo litawawezesha watu kuboresha maisha.
Hata hivyo, licha ya maendeleo haya, bado theluthi moja ya idadi ya watu duniani inasalia nje ya mtandao na wengi kati ya watu walio mtandaoni hawajaunganishwa ipasavyo.
Migawanyiko mingi ya kidijitali kama vile kati ya wanaume na wanawake, vijana na wazee, kati ya mijini na vijijini, pamoja na kati ya wale wanaofurahia intaneti bora na wenye intaneti hafifu inasababisha baadhi ya makundi kubaki nyuma.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU), asilimia tano ya watu duniani hawajaunganishwa kwenye Intaneti. Barani Afrika, ni asilimia 18 ya watu wake bado hawawezi kufikia huduma hiyo. Asilimia 32 zaidi ya watu duniani (asilimia 49 barani Afrika) wanafikiwa na mtandao lakini hawako mtandaoni kwa sababu mbalimbali ikiwemo bei wasizozimudu, ukosefu wa vifaa, na/au ukosefu wa ufahamu, ujuzi, au kusudi.
Hata hivyo, moja ya mambo ambayo intaneti imetoa ni usaidizi katika kutafuta kazi. Tovuti za kutafuta kazi, majukwaa ya kupashana taarifa na tovuti mbalimbali husaidia maelfu ya watu kupata kazi kila siku.
Ingawa nchi nyingi sasa zinatekeleza huduma hizi, huduma ya mtandao bado ina safari ndefu kuwa namna ya kutegemewa katika kutafuta kazi kwenye jamii maskini. Kikwazo kimoja katika maeneo hayo ni ufikiaji wa mtandao wenyewe.
Takwimu za Benki ya Dunia zinaeleza kuwa ongezeko la 10% la upenyaji wa mtandao wa intaneti barani Afrika linaweza kuongeza pato la mtu mmoja mmoja kwa karibu 2.5%. Utafiti zaidi juu ya nchi 12 za Kiafrika pia unaonesha kuwa watu ambao wana ufikiaji wa mtandao wa kasi ya juu wana uwezekano wa karibu 14% wa kuajiriwa kuliko wale wasio na ufikiaji huo.
Kuongezeka kwa ajira kunapunguza idadi ya kaya zinazoishi chini ya mstari wa umaskini. Hili lilidhihirishwa nchini Senegal ambapo kuanzishwa kwa 3G kulisababisha ongezeko la 14% la matumizi na kupunguza kwa 10% umaskini uliokithiri.
Hakuna shirika moja linaloweza kufanikisha lengo kuu la kuiunganisha dunia yote na intaneti. Mbinu shirikishi zinazohusisha wadau wa kimataifa wanaofanya kazi kwa karibu na wadau wa ndani na serikali zinahitajika. Pia inahitaji mchanganyiko wa ushirikiano wa serikali na sekta binafsi, na aina mbalimbali za teknolojia.
Intaneti ina manufaa makubwa ya kiuchumi na uwezekano wa kuimarisha ustawi wa mtu mmoja mmoja katika maisha yao yote. Inawezesha aina mpya za mawasiliano, burudani, kujieleza, na ushirikiano. Inawezesha ufikiaji wa huduma, ufikiaji wa maarifa mengi, nyenzo za kujifunzia, na fursa mbalimbali.