Mheshimiwa Spika:
Jambo jingine linalonisumbua linahusu upatikanaji na matumizi ya fedha na michango mingine kwenye uchaguzi. Yameanza kujitokeza mawazo, pamoja na kuanza kujengeka utamaduni, kuwa uongozi unaweza kununuliwa kwa fedha. Kama ni kweli, tusipokuwa waangalifu, nchi yetu inaweza kuwekwa rehani kwa watu wenye fedha za kununua uongozi au wanaoweza kupata fedha za kufanya hivyo. Ni kweli kwamba fedha ni nyenzo mojawapo muhimu katika kufanikisha uchaguzi, kwa kila chama na kwa kila mgombea. Lakini, fedha
kutumika kununua ushindi si halali. Kwa maoni yangu hatuna budi kupiga vita utamaduni huu kwa nguvu zetu zote. Ni vema sasa tuanzishe mjadala wa kitaifa na hatimaye kuelewana kuhusu utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutafuta fedha za uchaguzi; na utaratibu halali, ulio wazi, wa chama au mgombea kutumia fedha hizo. Na utaratibu tutakaokubaliana uwe ni sehemu ya maadili ya uchaguzi katika uchaguzi wa kiserikali na ndani ya vyama vya siasa.