Pre GE2025 Ilani ya chama cha siasa unachokiunga mkono inazungumziaje utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi?

Pre GE2025 Ilani ya chama cha siasa unachokiunga mkono inazungumziaje utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi?

Mijadala ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025 (Kabla, wakati na baada)

The Sheriff

JF-Expert Member
Joined
Oct 10, 2019
Posts
747
Reaction score
2,112
Climate Change.jpg


Utunzaji wa mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi ni masuala muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote, hasa zile zinazokabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kama ilivyo kwa nchi yetu Tanzania. Katika muktadha wa kisiasa, ilani za vyama vya siasa zinachukua nafasi muhimu katika kuainisha mipango ya kukabiliana na changamoto hizi.

Ilani hizi zinatupa fursa ya kuelewa ni kwa kiasi gani vyama vya siasa vinaangazia suala la mazingira na kupambana na mabadiliko ya tabianchi, na kwa nini wananchi wanapaswa kujua na kutathmini ahadi hizo kabla ya kufanya maamuzi yao ya kisiasa.

Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri sekta za kilimo, uvuvi, afya, na hata miundombinu, ambayo ni tegemeo kuu kwa uchumi wa Tanzania. Ripoti zinaonesha kuwa Tanzania ipo kwenye hatari ya mabadiliko haya, hasa kwa kuzingatia ongezeko la joto, kupungua kwa mvua katika maeneo ya kilimo, na kuongezeka kwa majanga kama mafuriko.

Hata msaada wa Tsh. Trilioni 2.06 kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi ulioidhinishwa hivi karibuni na Bodi ya Utendaji ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ni miongoni mwa vielelezo kuwa tupo kwenye hatari na tunapaswa kufanya vizuri zaidi kutunza mazingira yetu. Dira ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), lengo namba 13 linataka hatua madhubuti zichukuliwe kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku lengo namba 15 likilenga kulinda mazingira, ikiwa ni pamoja na misitu na bioanuwai.

Ingawa Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zinashiriki kikamilifu katika makongamano na mazungumzo ya kimataifa kujadili athari zitokanazo na Mabadiliko ya Tabianchi na kuweka Mikakati ya pamoja kama Dunia kukabiliana na athari hizi, bado kuna mahala hatujakaa vizuri. Kwa maoni yangu, mahali hapa ni suala la mazingira kutojadiliwa kwa kina na kuwekewa msisitizo ndani ya nchi, na katika ngazi mbalimbali, hasa na vyama vyetu vya siasa ambavyo ilani zake zina nguvu katika utekelezaji wa masuala ya maendeleo ya nchi.

Ilani za vyama vya siasa zinapaswa kuweka mikakati thabiti na inayotekelezeka ili kukabiliana na changamoto hizi. Changamoto kubwa niliyoiona wakati najaribu kuperuzi (hapa, hapa na hapa), ni kwamba ilani nyingi zinaweza kuwa na kauli za jumla tu kuhusu mazingira bila kutoa mipango maalum ya utekelezaji. Lakini pia, vyama vingi vimekuwa vikiweka masuala ya utunzaji wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa kiasi fulani tu, lakini utekelezaji mara nyingi umekuwa dhaifu au haupewi uzito unaostahili.

Kwa kuona hayo tunaweza kukubaliana kuwa vyama vya siasa vinapotunga ilani zao, ni muhimu kutazama kama wanazingatia mikakati inayoendana na changamoto halisi za kimazingira. Hii ni kwa sababu ilani hizi zinatoa mwelekeo wa kisera na zinawajibika kwa wananchi walio na haki ya kutathmini ni kwa kiasi gani mipango hiyo inaakisi uhalisia na changamoto zinazowakabili.

Kwa mfano, baadhi ya vyama vinaweza kuahidi kupanda miti milioni kadhaa bila kujali ni kwa namna gani watahakikisha miti hiyo inakua na kuchangia katika kupunguza athari za tabianchi. Wengine wanaweza kuzungumzia matumizi ya nishati mbadala, kama vile jua na upepo, lakini bila kutoa ufafanuzi wa kina juu ya ufadhili au miundombinu inayohitajika kufanikisha mipango hiyo.

Ni muhimu kuchambua sera hizi kwa kuzingatia pia hali halisi ya kiuchumi na kijiografia ya Tanzania. Vile vile, ni muhimu kutathmini ni kwa namna gani sera za mazingira zinaweza kuwa sehemu ya mfumo mpana wa maendeleo endelevu, ambapo mazingira na uchumi vinaweza kuunganishwa bila kudhoofishana.

Kuna umuhimu gani kwa wananchi kujua Ilani za vyama vyao kuhusu mazingira?

Wananchi wanapaswa kuwa na uelewa mpana kuhusu ilani za vyama vyao vya siasa, hasa kwenye suala la mazingira, kwani sera hizi ndizo zitakazounda mustakabali wa maisha yao na vizazi vijavyo. Uharibifu wa mazingira na kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kunaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na ongezeko la umasikini, ukosefu wa chakula, magonjwa, na athari kwenye sekta muhimu za kiuchumi.

Kwahiyo, kama wewe mwananchi unaunga mkono CCM, CHADEMA, ACT-WAZALENDO, CUF au chama kingine chochote, ni muhimu kujua chama chako kina mikakati gani ya kutunza dunia yetu. Ni suala la msingi sana.

Wananchi wanapaswa kutathmini ilani hizo kwa kutumia vigezo kama uhalisia wa mipango, rasilimali zitakazotumika, na namna utekelezaji utakavyofanyika. Pia, ni muhimu kufuatilia rekodi za utekelezaji wa sera hizo katika vipindi vya nyuma ili kuona kama ahadi zilizotolewa zilitimizwa au ni muendelezo wa blablaa za kisiasa tu.

Wananchi wanapaswa kuwa macho na makini katika kutathmini ilani hizo, kwani mazingira yanaathiri moja kwa moja maisha yao ya kila siku. Utunzaji wa mazingira na mipango ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi haipaswi kuwa suala la la kushughulikia baadaye, bali iwe ni sehemu kuu ya ajenda za kisiasa kwa vyama vyote nchini Tanzania, hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
 
Nadhan ni CCM na ACT labda ndio wana ilani. Sisi bavichaa tumekaakaa tu. Sasa hata hatueleleweki na tunamtaka Mdee awe Mwneyeketi wa chama.
 
Back
Top Bottom