Insha: YAH: Kuku wa kienyeji na kuku wa kizungu

Insha: YAH: Kuku wa kienyeji na kuku wa kizungu

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
33,771
Reaction score
41,027
KUKU WA KIENYEJI NA KUKU WA KIZUNGU – INSHA
2929952120102750892DuGDcJ_ph.jpg

Na. M. M. Mwanakijiji

Kuna kuku wa kienyeji na kuku wa kizungu; na katika watu wanaopenda kula kuku basi wapo wanaopenda ladha ya kuku wa kienyeji na wapo wale wanaopenda ladha ya kuku wa kizungu. Na kutokana na mapenzi hayo ya aina zao za kuku baadhi ya watu wameamua kufuga kabisa kuku wa kienyeji au kuku wa kizungu.

Japo wote ni kuku na kuku ni kuku bado zipo tofauti kadhaa kati ya kuku hawa na ninaamini ni kutokana na tofauti hizo ndio ilikojificha pia tofauti ya ladha zao. Kuku wa kienyeji ni wale kuku ambao wametokana na mbegu za majogoo ya kienyeji na wale wa kizungu wametokana na mbegu za majogoo ya kizungu na wametotoleshwa kitaalamu badala ya njia ile ya kienyeji ya kukufukuzwa na jogoo lenye usongo (wengine wanaita ukame) na kupapatikiwa nalo.

Kuku wa kienyeji mara karibu zote ni kuku mwenye uhuru mkubwa tu. Banda lililoko uani ni mahali pake pa kulala tu lakini tangu anapofunguliwa asububi hadi machweo ya jua kuku wa kienyeji yuko huru kurandaranda mitaani, kuchakuachakua mavumbi katika kutafuta chakula na marafiki. Jioni ikifika hasahau nyumbani utamuona taratibu anaanza kuelekea nyumbani na ukichelewa kumfungulia mlango wa banda basi utamkuta nje anasubiria, kachoka kwa siku ndefu.

Kuku wa kizungu hana uhuru huo. Tangu kutotolewa kwake, malezi yake na maisha yake yote yeye ni kuku wa kuangaliwa kwa karibu. Chakula chake kinatengenezwa maalum na hulishwa kwenye banda lililojengwa na lenye vifaa maalum vya chakula na maji. Kwa kweli amezoeshwa kutafutiwa na kupatiwa chakula kinachoitwa "bora". Akipatwa na "mafua" hutafutiwa dawa na mganga kumtibu kitu ambacho kuku wa kienyeji hakimsumbui.

Kuku wa kienyeji huishi maisha ya machale machale tu. Tangu anapotoka bandani asubuhi hadi jioni huangalia kwa makini kila anayeingia nyumbani hapo. Akiona kuna ugeni au wageni basi kuku huenda kucheza mbali na nyumbani. Anajua asipoangalia siku hiyo anaweza kugeuzwa kuwa mlo wa wageni. Hivyo, muda mrefu hujilinda na kucha za mwewe na vile vile hujiadhari na kisu cha mchinjaji.

Kuku wa kizungu hana machale hayo. Yeye huishi kwa ridhaa na furaha ya mfugaji. Anajua sababu ya yeye kuwepo kwake hapo nayo ni kumfurahisha mfugaji. Na hili linaonekana hasa kwa wale kuku wa kizungu ambao hufugwa kwa ajili ya kutaga mayai yaani, kuku wa mayai. Hawa inadaiwa na baadhi ya watu wenye uzoefu wa kuwafuga kuwa ni kuku wenye wito mkubwa zaidi; wito wa kuwa watamiaji.

Kuku wa kienyeji hata hivyo anajua kuwa jukumu lake kubwa ni kugeuzwa mlo mzuri siku ya siku ikifika. Hivyo, hujitahidi kufanya kila jitihada ya kupata jogo wa kumtagisha ili awe na muda wa kutamia na kutotoa na kuwatunza vifaranga vyake. Lakini anajua kabisa kuwa pindi vifaranga hivyo vitakapoweza kuwa huru tu kama kuku wengine wa kienyeji na yeye mwisho wake unakuwa umekaribia.

