JAMBO PEKEE NINALOLIOGOPA

josephdeo

Member
Joined
Nov 23, 2015
Posts
95
Reaction score
207
Wakati fulani nikiangalia documentary ya bilionea Billget iliyoitwa "inside the Billget brain" aliulizwa swali moja muhimu sana kwenye documentary yake kuwa ni jambo gani bilionea huyu analiogopa zaidi. Kwenye majibu yake anasema kuwa jambo ambalo analiogopa zaidi ni kuwa "siku akili yake itakapo acha kufanya kazi". Hili ndilo jambo ambalo billionea huyu analiogopa sana na pengine wengi wetu tunayo mambo ambayo tunayaogopa lakini hapa tumeonelea kuutaja mfano huu kuwa kama kielelezo tu juu ya kile ambacho tunakwenda kukizungumzia.

Leo hii ukimuuliza kila mmoja wetu lazima awe na kitu ambacho anakiogopa zaidi na kitu hicho kina maana kubwa zaidi kwake. Kuliko kwa wewe ambaye utayapokea majibu ya maswali hayo uliyo uliza. Leo hii ukiniuliza mimi ndugu Joseph Deogratius Migini ni jambo gani naliogopa zaidi kwenye maisha nitakujibu kwa ufupi kabisa kuwa jambo pekee ambalo naliogopa zaidi kwenye maisha ni "ukimya". Jambo hili lenye herufi au silabi chache zaidi ndilo jambo ambalo naliogopa zaidi kwenye ulimwengu huu.

Pia ukitaka kufahamu sababu za kwanini naogopa zaidi ukimya ni kuwa mara zote watu tumekuwa tukiingia kwenye matatizo kwa sababu hatukuyafahamu matokeo yake kama yatakuwa ni matatizo kwetu. Au watu tunaingia kwenye matatizo kwa sababu tu atukuambiwa au kupewa maarifa juu ya matatizo hayo na chanzo cha matatizo ya ulimwengu huu yanasababishwa na ukimya wa watu. Iweke kwa namna hii kuwa ni mambo mangapi ambayo wewe unayafahamu na unaona wengine wakiyakosea na wewe unanyamaza tu kwa kutokuwajulisha hao ambao wanayakosea ili wasiyakosee.

Kwa fikra zangu nafikiri ni mambo mengi sana hivyo sasa kwa mantiki hiyo ni kuwa kunyamaza kwetu ndio kunasababisha matatizo mengi zaidi yatokee. Ili kuweza kuitetea hoja yangu vyema ni vizuri nikakupa mfano ili tuweze kwenda sawa hiko hivi wakati fulani liliibuka wimbi la utapeli na utapeli huo kwanza ulianza wa simu na kisha wanakuuzia sabuni pili ukaja wa dhahabu feki na tatu ukaja wa uganga na mwisho ukaja wa kutapeliwa kwa njia ya simu.

Utapeli huu uliweza kujizolea umaarufu kwa sababu moja kubwa na sidhani kama wengi wetu tunatambua ni kuwa waliotapeliwa walikaa kimya bila kutoa taarifa kwa wenzao kwa kuhofia kuonekana washamba. Na kisha watu waliendelea kutapeliwa tu kwa kuwa walikaa na siri zao na kuogopa kuzitoa na laiti kama wangezitoa basi wangewezesha wenzao kutambua aina za utapeli huo na kisha kujiepusha nao au kujua namna ya kuukwepa utapeli huo.

Lakini watu walikaa kimya na baada ya kesi kuwa nyingi polisi basi serikali iliingilia kati swala hilo na kuanza kutoa elimu na matokeo yake ni kuwa utapeli huo ulipungua kwa kiwango kikubwa sana. Sasa kitu ambacho kinafanya niuogope sana ukimya ni kwa sababu unanyima nafasi kwa wewe kuweza kutoa elimu ya kile unachokifahamu kwa mwingine ili aweze kuyaepuka matatizo na badala yake unakificha na kusababisha matatizo kwa mwenzio. Matatizo yote tunayo yashuhudia leo ni kwa sababu ya ukimya wa watu fulani ambao wameamua kukaa na utatuzi walionao kwa sababu ya ukimya.

Kwangu jambo hili ndio naliogopa zaidi kwani mtu anaweza kuona kuwa unadondoka kwenye shimo na akakuacha mpaka udondoke ndio aje akuokote na kukupa pole wakati alikuwa na uwezo wa kukusaidia usidondoke. Ukimya umesababisha watu kukosa michongo kwa sababu wenye michongo wako kimya na wanao tafuta michongo hawawezi kuwafikia. Ukimya umesababisha propaganda kushika kasi kwenye maisha yetu ya kila siku kwa sababu wanaojua hizi ni propaganda hawazisemi na matokeo yake tunaumia ni sisi ambao tunazipokea propaganda hizo.

Kuna nukuu fulani sikumbuki vyema ni ya nani lakini nakumbuka vyema ilivyokuwa inasema kuwa "ulimwengu unateseka si kwa sababu ya watu wabaya bali ni kwa sababu ya ukimya wa watu wema". Watu wanaofahamu wengi wamekuwa wakimya uku wasio fahamu ndio wakiwa waongeaji na matokeo yake ni kuwa upotoshaji unashika kasi kwa watu kutambua yasiyo sahihi na kuacha yale yalio sahihi. Ukimya umesababisha watu kukosa elimu ya mambo muhimu kutoka kwa wanaojua kwa sababu watu wanaojua ni wakimya na hawapendi kuwaelimisha wengine. Huu ndio ukweli kuwa kuna mambo mengi ambayo yatupaswa kuelezwa lakini wanatakiwa kutueleza wao ndio wamekaa kimya.

Tunapaswa kufundishwa lakini wanaotakiwa kutufundisha ndio hao wamekaa kimya watu wanaotakiwa kutuongoza ndio hao wamekaa kimya. Ukimya ndio jambo pekee ambalo linabeba tafsiri kalibia zote kukubali, kukataa, dharau, kujifikiria na mambo mengine mengi. Haya yote tunayo yaona leo ni matokeo ya ukimya wa kizazi ambacho kimepita nyuma. Unaweza kuwa na jambo ambalo unaliogopa na wewe lakini kwa upande wangu ni ukimya hivyo natoa ushauri kwako usinyamaze ikiwa unaweza kuchangia kwenye kuwaondoa watu kwenye matatizo. Changia na ondoa ukimya nafsini mwako yatoe yale unayoyafahamu kwa wenzako ambao hayafahamu au hata kama yanayafahamu ila sio kwa namna ambayo wewe unayafahamu.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…