Mtazamo Wa Uislam Juu Ya Kuhesabu Idadi Ya Watu Katika Nchi (Sensa)
BISMILLAAHIR RAHMAANIR RAHIYM
MTAZAMO WA UISLAM JUU YA KUHESABU IDADI YA WATU KATIKA NCHI (SENSA)
UTANGULIZI
HISTORIA YA KUHESABIWA IDADI YA WATU NCHINI
Serikali ya nchi yetu imeshawahi kufanya Sensa yapata mara sita mara mbili wakati wa Serikali ya Kikoloni mwaka 1948 na 1957 na mara nne wakati wa Tanzania huru mwaka 1967, 1978, 1988 na 2002.
Sensa iliyofanywa na Wakoloni ya mwaka 1957 kipengele cha dini kilikuwepo ambapo Waislam walikuwa asilimia 58, Wakristo 32% na Wapagani 10% yaani wastani wa kila watu 3 basi Waislam ni 2 na Wakristo ni mmoja.
Sensa ya kwanza kufanywa na Tanzania huru ni ile ya mwaka 1967ambayo iliweka kipengele cha dini lakini la ajabu mara baada ya zoezi hilo, haikutajwa mara moja idadi ya watu kwa mujibu wa dini zao, lakini miaka ya baadae idara ya Taifa ya Takwimu ndio ikatoa idadi ya watu kwa mujibu wa dini zao na wakatangaza kwamba Wakristo ni asilimia 33.5, na Waislam asilimia 31.4 na Wapagani asilimia 34.3.
Hii imedhihirisha wazi kwamba takwimu hizi si za kweli na zitakuwa zimechakachuliwa hasa ukizingatia kwamba inadaiwa idadi ya Wapagani imeongezeka toka asilimia 10 zama za Mkoloni hadi kufikia asilimia 34 zama za uhuru na Wakristo kuonekana wengi kuliko Waislam.
Ajabu idadi ya Wapagani imeongezeka kwa kipindi cha miaka kumi tu, hii inaonyesha watu wengi wameacha dini zao na kuwa Wapagani na si rahisi kuamini hilo.
WAJIBU WA KUWASIKIZA NA KUWATII VIONGOZI
Uislam umeagizishia usikivu kwa watawala wetu endapo wametuamrisha yaliyo mema yanayomridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ
Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
"Enyi mlioamini Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wale waliopewa amri katika nyinyi." [An-Nisaa: 59].
Ni katika sehemu ya ibada kwetu Waislam kuwatii viongozi wetu lakini kwa sharti amri hizo zimemridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) endapo viongozi watatuamrisha maaasi, hatutakiwi kutii amri hizo kama alivyosema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
(لا طاعة لمخلوق في معصية الخالق😉 رواه البخاري
"Hakuna kumtii kiumbe katika kumuasi Muumba." [Imepokewa na Imaam Al-Bukhaariy].
Mafunzo haya yanapingana na yale yaliyomo ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo asili yake yaliandaliwa na wasio Waislam kama yalivyokuja katika kifungu cha 26 (i) cha Katiba ambayo inajulikana kama sheria mama ya nchi:
Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano
Sisi Waislam wa Tanzania tukiwa sehemu ya raia wa nchi hii tumelazimishwa kufuata na kutii Katiba na sheria za nchi bila ya masharti hata kama sheria hizo zinakhalifu sheria za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).
Kwa mfano sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kifungu namba 160 kinasema:
Mwanaume na Mwanamke wakiishi kwa muda wa miaka miwili mfulilizo huweza kuchukuliwa ni mke na mume mbele ya sheria japo kuwa hawakuwahi kufunga ndoa.
Hii kwa mtazamo wa Uislam ni sheria inayohalalisha uzinifu, kwa sababu ndoa katika Uislam haiwi halali mpaka kupatikane yafuatayo:
Walii, mahari, ‘Aqdi (mkataba wa ndoa), na mashahidi wawili.
Ndoa iliyotajwa katika sheria ya nchi si ndoa ni uzinifu na amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)
وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا
"Msiikaribie zinaa hakika hiyo (zinaa) ni uchafu na njia mbaya." [Al-Israa: 32].
Tukiangalia katika Uislam tunaona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameamrisha kuchukua idadi ya Waislam.
عن حذيفة رضي الله عنه قال:كنا مع رسول الله صلى الله عليه وسلم فقال:احصوا لي (وفي رواية البخاري اكتبوا لي😉 كم يلفظ الإسلام فقلنا يا رسول الله اتخاف علينا ونحن ما بين الستمائة إلى السبعمائة.قال.انكم لا تدرون لعلكم أن تبتلوا' قال:فابتلينا حتى جعل الرجل منا لا يصلي إلا سرا😉
رواه مسلم كتاب الإيمان باب الإسرا ر بالإيمان للخائف وللبخاري كتاب الجهاد باب كتابة الإمام للناس.