Hivyo, siku akiona watoto wanauliza uliza yuko wapi basi anajua leo ni leo. Na kwa kuonesha kuwa kuku huyo hana mpango wa kutoa ushirikiano wowote katika njama hiyo ya kumgeuza kitoweo basi huleta usumbufu mkubwa. Uzoefu wangu katika kujifunza juu ya kuku wa kienyeji ni kuwa kama wewe ni mtu wa kukata tamaa basi usijaribu kuwafukuzia kwani wanajua mazingira yao, ni wajanja na hawadanganywi kirahisi. Wanaweza kukukimbiza mtaa mzima hadi ukajikuta unafikiriwa wewe ni mwizi.

Kuku wa wa kizungu wa nyama waliofugwa vizuri huwa wanajileta wenyewe kwa mchinjaji kwani anachohitaji kufanya ni kuingia bandani tu. Mara nyingi mchinjaji ambaye anaweza kuingia huku kisu kakishika juu hupokelewa kwa kile kinachosadikiwa kuwa ni shangwe kubwa bandani kwani wanafikiri amewaletea chakula chao kile cha kizungu. Ni rahisi kumnyakua mmoja wao na kuelekea naye "kusikojulikana".

Na hata mtu akifanikiwa kumkamata kuku wa kienyeji baada ya mbio ndefu haina maana kuwa kuku huyo atalamba kisu kiulaini hivyo. Atajaribu kupigania uhuru wake lakini kama yanayosemwa ni kweli basi moyoni huwa anafurahia kuwa katika huduma ya mwenye nyumba.

Siri hii ya kuku huyu wa kienyeji huonekana katika kuku aliyepikwa vizuri na kienyeji; aidha kwa mchuzi, kuchomwa au kuokwa kuku wa kienyeji haitaji viungio vingi sana kwani ladha yake inatajwa kuwa imo "mumo kwa mumo". Ukiwakuta watu wanaopenda kuku wa kienyeji kwa kweli wako tayari kufunga safari ya mbali kwenda kutafuta nyama ya kuku hao. Hii imewahi kuwatokea baadhi ya watu wengi ambao wamejikuta wanaishi mazingira ambapo ni kuku wa kizungu wanafugwa na kupatikana kiurahisi.

Upande mwingine wanaopenda kuku wa kizungu hawasikii lolote kuhusu kuku wa kienyeji. Wao wanaamini hakuna kitu ambacho Mungu amekiomba bora kuliko kuku hao wa kizungu ambao wanajulikana pia kwa jina la "kuku wa kisasa". Wanasema kuwa kuku hao wamelishwa na kutunzwa vizuri na wana minofu iliyonona kuliko kuku wa kienyeji. Na wanaamini kuwa utamu wa kuku huyo huonjwa vizuri pale anapoongezewa viungo vya kila aina na hivyo kumuandaa kwake ni kwa gharama kubwa.

Wenye kupenda kuku wa kienyeji huwasifia kwa kusema kuwa ni kuku ambaye amejaribiwa katika mazingira magumu, ni mjuzi wa aina yake na kutokana na kuwa huru zaidi basi amejijengea kinga ya mwili kutoka katika magonjwa mbalimbali kulinganisha na kuku wa kizungu ambaye inasemekana hata ukimtoa bandani haendi kokote kwani hajui afanye nini.

Katika utafiti wangu mdogo katika ya wenye kupenda kuku hawa wa aina hizi mbili nimegundua kuwa wapo wale wanaopenda kuku wa kienyeji ambao kila kukicha wanatamani waonje kuku wa kizungu ili waone kinachowafanya watu wengine kuwapapatikia ni nini. Na vile vile wapo wale ambao wamezoea kula kuku wa kizungu na kwa vile wanaikumbuka ladha ya kuku wa kienyeji hujikuta mara moja moja uswahilini ili kupata kipapatio au kisusio cha kuku wa kienyeji katika kile ambacho wanakiita "kukumbushia".
Mjadala huu kati ya wanaopenda kuku wa kienyeji au wale wanaopenda kuku wa kisasa unaonekana ni wa kudumu kwa muda ujao kwa kadiri ya kwamba kuku hawa wa aina hizi mbili wanaendelea kuwepo katika jamii moja au katika maeneo ya karibu. Wachunguzi wananidokeza kuwa dalili ya mmojawapo kutoweka siku za karibuni kwa kweli haipo.

