SoC01 Ianzishwe Bima ya Sheria Tanzania

SoC01 Ianzishwe Bima ya Sheria Tanzania

Stories of Change - 2021 Competition

Filosofia ya Rorya

JF-Expert Member
Joined
Sep 20, 2021
Posts
3,211
Reaction score
3,611
Nyanja: Haki za Binadamu

Kama sehemu ya maboresho ya kudumu ya sekta ya sheria nchini ili kuipa jamii ya kitanzania huduma maridhawa zenye viwango vya kisheria kwa kutafsiri na kutoa haki kwa raia wake wote pasina kujali kama wana taaluma ya sheria au la, ni muda muafaka sasa kwamba taifa letu lipokee na kuifanyia kazi changamoto ya haja ya kuanzishwa bima ya sheria [Legal Insurance] kwa manufaa ya raia na serikali yao kama ilivyo bima zingine za afya nk.

Jamii ya kitanzania ina kila sababu ya kurudisha fadhila kwa serikali ambayo imejitahidi kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika maboresho haya ya sekta hii nyeti sana katika jamii ambapo imeajiri majaji wengi na mahakimu ikiwamo kutoa leseni kwa huduma za ki-uwakili kwa kasi ya kuridhisha ijapokuwa bado huduma hizi hazijawafikia raia hasa wale ambao uwezo wao wa kugharamia huduma hizi bado ni mdogo sana na ndiyo wanaounda sehemu kubwa ya jamii. Kama sehemu kubwa ya jamii haifaidiki na huduma hizi basi inaleta tafsiri kuwa mchakato wa kutoa haki bado unahitaji kuimarishwa ipasavyo hadi hapo huduma hizi zitakapowafaidisha watu wengi katika jamii pana.

Taaluma ya sheria ni taaluma inayohitaji umakini mkubwa sana na mbinu maridhawa katika kutafsiri sheria ili kutoa haki kwa mhusika. Jamii nyingi zimefarakana kutokana na sheria kutafsiriwa kinyume na kusababisha haki kutopatikana kwa baadhi ya watu, hii pia ndiyo sababu kubwa ya kada ya sheria kuwa na ngazi mbalimbali za kutafsiri sheria na kutoa haki. Udhaifu mkubwa unaosababisha baadhi ya watu kukosa haki ni kule kushindwa kutafsiri sheria yenyewe na hapa hata wanasheria wasio mawakili huwa baadhi yao pia wanahitaji wanasheria walio mawakili ili kuwapa msaada licha ya majukumu waliyonayo wanasheria wasio mawakili.

Aidha ni ukweli kuwa licha ya mawakili wengi kusajiliwa na serikali lakini idadi yao bado ni ndogo kama ilivyo kwa mahakimu na majaji ukilinganisha na idadi ya mashauri [kesi]. Pia serikali inastahiki pongezi kwa kuonyesha dhamira nyingine nzuri pia ya kuimarisha tasnia ya sheria kwa kuanzisha shule ya kuwanoa wenye taaluma ya sheria [law school] ili waweze kubobea katika taaluma yao hii nyeti sana. Hii pia ikiwa ni sehemu ya mpango mzima wa maboresho ya kudumu ya sekta ya sheria nchini ambayo pia inaenda sambamba na jitihada za makusudi za kuzindua/kuelimisha umma/jamii kuhusu kuepuka mazingira ya uhalifu kwa kuhakikisha utii wa sheria za nchi bila shuruti ili kuwa wazalendo.

Lakini pia serikali inatafakari uwezekano wa kuruhusu huduma za uwakili kusambaa hadi katika mahakama za mwanzo, kupanua na kuboresha miundombinu katika mahakama na magereza vikiwamo majengo bora na vitendea kazi vya kisasa. Jitihada zingine za serikali ni pamoja na kusisitiza umuhimu wa utaratibu wa usuluhishi na upatanishi wenye lengo la kumaliza migogoro katika hatua hiyo pasina kulazimika kufungua kesi, hapa walalamikaji na walalamikiwa wanapatanishwa na kuelezwa gharama na faida za usuluhishi na maridhiano dhidi ya gharama na faida za kufungua kesi halisi. Pia kuna kutumikia vifungo vya nje ya jela kwa kufanya kazi za umma, uanzishwaji wa bodi za parole na misamaha ya Rais nk.