Imepokewa kutoka kwa Swahaba Hudhayfah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:
"Tulikuwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema: Nihesabieni (na katika mapokezi ya Al-Bukhaariy): Niandikieni ni wangapi waliotamka Uislam' tukasema: Ee Mtume wa Allaah unatuogopea (tusipatwe na adha) sisi ni baina ya watu mia sita hadi mia saba. Akasema: "Hakika nyinyi hamjui huenda mkapewa mtihani." (Akasema Hudhayfah): Tukapata mtihani mpaka katika sisi ikawa mtu hawezi kuswali isipokuwa kisirisiri." [Imepokewa na Imaam Muslim katika Kitaabul Imaan mlango wa kusirisha imani kwa aliye mwoga. Na amepokea Imaam Al-Bukhaariy kutoka Kitaabul Jihaad Mlango wa ‘Kiongozi kuandikisha idadi ya watu'].
Mwanachuoni wa zama zetu Imaam Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy katika kusherehesha Hadiyth hii amesema:
"Na Hadiyth hii ndio asili ya kila kinachojulikana leo kuhesabu idadi ya watu (na kujua idadi ya Waislam." [Mukhtaswar Swahiyh Muslim uk. 24].
Na katika zama za Khalifa wa pili ‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allahu ‘anhu) wanasimulia Wanachuoni wa historia kama Ibn Jariyr Atw-Twabariy katika kitabu chake ‘Taariykh Atw-Twabariy' na Mwanachuoni Ibn Al-Athiyr katika kitabu chake ‘Al-Kaamil fiyl Taariykh' kwamba Khalifa ‘Umar zama zake alianzisha zoezi la kuwahesabu watu waliokuwa chini ya Dola ya Kiislam kwa lengo la la kuwagawia Zakaah na ngawira zinazopatikana katika vita.
Hivyo hivyo Makhalifa waliokuja baada yake waliendeleza zoezi hili na kuwahesabu hata wasiokuwa Waislam ili kudhibiti idadi yao kwa mpango wa maendeleo.
Kutokana na kauli hizi, hii inaonyesha wazi kuhesabu idadi ya watu ni sehemu ya mafunzo ya Dini yetu na kuhesabiwa idadi ya Waislam ni jambo la wajibu kwetu sote.
Isitoshe Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndio sheria mama ya nchi ibara ya 18 (i) na (ii) inatambua haki ya wananchi kutoa na kupata habari:
18 (i) Bila ya kuathiri sheria za nchi kila mtu yuko huru kuwa na maoni na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa.
(ii) Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbali mbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.
Ni jambo la kusikitisha kusikia kwamba Serikali katika zoezi hili imeondoa swali dodosa la kuuuliza mtu dini yake kwa madai kwamba swali hili halina maana na litasababisha kuwagawa wa-Tanzania kwa misingi ya udini, hatimae uvunjifu wa amani kwani lengo la Serikali kuweka mipango ya maendeleo bila ya kujali dini au kabila ya mtu.
Lakini la kushangaza Serikali hiyo hiyo imetaka kujua idadi ya makanisa na Misikiti iliyopo nchini. (Angalia gazeti la Annur la tarehe 06 Julai 2012).
Kuna mantiki gani Serikali inayojigamba kwamba haina dini ihesabu idadi ya Misikiti na makanisa na ikatae kuhesabu idadi ya wenye makanisa na Misikiti. (Hatimae Serikali imeondoa kipengele hiki baada ya Waislam kulalamika).
Kwa kweli msimamo huu umeleta utata na hisia nyingi kwa Wa-Tanzania hasa Waislam kama ifuatavyo:
1. Mfumo Kristo unaendelea kufanya kazi yake wenye kukusudia kuficha idadi halisi ya Waislam ukiangalia takwimu za nyuma zote zimeashiria kwamba idadi ya Waislam ni wengi nchi hii kwa kuzingatia yafuatayo.
Kwanza: Uislam umeingia nchi hii tangu miaka 1200 iliyopita wakati Ukristo nchii hii umeingia si zaidi ya miaka 150 tu iliyopita.
Pili: Waislam katika Dini yao wameamrishwa kuoa zaidi ya mke mmoja hadi kuoa wake wanne. Hii imepelekea Waislam kuzaa sana na kupelekea idadi yao kuwa kubwa jambo ambalo halipo katika Ukristo kwa sababu Wakristo hawaruhusiwi kuoa zaidi ya mke mmoja.
