SoC02 Iwe usiku, iwe kuchwa usipoteze tumaini lako

SoC02 Iwe usiku, iwe kuchwa usipoteze tumaini lako

Stories of Change - 2022 Competition

SamNah

New Member
Joined
Aug 29, 2022
Posts
4
Reaction score
1
IWE USIKU, IWE KUCHWA USIPOTEZE TUMAINI LAKO.

Karibu katika Makala/Andiko hili ambalo kwa ukubwa limejikita kwa Wapambanaji, wanaonza kufikiri kuanza kupambana na wale waliopo kwenye mapambano na hata waliofanikiwa ambao wanahitaji kuwashika mkono wapambanaji wanaoanza.

Tunapozungumzia kupambana haimaanishi ugomvi, haimaanishi vita, hapana inamana ndogo kati ya nyingi ambao inalenga wapambanaji katika maisha, ingawa kuna wakati hayo mapambano ni zaidi ya vita, na ni zaidi ya ugomvi. Pamoja na yote kikubwa ni kuhakikisha tunatoka hali ya kawaida/Umasikini kimaisha kwenda hali nzuri zaidi.

Kwanini Usiku na Kuchwa? Nitagawa hizi nyakati mbili katika maeneo sita kwa Ujumla, ambapo kila moja itabeba tatu, Usiku itabeba Jioni/Usiku Mchanga, Usiku wa Manane, Na Alfajiri. Wakati huo Kuchwa pia itabeba tatu, Asubuhi, Mchana na Alasiri. Vipo viswahili vingi vya hizi nyakati lakini katika andiko hili nimechagua kutumia Kiswahili cha nyakati hizo kama ilivyoainishwa.

Twende pamoja nami, Tukianza moja baada ya nyingine si kwa umuhimu bali kwa Mpangilio wa fikra katika andiko hili, hii ni kutokana na ukweli kwamba katika maisha kila mtu anasehemu yake ya kuanzia kuishi kulingana na kutofautiana kwa vipato na historia za famila zetu, huyu ananzia hapa, huyu mwingine pale wakati mwingine anaanzia kule. Vitendawili visiwe vingi, naomba sasa niingie moja kwa moja kwenye upambanuzi wa hizi nyakati mbili kulingana na zilivyogawanywa kama ifuatavyo;

Jioni/Usiku mchanga, Huu ni wakati ambao tutauangalia kwa sehemu Mbili, ambazo ni yule Mtu anaanza kupambana, na yule ambaye anaanguka kutoka kwenye kilele cha Mapambano.

Tukianza na Mpambanaji anayeanza hapa hukumbana na giza totoro kwenye njia yake ya mwanzo, ni wachache ambao huwa wanaanza na kufanikiwa moja kwa moja au kwenda hatua nyingine, matokeo yake wengine hukata tamaa, atajaribu hili na lile akiona yote yanakwama anaamua kubaki na lawama pamoja na Imani za kishirikina akiamini huwezi fanikiwa bila hivo kitu ambacho si sawa, hii hatua ndio hujenga misingi na dira ya mpambanaji ukiifuzu pamoja na changamoto zote, mafanikio kwako yatakuja tu, kwa wale waliofanikiwa wengi huwa wanajisahau na kuwakatia au kuwakatisha tamaa wanaoanza mapambo kwa kuwa pengine wao hawakuanzia hiyo hatua, au kwakughubhikwa na kiburi cha mafanikio wao husahau ni kiasi gani au mara ngapi walitereza lakini hawakukata tamaa ya kupambana ndipo wakafika walipo. Nawasihi wanajamii kuwajenga na kuzidi kuwapa Nguvu wapambanaji wanaoanza.

Sehemu ya pili, ni mtu aliyekuwa kwenye kilele cha mafanikio kwa sababu za kutokuwa na misingi imara, ama kukosa ubunifu, ama kudoda kwa alilokuwa analifanya inapelekea katika njia zake kuanza kuona giza jepesi jepesi, hii inakuwa inaashiria kama anahitajika kujenga misingi upya au kuanza kitu alichokuwa anakifanya upya kabisa.

