Serikali ya JK yaweka historia
Habari Zinazoshabihiana
Karume abeza wapinzani Zanzibar 01.02.2007 [Soma]
Mpasuko wa kisiasa Z'bar wawa mwiba 27.07.2006 [Soma]
Mpasuko wa kisiasa Z'bar wawa mwiba 27.07.2006 [Soma]
*Yajadili taarifa Mdhibiti, Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali
*Yaelezwa kuwa haijawahi kufanyika tangu historia ya nchi hii
Na Mwandishi Wetu
KWA mara ya kwanza katika historia ya nchi, Baraza la Mawaziri limepokea na kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2005/2006.
Taarifa iliyotolewa Ikulu Dar es Salaam jana, ilisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, aliwasilisha taarifa hiyo kwa Rais Jakaya Kikwete, kwa mujibu wa Sheria Machi 26 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo, taarifa hiyo inatakiwa iwasilishwe katika kikao cha Bunge kinachofuata baada ya kuwasilishwa kwa Rais.
Taarifa hiyo iliwasilishwa bungeni juzi na baada ya hapo, Rais Jakaya Kikwete aliitisha Baraza la Mawaziri kuijadili katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), mjini Dodoma.
Rais aliagiza huo ndio uwe utaratibu wa kila mwaka wa kuijadili taarifa hiyo ya Mkaguzi Mkuu, ambapo Baraza la Mawaziri liliafiki na kuupongeza utaratibu huo.
Baraza pia lilimpongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Bw. Ludovick Utouh, kwa kutoa taarifa hiyo kwa wakati.
Katika majadiliano hayo, mawaziri hao walisisitiza kuwa ni muhimu na jambo la msingi fedha za umma zikasimamiwa na kutumiwa vizuri.
Kwa ajili hiyo Baraza limekubaliana kuwa udhaifu ulioainishwa katika taarifa hyo ufanyiwe kazi kwa dhati, ili taarifa ya miaka ijayo iwe nzuri.
Vile vile Baraza liliamua kuwa kila wizara, mkoa , idara za Serikali na Halmashauri, ziwe zinatoa taarifa za mapato na matumizi ya fedha kwa kila miezi mitatu na zijadiliwe chini ya uongozi wa mawaziri, viongozi wakuu wa idara, taasisi na halmashauri husika.
Katika kikao hicho, Baraza limeagiza kuwa hatua za haraka zichukuliwe kurekebisha kasoro zitakazobainika.
Mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, naibu makatibu wakuu, wakuu wa mikoa na makatibu tawala, wahasibu wakuu na wakaguzi wa ndani watakutana kesho mjini Dodoma, chini ya Rais Kikwete.
Baada ya kikao hicho, Aprili 29 mwaka huu, kutakuwa na kikao kingine Dar es Salaam kitakachohusisha wahasibu na wakaguzi wa ndani wa halmashauri zote za wilaya na miji nchini na wakurugenzi wa halmashauri hizo, nacho kitaongozwa na Rais.
Baraza la Mawaziri linatumaini kwamba baada ya vikao hivyo, viongozi na watendaji wote husika watakuwa makini na matumizi ya fedha nchini na kuongeza nidhamu, ili kutekeleza malengo yaliyokusudiwa