Huduma za uwakili nchini kama ilivyo sehemu zingine za dunia ni ghali sana kiasi kwamba kama jamii haiwezi kutafakari swala hili kwa namna ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu basi huenda jamii ikajijengea mtazamo hasi kuwa huduma za ki-uwakili ni kwa watu na makundi teule tu ndani ya jamii ambao wana uwezo wa kiuchumi, kundi ambalo ni dogo ukilinganisha na wale wengi wasio na uchumi imara na kwamba asasi za kutoa haki zitatafsirika kuwa ni kwa ajili ya kundi hilo dogo tu na hapa moyo wa uzalendo utawatoka wananchi. Ni kwa sababu hii andiko hili linajaribu kuchagiza uanzishwaji wa huduma ya bima ya uwakili ili kuifanya jamii iendelee kujenga imani kubwa kwa mfumo wa uendeshaji wake.

Serikali itunge sheria ya kuanzishwa bima ya uwakili [Legal Insurance Act] ambapo makampuni ya uwakili [chambers] yaliyosajiliwa yatahitajika chini ya sheria hii kusajiliwa kama makampuni ya bima ya uwakili pia ambapo yatakuwa chini ya udhibiti wa mamlaka ya kuratibu mifuko ya hifadhi za jamii nchini kwa mambo ya bima tu na siyo kwa mambo ya shughuli zao za kisheria na uwakili. Chamber hizi ziweke amana [deposit] kwa mamlaka ya udhibiti wa mifuko ya hifadhi za jamii ili kwamba kama chamber itafunga shughuli zake basi wanachama [wateja] walazimike kuchagua chamber nyingine ambayo mamlaka ya udhibiti wa mifuko ya hifadhi za jamii itaendeleza bima yao huko kwenye chamber mpya watakayokuwa wamejiunga nayo kwa kuhamishia huko amana [deposits] ya chamber iliyofunga shughuli zake. Vinginevyo chamber moja ikifunga shughuli zake basi amana [deposits] zake ambazo ziko katika sura ya dhamana/security kule mamlaka ya udhibiti mifuko ya hifadhi za jamii, mamlaka hiyo iruhusiwe na sheria kuziweka sokoni amana hizo ili chamber zingine zenye nia ziweze kuzinunua na kuendeleza uanachama wa wateja wa chamber iliyofunga shughuli zake ijapokuwa hapa uhuru wa wanachama kujiunga na mfuko waupendao utakuwa umeminywa.

Sheria hiyo itoe uhuru wa wanachama [wateja] kujiunga na mfuko wa bima ya uwakili bila vikwazo na huduma zingine za wateja-makampuni [corporate customers] wa chamber hizi ama ziendelee kama zilivyo hivi sasa au sheria hiyo ya bima ya uwakili iweke utaratibu mpya utakaofaa baada ya kuruhusu mjadala mpana wa wadau wote wa kuanzishwa bima ya uwakili/sheria.

Wanachama [wateja] ambao watatokana na raia wote wa Tanzania na wale wenye vibali vya kuishi na kufanyakazi nchini, watatakiwa kulipia bima hii kila mwezi toka kwenye mapato yao asilimia fulani kama itakavyoamuliwa na sheria hiyo kwa ajili ya huduma za bima ya uwakili.

Kuna faida nyingi za kuwa na bima ya uwakili nchini zikiwemo kupanua wigo wa serikali kukusanya mapato kwa njia ya ushuru [ama toka kwa wanachama au chambers]. Sheria itaamua ni njia gani muafaka ya serikali kukusanya mapato kutokana na ubunifu huu wa chanzo cha mapato ambayo yatarudi kuisaidia jamii kupitia bajeti za serikali.

Chamber zitapanua wigo wa ajira za wanasheria, mawakili na wenye taaluma ya bima nk ambao wamekosa ajira na pia itaziwezesha chambers kuboresha mapato ya wafanyakazi wao. Hii pia itakuwa imeipunguzia serikali mzigo wa raia wake kukosa ajira.

