India imepata uwenyeji wa kukaribisha mkutano wa
BRICS Septemba hii. Mijadala yenye tija ni mingi sana kwenye mkutano huo, na mimi nimeamua kutega sikio maana kwa siasa za dunia za siku za usoni, kuna uwezekano mkubwa sera za dunia zikawa zinashinikizwa na wao.
Mambo ni mengi mjini
New Delhi; mitaa imefurikwa na misafara, itifaki kali ya ulinzi, na vyombo vya habari vikijaribu kupata matukio.
Kilichonishangaza ni kwamba
mitaa mingi imefungwa isionekane kwa kutumia pazia la zaidi ya futi kumi. Kwa mtazamo wa kiusalama, unaweza kudhani
mitaa hii ina viashiria vya uhaini au vitendo vya kigaidi. Lakini ukilitazama kwa undani zaidi, utagundua ni matokeo ya kuwa na
umaskini uliokithiri, mpaka waliousababisha wanaona aibu wageni wakiuona.
Kwenye video hapo juu ni mtaa wa
Coolie Camp uliopo Vasant Vihar. Huu mtaa ni wa
mabanda (slams) na makazi ya watu
wanaoishi kwenye ufukara wa hali ya juu, na kwa namna hilo pazia lilivyowekwa, lengo lake
si kuuficha tu mtaa huo, bali
kuwafungia watu wa mtaa huo wasitoke na wasionekane "
wageni wasije wakaona ufukara wao."
Kwenye jamii, kitendo kama hiki kinaweza kuonekana ni cha
kuficha aibu kwa muda, lakini kiuhalisia kinamaanisha
mfumo kushindwa kutimiza majukumu yake. Ni
usaliti na kuwatenga watu waliopo kwenye
matatizo ambayo, kwa sehemu kubwa, ni
matokeo ya mfumo huo huo.
Wakuu, hii ngoma kwa sasa
inachezwa na wenzetu kwa ala za kihindi, lakini kwa ujio wa matukio ya kimataifa hapo mwakani,
tujiandae na kucheza Punjabi, mfumo lazima na sisi utufiche ndani (uwezo wanao na sababu za kufanya hivyo wanazo).
Kama mnadhani hili suala ni maigizo na haliwezi kuwakuta, basi fanyeni rejea ya
Julai 2013 kipindi Barack Obama anakuja. Na kama mnadhani 2013 mlikuwa maskini sana mpaka mlifaa kufichwa, basi naomba mrejee
Januari 2025, kipindi marais 27 walipokuja kwenye mkutano wa nishati (
Africa Energy Summit / Mission 300). Na vile ameshasema mji ni mchafu,
mtaoga na kuulamba, lakini mjini hamtaenda ng'o!
Hii nikawaida yetu, tunapopokea mikutano mikubwa, igizo hili hili linajirudia. Tunatenga njia za VIP,
tunapaka rangi kuta zinazotazama barabara kuu pekee, na
kuwafukuza wamachinga kama wadudu. Tunafanya "
maendeleo" ya muda mfupi kwa ajili ya kamera za kimataifa huku tukisukuma wananchi washinde na njaa huko majumbani.
Wakuu hii fomula haina huruma kote duniani;
Kwanza, wanakunyima makazi bora, huduma, na sauti ya kujitetea. Kisha, wageni wakifika, wanachukulia kujitafutia kwako riziki kama aibu na kukuamuru usimame nyuma ya pazia ili picha zao zitoke vizuri
Serikali inayoficha maskini wake mbele ya wageni inakiri kufeli kutimiza majukumu yake, lakini pia inakiri haina mpango wa kuwatoa watu kwenye umaskini huo.
Kama umaskini wa nchi una aibu kubwa hivi mpaka unafichwa usionekane, mbona inakuwa halali kwa wananchi kuuishi kila siku?