MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ametoa ufafanuzi kuhusu hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa usiku wa mwaka mpya na kuzungumzia mchakato wa katiba unaoendelea, na kusema rais hapaswi kulalamikiwa kwani yote aliyosema yamo ndani ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Jaji Warioba alitoa kauli hiyo kujibu kauli ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), iliyomlalamikia Rais Kikwete kuingilia kazi za Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Jaji Warioba alitoa ufafanuzi huo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari wakati akizungumzia tathmini ya kazi ya kukusanya maoni binafsi ya wananchi kupitia mikutano iliyomalizika Desemba 19 mwaka jana.
"Kuna kitu gani kipya alichosema rais? Yote aliyosema yapo kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, na mimi katika mikutano yangu yote nimeyaeleza na hakuna asiyejua," alisema Jaji Warioba ambaye ameshawahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais.
"Rais alielezea mchakato wote kuanzia kukusanya maoni, kuandaa rasimu, kufanyika kwa mabaraza ya katiba, Bunge maalum la katiba na kura ya maoni…haya yote yapo kwenye sheria ambayo wabunge waliipitisha," alisema Jaji Warioba wakati akijibu swali la mwandishi wa habari Jabir Idrissa aliyetaka kujua kauli ya tume kuhusu maoni ya baadhi ya wanasiasa kuwa rais aliingilia kazi zake.
"Hivi ingekuwaje kama rais angetoa salamu za Mwaka Mpya bila kuzungumzia mchakato muhimu kwa nchi kama huu wa katiba?" alihoji Jaji Warioba.
Akizungumzia mikutano ya kukusanya maoni iliyomalizika mwezi uliopita, Jaji Warioba alisema kazi hiyo ilianza Julai 2 mwaka jana na Tume yake imetembelea na kufanya mikutano 1,776 katika mikoa yote 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, jumla ya wananchi 1,365,337 walihudhuria mikutano hiyo na kati yao, 64,737 walitoa maoni kwa kuzungumza katika mikutano na wengine 253,486 walitoa kwa maandishi katika mikutano hiyo.
Alisema takwimu hizi hazijumuishi maoni yanayoendelea kukusanywa na tume yake kupitia posta, totuvi ya tume, mitandao ya kijamii na ujumbe mfupi wa simu za mkononi ambao hadi kufikia jana walipokea sms 16,261.
Kuhusu idadi ya wananchi waliojitokeza mikutanoni na kutoa maoni yao, mwenyekiti huyo alisema tume imeridhika na idadi hiyo na kufafanua kuwa kilichokuwa kinatafutwa ni hoja na kwamba haukuwa wakati wa kupiga kura.
Jaji Warioba alifafanua kuwa, katika awamu zote nne za mikutano ya kukusanya maoni, wananchi wametoa maoni kuhusu maeneo yote muhimu kama utawala, haki, maadili na mamlaka yao na mengineyo.
Akizungumzia hatua inayofuata, Jaji Warioba alisema kuwa kuanzia Jumatatu, tume hiyo itaanza kukutana na makundi mbalimbali kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu katiba mpya.
Makundi hayo ni vyama vya siasa; vyama vya kitaaluma; asasi za kiraia; taasisi za kidini, vyama vya wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara na makundi mengine mbalimbali.
|
|