Hivi karibuni jijini Dar es salaam, tukiwa tunapambana kuingia ndani ya basi la Mwendokasi lililokuwa ‘limeshona’ abiria, nilimsikia mwenzangu mmoja akisema kwa uchungu, “Kama Mwendokasi inatutesa namna hii, hiyo treni ya SGR si itatuua kabisa?”
Nilibahatika kuingia, lakini yeye hakufanikiwa. Mlango ulijibamiza nyuma yangu kwa nguvu, nusura univunje mkono. Safari ilianza, Mungu bariki nilifika salama nilikokuwa nikienda! Haya ndio masaibu ya usafiri wa mabasi ya UDART, yanayowapata wananchi wa Dar es salaam kila siku, kinyume na matarajio yao. Ni mateso!
Ni muda sasa, tunazisikia tambo za serikali kuhusu ujio wa TRENI “ya mwendokasi” ya SGR. Kama ilivyokuwa kwa mabasi ya UDART, wananchi wanashangilia na kuipongeza serikali kwa kuanzisha usafiri mpya wa treni, ukilenga kuwapunguzia adha ya usafiri. Je, furaha hii itakuwa endelevu? Hatujui! Tunachojua ni kwamba furaha ya Watanzania kwa UDART imeyeyuka!
Kwa kuanzia nitajadili masaibu ya mradi wa mabasi ya UDART, halafu nitajadili historia ya usafiri wa reli nchini Tanzania. Nitamalizia kwa kuonesha hamu yangu ya kuona usafiri chini ya TRC mpya ukiendeshwa kwa umahiri, tija na faraja kwa wasafiri.
Hivi karibuni katika mtandao wa X nilikutana na picha, iliyoonesha kama mia tano, wakiwa wamejazana kwenye kituo cha Mwendokasi, mbele yao kukiwa na basi moja tu! Niliitazama picha hiyo kwa masikitiko! Maoni ya watu kwa picha hiyo yalikuwa mengi. Mmoja alisema, “Huu si usafiri wa mwendokasi, bali ni usafiri wa kujazana, kukanyagana, kuchafuana na kuchelewa kazini!”
Mwingine aliandika, “Jinsi nilivyoufurahia usafiri huu mwanzoni, siamini kama tumefikia hali hii, si bure Watanzania tutakuwa tumerogwa!” Kuna aliyeandika, “Mwendokasi imekufa, imekufa, imekufa! Menejimenti ya UDART imefeli kwa asilimia mia. Ni aibu kwa mradi mkubwa kiasi hiki kuishia kuwa kero namna hii.
Mwingine aliandika, “Kwa mazingira haya, tusije kushangaa kushuhudia vifo vya kukanyagana. Na hatari zaidi ipo kwa wanafunzi, wajawazito, wazee na walemavu. Kwa jinsi watu wanavyominyana, iko siku tutavuna maafa, na sijui kwa nini hakuna anayeliona hili!”
Gazeti la Mwananchi (2018) liliandika kuwa, Mradi wa mabasi ya Mwendokasi, ulianza Mei 2016, na ulionekana mkombozi kwa wakazi wa Dar es salaam, waliokuwa wakiteswa na usafiri wa daladala. Mradi ulianza vizuri, vituo na wafanyakazi walikuwa safi na wenye nidhamu. Magari yalikuwa mengi, yakija vituoni kwa wakati, na yakitaja majina ya vituo njiani.
Kulikuwa na utaratibu mzuri wa kukata tiketi, ustaarabu katika kupanda na kushuka, unafuu wa bei, usafi na usalama, kukaa au kusimama kwa nafasi, na kujali muda. Vitu hivi, vilizikonga nyoyo za wasafiri. Hata hivyo, Waswahili walisema, “Kuzaa si kupata”. Usafiri huu umegeuka kuwa SHUBIRI. Wapo wanaosema afadhali hata usafiri wa daladala!
Je, kuzorota kwa huduma za UDART kumetokana na nini? Binafsi, nimeziona sababu tatu. Ya kwanza ni ya kiutawala. Hii ni pana, lakini kikubwa ni ukosefu wa usimamizi. Uajiri usiozingatia uwezo, usimamizi mbovu wa wafanyakazi, usimamizi mbovu wa mifumo na michakato ya uendeshaji, urasimu na vitendo vya rushwa, ni vyanzo vikuu vya hali hii.
Pili, inaonekana kama UDART imefilisika, yaani haina fedha (mtaji) za kununulia mabasi mapya, kufanya ukarabati wa mabasi na mioundombinu, au kuboresha mifumo.