Kutakuwa na kuchochea ufanisi wa chambers katika kushughulikia kesi kwa viwango stahiki kwa namna ya ushindani ili kuvutia wateja wengi zaidi. Chamber ikiwa na ufanisi na umahiri wa kuendesha kesi kwa mafanikio itakuwa imejijengea sifa kwenye soko la shughuli za uwakili.

Wananchi kwa ujumla au wanachama wa mifuko hii ya bima ya uwakili watakuwa na uhakikisho wa usalama wao wawapo na shauri la kisheria nje na ndani ya mahakama kwa sababu hawatahitajika kuvuja jasho kutafuta pesa ikiwamo kuuza mali zao ili kugharamia mashauri [kesi hizo] hayo kwa sababu gharama zote za kuendesha shauri zitatokana na bima yake ambayo tayari alikwishalipia kwa kukatwa kwenye mapato yake e.g. mshahara nk.

Chamber zitaboresha mapato yao kwa kiwango cha juu kabisa kwa sababu wakati ambapo wateja wengine watakuwa hawana kesi basi makusanyo ya mapato ya vipindi hivyo yatawekezwa kwenye shughuli zingine za chamber za kuzalisha mapato zaidi.


Somo la bima ya sheria/uwakili liingizwe kama moduli ya kozi ya sheria kwenye mtaala wa masomo ya sheria ili kuepusha wanasheria kwenda kufanya kozi-tengefu mpya ya bima. Ni muhimu wanasheria wakajuwa uendeshaji wa mfumo wa bima katika mazingira ya sheria ili iwasaidie kuwa na ufanisi na tija zaidi katika shughuli zao za uwakili.

Faida kubwa ya uanzishwaji wa bima ya sheria/uwakili nchini ni kuwa itasaidia ama kuondoa kabisa au kupunguza kwa asilimia kubwa sana vitendo vya rushwa, ufisadi na ukengeufu wa kimaadili kwenye taasisi zote za kusimamia haki. Wanachama au wateja wa chambers/mifuko ya bima ya uwakili wawapo na mashauri/kesi hawatalazimika kutoa fedha kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa mashauri hayo kwenye taasisi hizi za kutoa haki kwa sababu fedha hizo watakuwa wameishazilipa chambers/mifuko ya bima zao za sheria kutoka kwenye makato ya mapato yao ya kila mwezi. Kama kutakuwa na usimamizi/uendeshaji mzuri wa utaratibu huu basi nina ujasiri kutamka kuwa vitendo viovu vya rushwa vitapungua sana kwenye asasi za kutoa haki.

Faida nyingine kubwa ni kuwa gharama zote zitakazotakiwa kulipwa kwa taasisi hizi za kugawa haki, miamala yake [transactions zake] itafanyika kati ya chamber/mfuko wa bima ya sheria na taasisi hizi za kutoa haki e.g. mahakama na kwamba malipo yote yatakwenda kwenye hazina ya serikali hivyo mianya ya uvujaji wa mapato haya itakuwa imezibika kwa sababu pesa taslimu hazitalipwa mahakamani bali ni hundi ndiyo itapelekwa hazina ya serikali na hati ya malipo kuonyeshwa mahakamani kama kithibitisho ili kufunga au kuendelea na hatua za shauri husika.

Andiko hili linapendekeza kuwa katika utekelezaji wa uanzishwaji wa bima hii, serikali inaweza kuanza na mradi wa majaribio [pilot project] kwa kuanza majaribio haya katika sekta ya ulinzi binafsi [makampuni ya ulinzi], sekta ya utalii na hoteli na sekta ya viwanda; hizi zikiwa ni sekta ambazo hivi sasa zinaongoza kwa idadi kubwa ya migogoro ya kazi na kutokana na kipato kidogo na asili ya mikataba yao ya ajira, wengi wa wafanyakazi wake wamepoteza haki zao kwa kukosa maarifa ya sheria na uwezo wa kugharamia huduma za uwakili. Vinginevyo bima hii ianzishwe kwa sekta zote rasmi na zisizo rasmi hata na wafanyabiashara na wakulima pia watakaoweza kuchangia ili kuruhusu bima kuhudumia wigo mpana wa mashauri [kesi] yote ya madai na jinai [civil and criminal cause].

Naomba kura zote
 
Upvote 1
Back
Top Bottom