2. Kuna takwimu zinatolewa na vyombo vya habari vya Serikali k.v. TBC zilizoonyesha kwamba idadi ya Wakristo ni kubwa kuliko Waislam na taasisi nyingine zisizo kuwa za Kiislam zikieneza propaganda hizo kwa malengo ya kupotosha ulimwengu ili kuhalalisha dhulma wanazofanyiwa Waislam kwa madai kwamba wao ni wachache kuliko Wakristo.
Cha kusikitisha sana ni kuona baadhi ya Mashekhe nchi hii wamekuwa na msimamo wa kuunga mkono Serikali na Kanisa kwa madai kwamba kipengele cha kuulizwa dini ya mtu hakina faida yoyote.
ATHARI ZA KUONDOLEWA KIPENGELE CHA DINI KATIKA SENSA BAADA YA MWAKA 1967
Baada ya Serikali kuondoa kipengele cha dini katika Sensa katika maswali dodosa ya Sensa, hivyo kushindwa kutoa takwimu sahihi zinazoonyesha idadi halisi ya Waislam, Wakristo na Wapagani katika nchi hii.
Hii inapelekea kuibuka taarifa zisizo rasmi kutoka kwenye taasisi mbali mbali, idara, wizara na mashirika mbali mbali ndani na nje ya nchi, kila mmoja kujipa mamlaka ya kutangaza takwimu zake za kubuni bila ya kuwa na machimbuko ya taarifa sahihi. Kila mmoja alitoa takwimu zake kwa malengo yake ya kisiasa, kidini na kiuchumi.
Ni hivi karibuni Serikali ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania imetangaza azma yake ya kufanya zoezi la kufanya Sensa ya watu na makazi nchi nzima kwa malengo ya kupanga mikakati ya maendeleo ili kuboresha maisha ya Wa-Tanzania.
BAADHI YA TAKWIMU BANDIA ZINAZOENDELEA KUTOLEWA NA TAASISI MBALI MBALI NDANI NA NJE YA NCHI
1. Shirika la Utangazaji la Serikali la Taifa (TBC) kupitia televisheni yake ya taifa TBC1 siku ya sherehe ya Muungano 26 April 2012 ilitangaza kwamba idadi ya Waislam nchini ni asilimia 32, Wakristo ni asilimia 52 na Wapagani ni asilimia16, Takwimu hizi zinamaanisha kwamba yaani sisi Waislam tunazidiwa na Wakristo kwa tofauti ya asilimia 20!
2. Kanisa Katoliki nchini katika tovuti yake ya
www.rcnet [1], wanadai kwamba mwaka 2008 Wakristo walikuwa asilimia 44, Waislam asilimia 34 na Wapagani asilimia 22. Hii inaonyesha kwamba Wakristo wamewazidi Waislam kwa tofauti ya asilimia 10!
3. Bodi ya taifa ya Utalii (TTB) katika tovuti yake ya www. Tanzaniatourismboard.com/about /Tanzania /religion, mpaka tarehe 20 Juni 2012 ilikuwa inaonyesha Wakristo ni kati ya asilimia 40 hadi 45, Waislam kati ya asilimia 35 hadi 40 na waliosalia ni Wapagani!
Lengo la kuwaonyesha Watalii idadi hii ni kuwapa picha Watalii ambao wengi wanaokuja katika nchi hii ni Wazungu ambao ni Wakristo, kwamba nchi hii ni ya ndugu zao, hivyo wafanye watakavyo. (Taarifa hii baada ya Waislam kulalamika, imeondolewa kwenye tovuti hiyo ili kuficha ukweli).
4. Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani kwenye tovuti yake
www.state.gov [2] inasema mwaka 2011 Wakristo Tanzania walikuwa asilimia 62, Waislam asilimia 34 na Wapagani asilimia 4 yaani Wakristo wamewazidi Waislam kwa asilimia 28!
5. Shirika la kijasusi la Kimarekani (CIA) kwenye tovuti yake
www.cia.gov [3] linadai kwamba mwaka 2005 Waislam nchini Tanzania walikuwa asilimia 52 Wakristo asilimia 38 na Wapagani asilimia 10. Sisi Waislam ni wengi nchi hii tukiwazidi Wakristo kwa asilimia 14. Mwaka 2012 shirika hilo linadai kwamba Waislam nchi hii ni asilimia 35, Wakristo ni asilimia 30, na Wapagani asilimia 35. Hivyo Waislam tulikuwa wengi tukiwazidi Wakristo kwa asilimia 5. Kwa kipindi cha miaka 7 tu, sisi Waislam tumepungua kiasi cha asilimia 9, au wakiristo kuongezeka kwa zaidi ya aslimia 9 kwa kipindi cha miaka 7!!