Ninamini wenye kupenda kuku wa kienyeji hawawezi kuambiwa lolote juu ya kuku wa kizungu na wale wenye kupenda kuku wa kizungu japo hawakiri kudharau kuku wa kienyeji wanaamini kuwa "wana sababu zao" za kupenda kuku wa kizungu na hivyo hawasikii lolote la mtu.

Ni kwa sababu hiyo nimejifunza kuamini kuwa kila mtu na ladha yake. Kama vile tulivyoumbwa na ndimi mbalimbali ndivyo hivyo hivyo ladha zetu ziko tofauti tofauti na huwezi kujua kinachompa utamu mmoja chaweza kuwa ni kichungu kwa mwingine na hivyo ni vizuri kujua kuwa kile mtu apendacho kwake ndicho kina thamani.

Ushauri wangu kwa pande hizi mbili ni kuwa haijalishi ni kuku gani unawapenda au yupi umeamua kumfuga la maana ni kuhakikisha unawatunza vizuri, na kuwalinda na wezi na kuwafanya wajisikie kuwa wanathamani na nina uhakika siku ukitaka kuwachinja kwa mlo na wao wenyewe watazitangulisha shingo zao mbele ya kisu chenye makali kwa furaha na ukishawaandaa mezani nina uhakika hata mgeni huwezi kumkaribisha.

Kwa upande wangu bado ninaendelea na utafiti wa kuku gani hasa nifuge kwa kujihakikishia mlo wa muda mrefu.

Niandikie: mwanakijiji@mwanakijiji.com
 
Last edited:
kwa uzoefu wangu, kuku wa kienyeji anafaa kwa aina zote za mapishi, iwe kwa mchuzi, wa kukaanga au kuchoma. lakini kuku wa kizungu ni kukaanga na kuchoma tu na hiyo infanya kuku wa kienyeji kuwa bora. lakini huu ni mtazamo wangu tu.
 
Ushauri wangu kwa pande hizi mbili ni kuwa haijalishi ni kuku gani unawapenda au yupi umeamua kumfuga la maana ni kuhakikisha unawatunza vizuri, na kuwalinda na wezi na kuwafanya wajisikie kuwa wanathamani na nina uhakika siku ukitaka kuwachinja kwa mlo na wao wenyewe watazitangulisha shingo zao mbele ya kisu chenye makali kwa furaha na ukishawaandaa mezani nina uhakika hata mgeni huwezi kumkaribisha.

Kwa upande wangu bado ninaendelea na utafiti wa kuku gani hasa nifuge kwa kujihakikishia mlo wa muda mrefu.

Wenzako wamepata kanuni mpya ya kugeuza kuku wa kienyeji kuwa wa kizungu ndio maana wala hawahangaiki kuwachinja kuku wote wa kienyeji!

"Uwike usiwike kutakucha" - Msemo wa Kienyeji

"Dua la Kuku Halimpati Mwewe" - Methali ya Kienyeji
 
katika monekano wangu ni kwamba kuku wa kizungu na kuku wa kienyeji wote ni kuku ila utofautiwao unajitokeza pale kuku wa kienyeji anajitafutia chakula mwenyewe au anachakula mwenyewe na kuku wa kizungu anachakula kwa kuletewa karibu chakula.sio hivyo tu ila wanautofauti wa kwamba kuku wa kienyeji ananyama ngumu ukilinganisha na kuku wa kizungu kwani yeye huwana nyama nyepesi sana na huwa wanataga mayai mengi pia wengine huwaita kuku wa mayai na hata wa nyama.
ila tu mwisho wasiku utakubaliana na mimi yakuwa kuku ni kuku na wote ni jamii ya ndege .
 
