Herbalist Dr MziziMkavu
JF-Expert Member
- Feb 3, 2009
- 42,872
- 34,363
Mkuu wa Idara ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam Prof. Adolf Mkenda
Shirika la Fedha Duniani (IMF) limeishauri Tanzania kuongeza jitihada katika usimamizi mzuri wa kisera utakazosaidia kukuza uchumi wake sambamba na kupunguza tatizo la umasikini wa kipato linaloikabili asilimia kubwa ya wananchi wake.
Rai hiyo ilitolewa juzi na Mwakilishi wa shirika hilo hapa nchini, Thomas Baunsgaard, wakati akitoa ripoti ya IMF juu ya mapitio ya mwenendo wa kiuchumi na vipaumbele vyake katika nchi mbalimbali duniani.
Ripoti hiyo imeonyesha kuwa, Bara la Afrika limefanikiwa kufanya vizuri katika kipindi cha hivi karibuni ikilinganishwa na miaka mingine iliyopita, suala alilosema limechangiwa na sera mbalimbali lililoanza kuzitumia.
Baunsgaard alisema ni vyema Tanzania ikawa na usimamizi mzuri hasa katika matumizi ya rasilimali zake ili ziweze kuwasaidia wananchi na kukuza uchumi wake.
Kumekuwa na usimamizi mzuri wa kisera ambao umesaidia utulivu wa kiuchumi na kuleta matumaini, pia mfumuko wa bei umeendelea kushuka, endapo jitihada za usimamizi wa kisera zitaongezwa, ni dhahiri hali ya uchumi itazidi kubadilika na kuwa nzuri zaidi alisisitiza Baunsgaard.
Alisema ni muhimu kuendelea kudhibiti sera za mapato na matumizi ya serikali sambamba na sera za usimamizi wa fedha ili kuwa na uchumi endelevu.
Baunsgaard alisema hali inaonyesha kuwa, Tanzania imedhamiria kuchukua hatua za ziada ili kuhakikisha inafikia lengo lake la kupunguza mfumuko wa bei hapa nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam Prof. Adolf Mkenda, alisema licha ya uchumi kuonyesha kuwa unakuwa kwa asilimia 7 kwa mwaka, tatizo la umasikini kwa wananchi wake bado linaonekana kuwa kubwa.
Alisema licha ya maeneo ya elimu, miundombinu, afya kufanya vizuri, bado kuna haja kwa serikali kufanya kila linalowezekana ili kupunguza umasikini huo kwa wananchi wake hasa wa kipato.
CHANZO: NIPASHE