Jamaa akaambiwa ruksa kumuoa…

Mtambuzi

Platinum Member
Joined
Oct 29, 2008
Posts
8,809
Reaction score
15,421
Ngoja niwamegee kesi hii kati ya Hasumati dhidi ya Bashirihussein na mwenzie na ni kesi iliyoripotiwa katika ripoti za kisheria za Tanzania za mwaka 1983.

Je ilikuwaje?

Katika kesi hii Mama raia wa India alikuwa ndiyo mlalamikaji na alikuwa anamshitaki mkwewe na binti yake.

Kisa cha kuwashitaki kilikuwa ni kwamba mkwewe alifunga ndoa na binti yake huyo mdogo aliyekuwa na miaka 14 wakati huo bila ridhaa yake na ya mumewe na vile vile alimpa mimba binti yake huyo na kumsababishia abadili dini kutoka katika dini yake ya Kihindu na kumsilimisha (kumfanya awe muislamu).

Mama huyu alikuwa anataka ndoa ibatilishwe na uamuzi wa mwanaye kubadili dini na kuwa mwislamu nao pia ubatilishwe. Na pia alitaka mkwewe apewe adhabu kama sheria ya kuwalinda wasichana ambao hawajaolewa (spinster protection act no. 5) ya mwaka 1970 inavyoruhusu, kutokana na kumpa mimba binti yake.

Katika kuichambua kesi hii kabla ya kufikia uamuzi, Jaji alisoma historia nzima ya kesi na alielezea jinsi gani aliufikia uamuzi katika kesi hii.

Jaji alisema kwamba mlalamikaji alikuwa anataka Mahakama imsaidie kuvunja ndoa ya mwanaye. Pili alitaka Mahakama imrudishie haki ya kuishi na mwanaye na mwisho mkwewe apewe adhabu kwa kumpa mimba binti yake na alitumia sheria namba 5 ya mwaka 1970 niliyoitaja awali, kusimika madai yake hayo....

Pia alitaka kujua kama mjumbe wa nyumba kumi aliruhusiwa kisheria kumhifadhi mwanaye usiku wa Julai, Mosi, 1980 na Julia 2, 1980.

Ushahidi uliotolewa ulionyesha kuwa mwanaye alikubali kubadili dini na kuwa mwislamu na pia alikubali kuoana na mumewe Juni 27, 1980 na walienda kwa Kadhi Mkuu kwa ajili ya suala hilo na aliwaruhusu. Hivyo binti huyo alipata jina jipya na kuitwa Fatima.

Tarehe 30/6/1980 siku tatu baada ya ndoa yao ya siri na baada ya kuporwa mke, kijana yule wa Kinzanibar aliamua kwenda kwa Kadhi ili kuchukua cheti cha ndoa na alilalamika kwa kadhi suala la kuporwa mke wake huyo.

Lakini aliamua kumpa barua ili aende kwa mjumbe wa nyumba kumi ili kesho yake tarehe 1/7/1980 aende Mahakamani.

Nia ya barua ilikuwa ni kumtaka mama mkwe na baba mkwe wake waende Mahakamani. Pili ilikuwa kumpa mamlaka mjumbe wa nyumba kumi amuhifadhi Fatuma usiku wa tarehe 1/7/1980 hadi 2/7/1980 ili kesho yake aweze kufika Mahakamani.

Katika Mahakama, suala la kwanza kuangaliwa lilikuwa ni uhalali wa ndoa na ili kujua kama ndoa ilikuwa ni halali au la, mahakama iliangalia kwanza kama kitendo cha kubadilisha dini kilichofanywa na Fatuma kilikuwa ni halali au la.

Mama Mkwe ambaye alikuwa ni mlalamikaji alitoa vigezo ifuatavyo:

Kwanza alisema kwamba binti yake ni Mtoto mdogo hivyo huwezi kujitolea maamuzi mwenyewe katika masuala ya ndoa pasipo uangalizi wa wao wazazi. Pili, si yeye wala mumewe hawakupewa taarifa kuhusu suala hili.

