Magazetini
JF-Expert Member
- Aug 16, 2014
- 593
- 1,712
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Ernest Mangu, ameonya kuwa watu wote watakaobainika kughushi vyeti katika kuomba ajira pamoja na wanaodahiliwa kuingia katika vyuo mbalimbali nchini watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia amewataka wananchi kuacha tabia ya kuvamia vituo vya polisi, badala yake washirikiane kwa pamoja kuwabaini wahalifu wanaotumia silaha za moto pamoja na zile za jadi.
IGP Mangu alisema hayo wakati akimkaribisha Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima, kwenye mahafali ya kufunga mafunzo ya askari 396 katika Chuo cha Taaluma ya Polisi (CCP), mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Alisema kutokana na kuwapo wimbi kubwa la watu wanaogushi vyeti ili kupata ajira, polisi kwa kushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) wamejipanga kuhakiki vyeti na kuonya kuwa atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
"Serikali imekuwa ikipata hasara kubwa kutokana na kuwalipa watu wawili waliotumia jina moja na cheti kimoja katika kuomba ajira…hali hii sasa imefika mwisho. Na ndiyo maana kwa kuanza, tumeanza na idara yetu, hasa kwa wanaoingia kwenye ajira mpya," alisema IGP Mangu.
Aliwataka wananchi kushirikiana na polisi kupambana na uhalifu na kusema kwa sasa jeshi hilo limerudi kwao, hivyo ni vyema wakaacha kujichukulia sheria mikononi pindi wanapomkamata mhalifu, badala yake wamfikishe katika mikono ya sheria.
Pia aliwataka wananchi kuwafichua wahalifu wote, kwani wengi wao wapo ndani ya jamii na kuwahakikishia kwamba, siri zitatunzwa atakayetoa taarifa za kukamata wahalifu.
Vilevile, alilaani vikali vitendo vya uvamizi wa vituo vya polisi na kusema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika.
CHANZO: NIPASHE