Tatu, ni maamuzi ya kisiasa. Wanasiasa nchini Tanzania wana historia ya kuingilia utendaji wa mashirika ya umma, hivyo kuyaangamiza. Teuzi za kisiasa za Wakurugenzi, ajira za vimemo, shinikizo la kuchangiwa pesa, za siasa nk. Mkono wa wanasiasa kwenye mashirika yetu, umeyaangamiza mengi.
Baada ya kuyaona mapungufu ya UDART, naomba sasa tujadili ujio wa usafiri wa treni ya SGR chini ya TRC mpya. Kihistoria, usafiri wa reli Tanzania ulianza enzi za ukoloni. Mwaka 1948 Shirika na Reli na Bandari la Afrika Mashariki lilizaliwa chini ya Jumuia ya Afrika ya Mashariki. Lilikufa mwaka 1977, Jumuia hiyo ilipovunjika.
Mwaka 1977 nchini Tanzania, liliundwa Shirika la Reli (TRC). Mwanzoni, shirika hilo liliendeshwa kwa ubora mkubwa. Nakumbuka, nilisafiri kwa mara ya kwanza kwa treni mwaka 1978, kutoka Mwanza hadi Dar es salaam. Nilisafiri kwa daraja la tatu, lakini nilifurahi!
Kwanza, sikusumbuka kupata tiketi pale Mwanza. Halafu, ndani ya treni, hakuwapo aliyesimama. Ni nafasi za abiria walioshuka njiani tu, zilizojazwa na waliopanda. Mabehewa yalikuwa safi, na yalisafishwa kila wakati, njia nzima. Vyoo vilikuwa visafi, vikiwa na maji safi muda wote. Mabehewa yalikuwa na taa, na feni zilifanya kazi muda wote.
Viti vilikuwa na sponji zilizofunikwa kwa ngozi iliyong’aa. Madirisha yalikuwa yakifunguka na kufunga kiurahisi. Ni mabegi tu, yaliyoruhusiwa kuingia ndani ya treni, sio matenga au magunia. Wahudumu walikuwa na nidhamu, wasafi na wacheshi. Lakini, haukupita muda mambo yalibadilika! Mwaka 1981 na kuendelea, hali ya shirika ilianza kudidimia, na huduma kudorora!
Huduma zilianza kuwa mbovu, kama zinazoonekana leo kwenye treni ya jijini Dar es salaam maarufu kama “Treni ya Mwakyembe”. Ubovu katika ukataji wa tiketi, muda wa kuondoka, mkanyagano ndani na wakati wa kupanda treni, uchafu wa vituo (stesheni) na mabehewa, ikawa ndiyo habari ya mjini.
Huduma za feni, taa na hewa safi ziliyeyuka. Viti vilikosa sponji na ngozi juu yake, watu wakakaa juu ya mbao. Huduma za chakula ndani ya treni zilizorota, na mabehewa yalijaa kunguni, mende, panya na harufu mbaya. Shirika la TRC likajifia kifo cha mende! Je, nini kilisababisha hali hiyo? Sababu ni hizi hizi, zinazoiporomosha UDART leo. Si bure, Watanzania tumerogwa!
Mwaka 2006 TRC hiyo ikavunjwa rasmi, na kuundwa Kampuni ya TRL na RAHCO. Huduma zilianza kuwa bora, lakini baadaye zikazorota tena. Sababu? Ni zilezile!
Mwaka 2017 TRL na RAHCO ziliunganishwa kuunda Shirika la Reli Tanzania (TRC) jipya, kisha kuanzisha mradi wa SGR. Uwekezaji katika SGR una lengo la kuongeza tija na ufanisi, kuchochea maendeleo, na kuwapa faraja wasafiri wa treni kwa huduma bora na za haraka.
Swali, je uongozi wa TRC mpya, umejifunza chochote kutoka kwa UDART, TRC ya zamani na TRL? Hizi tambo na mbwembwe zao zitatuletea faraja tunayoitamani? Kuhusu huduma za UDART mwananchi mmoja, kupitia Instagram aliandika, “Usafiri wa Mwendokasi ulipoanza, niliamini tulikuwa tumeagana na usumbufu wa usafiri, Dar es salaam. Nilijidanganya. Hakika naililia nchi yangu!”
Sasa, usafiri wa treni ya SGR uko mbioni kuanza. Ukweli, sitamani hata kidogo kuyaona ya UDART, TRC ya zamani, TRL, wala Treni ya Mwakyembe (angalia viambatisho). Ninataka kuona viongozi wa Wizara na TRC wakiamka na kujifunza kupitia historia. Viongozi, msikubali aibu, jipangeni vizuri! Tunataka TRC yetu iendeshwe kwa ufanisi, muda wote!

Upvote
4