Kutokana na ushahidi wa paspoti ya mama yake Fatuma ilionekana Fatuma pia ni raia wa India na katika kujadili suala kuwa ni sheria gani itumike kati ya ile ya India na ya Zanzibar, Jaji alifafanua suala hili kwa kutumia kesi na vitabu mbalimbali

Mojawapo ya kesi zilizonukuliwa ni ile ya Barbara Simpson na katika kesi hii Mama ambaye alikuwa ni raia wa Uingereza alienda kuishi Kenya na walipofika huko binti yake aliyekuwa na umri wa miaka kumi na nne aliolewa na Patwa.

Mama wa binti wa Kiingereza aliomba Mahakamani Patwa amrudishe binti yake huyo.

Umuhimi wa kesi iliyonukuliwa ni kwamba maamuzi yaliangalia zaidi umri ambao mtu anakuwa huru kufanya maamuzi yake binafsi.

Hivyo mahakama iliona kwamba, hata katika kesi hii, msichana alikuwa na uwezo wa kuelewa maana ya jambo alilokuwa akilifanya na zaidi ya hapo alikwishafikia umri wa kufanya maamuzi sahihi na hakulazimishwa kufanya jambo hili kwa sababu japokuwa mwanzoni alihofia kuolewa kutokana na tofauti ya dini kati yake na ya mumewe, mwisho alikubali kuolewa na mumewe huyo na hata wazazi wake walipomuomba arudi nyumbanï alikataa na mama yake alipotishia kumtenga hakuwa na wasiwasi na alisema tayari ana mama mwingine ambaye ni mama mkwe wake.

Hivyo yote hii inaonyesha kuwa alikuwa na maamuzi binafsi na alikuwa anaelewa anachokifanya.

Katika suala la uhalali wa ndoa, Sheria ya Mohamedan inasema kwamba rukhsa ya Walii ni muhimu na kutokana na mathehebu ya Shafi ambayo ndiyo ilikuwa dini ya mlalamikiwa na mkewe, Walii huwa Baba wa binti au mwangalizi yeyote wa kiume wa binti huyo. Lakini walii huyo inabidi awe ni Mwislamu, hivyo hapa Walii alikuwa ni Kadhi aliyefungisha Ndoa na wala siyo baba wa msichana, kwa sababu baba wa msichana alikuwa ni mhindi aliyekuwa akiabudu katika madhehebu ya kihindu.

Pia Mahakama ilisema kwamba hakuna mahali ambapo maandiko ya kiislamu yanakataza mtu kuolewa na mimba ila kuna maandiko yanasisitiza iddat ili kujua kuwa mwanamke aliyeachwa au aliyefiwa na mumewe ana mimba ya mumewe huyo na hivyo kuzuia mtu asidai mimba ya mtu mwingine.

Kwa kuongezea mahakama ilisema kwamba spinster protection act no. 5 ya mwaka 1970 inatoa adhabu ya kifungo cha miaka mitano kwa watu wanaopeana mimba nje ya ndoa lakini hapa anayeumia ni mtoto atakayezaliwa kwa sababu atakulia jela na kulelewa jela kwa miaka yote mitano ya mwanzo na nia ya sheria siyo kumuumiza Mtoto ila kumlinda....

Kabla ya kumalizia suala la mjumbe wa nyumba kumi kumhifadhi binti lilipingwa na mahakama na mahakama ilisema kwamba mjumbe hakuwa na mamlaka hayo lakini ilimpa tu onyo kuwa asirudie tena kosa hilo.

Kwa kumalizia kama nilivyosema hapo awali sheria ya ndoa ya Tanzania ya mwaka 1971 inakataza watu wenye umri mdogo kuoana na inatoa adhabu za kifungo cha miaka miwili kwa washiriki. Na hii inaonekana katika kifungu cha 13 na 148 cha sheria hiyo. Lakini hata hivyo sheria hiyo katika kifungu chake cha kumi na saba inaruhusu "watoto" kuoana kama kuna mazingira Maalum.

Mfano katika kesi hii ambayo naijadili, ndoa ingewezekana kwa sababu ya mazingira maalum ambayo ni kuwa binti alikuwa na mimba na yeye na mumewe walikuwa wakipendana sana.

Kwa kuongezea pia nia ya mahakama inakuwa ni kumlinda msichana asirubuniwe na wanaume na kufanya jambo bila kujua matokeo yake, lakini kama ikionekana kuwa msichana huyo anaelewa anachokifanya kama ilivyoainishwa katika kesi hii Mahakama huwa haina kipingamizi cha zaidi.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…