Nionavyo mimi, taarabu ni sanaa, kama sanaa nyingine. Kwa vile ni sanaa inayotumia lugha, basi tunaiita "fasihi" (literature) na imo katika tapo la "fasihi simulizi" (oral literature).
Kama ilivyo sanaa yoyote ile, taarabu ni kitu kiko pale kwa ajili ya matumizi ya jamii. Sasa huwezi ukasema taarabu ni mbaya au ni nzuri kabla hujaitumia, au kabla haijawekwa kwenye matumizi, au kabla haijaimbwa, kama ambavyo huwezi kusema kisu au moto ni mbaya kabla havijatumika. Kisu ni kizuri kikitumika kukatia vitu tunavyotaka kukata, au kumenya, lakini kinaweza kuwa kibaya kikitumika kwa mfano kuulia. Vile vile moto ni mzuri ukikuivishia chakula, au ukikupashia joto maji ya kuoga, au ukikupa joto wakati wa baridi, lakini unakuwa ni mbaya ukikuunguzia nyumba, au ukitumika na watu kama akina Kibwetere kuteketeza wenzao, tena makanisani.
Taarabu nayo ni nzuri ikitumiwa na watu wenye busara, kwa kuimba nyimbo ambazo hata mtu na heshima zake anaweza akaimba akiwa popote, au hata Rais anaweza kuunukuu kwenye hotuba zake, kama ambavyo Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi alivyowahi kumnukuu Siti binti Saad. Lakini taarab ni mbaya ikiwa itaimbwa na mtu domo kaya, asiyeona tabu kuharisha kwa kupitia mdomoni. Kuharisha ni kutokwa na kitu katika hali ambayo si ile ya kawaida. Tumbo likichafuka utaharisha, kwa maana ile haja kubwa itatoka bila ya mpangilio. Vile vile ubongo ukichafuka, basi maneno nayo hutoka bila ya mpangilio. Mtu akila uchafu, tumbo huchafuka naye huharisha. Vile vile mtu akinywa uchafu (mfano pombe), ubongo huchafuka, naye pia huharisha kupitia mdomoni, maana maneno yake hutoka bila ya mpangilio.
Nilichogundua mimi ni kwamba taarab imevamiwa na watu wasio na ubongo uliotulia. Watu wasio na la kuwaambia watu zaidi ya kuchukua choko choko za mtaani na kuzifanya ndio maudhui ya simulizi zao, kama ambavyo fasihi andishi ilivyovamiwa na watu wasio na falsafa za kuipa jamii. Leo meza za magazeti zimejaa trashes zenye mambo ya kijinga, utakuta vijarida vimeandikwa uharo mtupu; sijui "Mtandao wa mapenzi", "Hadithi za Chumbani", "Shemeji Kula", n.k. Utashangaa leo, hata shuleni, katika somo la Kiingereza, kwa mfano, vitabu vingi vinavyosomwa vimeandikwa na watu wa Afrika ya Magharibi tu, akina Achebe, Armah, Sembene, n.k. Kutoka Afrika Mashariki yuko Ngugi (Kenya) na p'Bitek (Uganda). Wabongo wachache na vitabu vyao havisomwi. Hao niliowataja hapo juu, vitabu vyao vina mafundisho mazuri sana, lakini vinasomwa kwa kulazimishwa, kwa vile kuna mtihani.
Tatizo ni kwamba, narudia, taarabu imevamiwa na watu wasio na asili nayo. Taarabu ina wenyewe, kama Marehemu Kolimba nilivyomsikia wakati fulani akisema C.C.M. ina wenyewe. Akina ustadhi na akina Al-Anissa ndio walikuwa wakiimba taarab, sasa hivi hata wa-kuja nao eti wanaimba. La kuimba hawana ni "Mambo iko huku eeeh mambo iko kule", basi!
Kwenye taarabu watu wastaarabu walikuwa wanakwenda kutulia kupata burdani, leo walevi nao taarabu imekuwa yao. Kwenye taarabu kumeshaingizwa utamaduni wa pombe, na raha ya kilabuni, muziki uwe na fujo na ghasia na matusi ndio panakuwa na "raha". Hili ndilo tatizo la kwanza la kuharibiwa kwa taarabu, starehe ya waungwana imevamiwa na watu waso haya wala haiba.
Pili, jamii nayo inalikaribisha hili. Ndio maana nasema, mafunza hustawi kwenye kinyesi. Pakiwa na kinyesi lazima funza watastawi. Taarabu chafu sasa hivi imeshamiri kwa sababu wachafuzi wa mazingira wamefanikiwa sana kuyachafua. Jamii imeoza. Jamii yetu si jamii tena bali ni kinyesi, na ndio maana mafunza, yale yanayoandika na kuimba upuuzi, ujinga, matusi, yanastawi. Unadhani kama pasingekuwepo na watu wanaopenda mambo ya kipuuzi yaandikwayo, au yaimbwayo, waandishi hawa na waimbaji hawa wangekuwepo? Au hata kama wangekuwepo, wangepata pa kuuzia uharo wao?