Usiku Wa Manane, Hapa pana kiza kinene, walionzia kupambana jioni ndipo hukumbana muda mwingine na hatima zao, Je unalofanya au uliloanzisha linasimama, linakubalika na watu, au linapingwa? Je umelifanyia utafiti wa kiina, wakatishaji tamaa wamekuzidi au umewazidi, Je umepima usahihi kwa ufasaha kile unachofikiria kukifanya au unachokifanya, unazichukuliaje Changamoto zote, hapa tunaweza pata mfano wa mtu analiyeanza kulima Nyanya, akazivuka hatua zote madhubuti na ngumu matunda yameanza anaingia kanitangaze, ugonjwa ambao ukiingia shambani kuutibu ni kazi ngumu, kwa ufupi katika mazingira ya kitu unachofanya umejipangaje kukabiliana na Changamoto zitakazoibuka kukirudisha nyuma kile unachokifanya, usichoke pambana kwa hali na mali. Wapo watu hukata tamaa katika mazingira haya, pengine ameangukia hapa kutoka alasiri au namna yoyote, waneni wanasema kiza kikizidi ujue mapambaziko yapo karibu.

Alfajiri, hapa tunaanza kuiona afadhari, ni pale tunapoona tumepita kwenye hatua ngumu mbili na matunda kwa mbali tunaanza kuyaona waswahili husema ni "Comfort Zone" kwa mpambanaji lazima uelewe ni sehemu salama lakini pia ni sehemu hatarishi, kwa kuwa ukibweteka unaweza rudi ulikotoka, kwa mjasiriamali au mpambanaji lazima maono yako yawe makubwa, usijenge nidhamu ya kuridhika jenga hitaji au nidhamu au tumaini la kuhitaji zaidi na zaidi, hii itakufanya mara zote uone hujafikia malengo, kwa ufupi hili ni eneo ambalo pamoja na kuanza kupambazuka linahitaji umakini wa hali ya juu ili uweze kuona mafanikio yako.

Asubuhi, hapa ndipo tunaanza kunusa faida ya tunayoyapambania, tunaanza kuona yale tunayoyafanya yanahitajika au yanaleta tija kwa ukubwa gani katika maisha yetu,ni sehemu ambayo inatakiwa nidhamu ya kuhakikisha ubora wa huduma na unaowahudumia, ni sehemu ambayo inakuhitaji utengeneze na kuboresha kichwa chako, ni sehemu ambayo inakuhitaji uwe makini kuhakikisha mambo yako hayakwami kwa sababu yoyote ile. Ni sehemu ambayo itakutoa kwenye jua tamu la asubuhi na kukupeleka jua tamu zaidi la mchana.

Mchana, Hapa Umeimarika, unawatu wanafaidi huduma yako huku nawe ukifaidi marejesho ya huduma unayotoa kwao, kumbuka hili jua ni kali, hakikisha unakuwa na kivuli cha ziada kulinda kazi yako na wateja wako hii itakupa nguvu ya kuhimili kazi zako kama mpambanaji, itakupa fursa ya kuyaona mafanikio yako kwa kina huku ukijishangaa ni mimi kweli? Kwa kuwa utakuwa unaikaribia kilele chako cha mafanikio, cha msingi na endelea kuwa na nidhamu na ufanyalo.

Alasiri, hapa ndipo mtu wanasema anamfumo wa maisha, kiufupi umefanikiwa, katika hatua zote ushatengemaa sehemu zote ulizopita umetengeneza mtiririko madhubuti wa mafanikio. Kitakachokufanya ufurahie zaidi hatua hii ni vile namna ulivyojenga nidhamu ya uaminifu na kuwainua watu katika mapambano yako, maana hao ndio mtaji wako Mkubwa katika mapambano. Jipongeze kwa kufikia hatua hii.

Mwisho hatutakiwi kukataa tamaa, hamna usiku uliodumu na kuchwa kusije wala hamna kuchwa kusikopelekea usiku.
Mapambano Yaendelee.
Ahsante kwa kusoma Makala hii.
 
Upvote 0
Back
Top Bottom