kwa mahitaji ya kufuga kuku wa kizungu anafaa hasa kufugwa mijini na sio kijijini kwani wanahitaji matunzo ya hali ya juu na pia wataaramu hawapatikani vijijini.Ila wanaweza kumudu sehemu zote kama mahitaji yao yanapatikana bira shida yoyote.Pia kuku wa kienyeji wanafaa kufugwa vijijini kwasababu wanapenda kuchakula hasa kwenye kufukuafukua uchafu na aridhi ambavyo kwa mijini sirahisa kuwamudu kwasababu huchukuliwa kama wachafuzi wa mazingira na hivyo kupigwa vita na wakazi wa mijini.Hawa hawahitaji gharama zozote katika matunzo kwani huvumilia mazingira yote ya shida na raha penye magonjwa na pasipo na magonjwa.
 
Mimi binafsi niliacha kula kuku wa kizungu baada ya kula siku moja na kusikia harufu kama ya dawa ya sindano. Nilipofuatilia nikagundua kuwa ni kweli kuku wale walikuwa wamepewa dawa siku iliyotangulia. Wafugaji wanapaswa kuwa wakweli kwenye biashara ya kuku wa kizungu kwani wanaweza kuleta madhara ya kiafya kwa walaji. Sasa hivi nakula kuku wa kinyeji tu kuanzia supu hadi kuku choma jioni wakati napata bia zangu.
 
Mwanakijiji
Nimekukubali insha kiboko na inabidi akili izunguke kweli kweli kuichanganua insha hii.

Najua katika maisha kuna kitu ambacho lazima kikukute ambacho ni kifo. ila raha ya kifo si kujipeleka bali kupambana kiume mpaka kieleweke. Na kama ujuavyo kama mna mpango wa kumtoa kususio kuku wa kienyeji ni budi kupanga siku kabla au la ndo utaishia kufukuzana nae chini ya magari mabovu uswahilini, lakini jioni kama kawa atarudi home.

Kuku wa kienyeji kama usemavyo kwamba anajitafutia mlo na marafiki ina maana kipindi kifupi cha maisha yake anaishi kwa starehe na kujiamini huku akizitumainia nguvu zake za miguu kuchakurachakura mchangani akisaka punje za chuwa.

Sitaki kuamini kwamba wabongo wengi ni kama kuku wa kisasa. najitoa huko walah
 
Mwanakijiji
Nimekukubali insha kiboko na inabidi akili izunguke kweli kweli kuichanganua insha hii.

Najua katika maisha kuna kitu ambacho lazima kikukute ambacho ni kifo. ila raha ya kifo si kujipeleka bali kupambana kiume mpaka kieleweke. Na kama ujuavyo kama mna mpango wa kumtoa kususio kuku wa kienyeji ni budi kupanga siku kabla au la ndo utaishia kufukuzana nae chini ya magari mabovu uswahilini, lakini jioni kama kawa atarudi home.

Kuku wa kienyeji kama usemavyo kwamba anajitafutia mlo na marafiki ina maana kipindi kifupi cha maisha yake anaishi kwa starehe na kujiamini huku akizitumainia nguvu zake za miguu kuchakurachakura mchangani akisaka punje za chuwa.

Sitaki kuamini kwamba wabongo wengi ni kama kuku wa kisasa. najitoa huko walah

Unajuwa bro ukiisoma kwa hisia fulani hii Insha, na ukitumia elimu ya fasihi andishi, unaweza ukainasibisha na maisha ya Wabongo hivi leo.

Ila unatakiwa huwe makini kidogo, otherwise unaweza kuleta mchafuko wa hali ya hewa.
 
nimeisoma na kuidadavua hii insha, naamini mwanakijiji ametumia tamathali ya semi kuwakilisha ujumbe wake, naweza kusema aidha ametumia Taswira au Taashira(Symbolism). lakini kiukweli Mzee Mwanakijiji hakumaanisha kuku kama kuku.
 
Back
Top Bottom