6. Shirika la kimataifa la Nationmaster katika tovuti yake
www.nationmaster.com [4] linadai kwamba mwaka 2012 Waislam Tanzania ni asilimia 35%. Wakristo asilimia 35% na Wapagani ni asilimia 30%. Yaani Waislam na Wakristo wamekuwa sawa kwa idadi.
Takwimu hizo hapo huu zinaonyesha wazi kwamba hakuna ukweli wowote juu ya taarifa zilizotolewa ambazo ni kazi ya kubuni tu, kwa sababu hakuna machimbuko sahihi tyaliyotolewa na idara ya Takwimu, kujua idadi ya watu kwa mujibu wa dini zao.
Kwa mnasaba huu tunapenda kuwakumbusha faida angalau chache ambazo faida hizo zinarejea kwanza kwa Waislam wenyewe pili kwa Serikali na watu wa dini nyingine kwa ujumla nazo ni kama zifuatazo.
(a) Kujua idadi ya Waislam kama wameongezeka ni dalili kwetu kwamba Uislam unasonga mbele katika ulinganizi (da'wah) na kwamba agizo la Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) limetimizwa
رواه أبوداود والنسائي مكاثر بكم الأمم😉 الودود الولود فإني (تزوجوا
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
"Oeni wanawake wenye kupendeza na wenye kuzaa kwani mimi nitajivunia na wingi wenu". [Imepokewa na Abu Daawuud na An-Nasaaiy].
(b) Kujua idadi ya Waislam kama wamepungua hii inaonyesha kwamba kuna mapungufu katika shughuli za kulingania, hivyo inabidi tujipange upya kulinda afya zetu na kufanya juhudi ya kueneza Uislam. Au Waislam tunakufa wengi au tunatoka katika Uislam.
(c) Ni matarajio yetu Waislam kwamba Mahakama za Qaadhi zitaanzishwa hivyo kujua idadi ya Waislam kutasaidia kufunguliwa Mahakama ya Qaadhi hasa ukizingatia kwamba Serikali kwa sasa haina uwezo mkubwa wa kifedha wa kuanzisha mahakama hizo kila pembe ya nchi, hivyo itaangalia ni wapi penye Waislam wengi ipate kuanzisha na hili halijulikani ila kwa Sensa sahihi.
(d) Serikali sasa imeruhusu kuanzishwa kwa Benki za Kiislam, bila shaka Wawekezaji wanaotaka kuanzisha Mabenki ya Kiislam watataka kujua ni maeneo gani katika nchi yenye wateja wengi ili waanzishe miradi hiyo kwa faida za kibiashara, bila shaka maeneo hayo ni yale yenye Waislam wengi, itabidi wakitaka kujua hilo waiulize Serikali ambayo itawapa takwimu sahihi ni wapi nchini penye Waislam wengi? Isitoshe mabenki ya Kiislam yakianzishwa hayabagui wateja wake kwa msingi wa kidini hivyo watafaidika wa-Tanzania wote kuinua hali za maisha yao kama vile kupewa mikopo isiyo na ribaa n.k.
(e) Kujua idadi ya watu kwa mujibu wa dini zao inasaidia Serikali kupanga mipango wa maendeleo, kwa mfano ugavi wa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za ibada, shughuli za kidini, maeneo ya makaburi. Serikali kwa sasa imekuwa ikifanya upendeleo kwa kuwapa Wakristo maeneo makubwa ya ardhi kwa ajili ya makanisa na makaburi, hata katika miji ya Waislam wengi na hii inajenga hisia ya dhulma, lakini kama ingegawa ardhi kwa uwiano sahihi basi hisia hizi zisingekuwako na hili haliwi ila baada ya kuchukuliwa takwimu sahihi kikiwemo kipengele cha kuuliza dini ya mtu na madhehebu yake.
(f) Serikali ya Saudi Arabia katika kudhibti idadi ya wanaokwenda kutekeleza ibada ya Hijjah ambapo kwa sasa kila nchi inataka kupeleka idadi kubwa inavyowezekana. Ili kupunguza msongamano Serikali ya nchi hiyo inatoa nafasi ya idadi maalum (quota) kwa kila nchi kulingana na wingi au uchache wa Waislam katika nchi hiyo.
Waislam wa Tanzania siku zote za nyuma tukipewa nafasi ndogo kwa sababu hakuna takwimu sahihi za kujua idadi ya watu.
MADHARA YANAYOWAFIKA WAISLAM KWA KUTOKUWEPO TAKWIMU SAHIHI JUU YA IDADI YAO
1. Kuwepo kwa idadi kubwa ya Wakristo katika nyadhifa mbali mbali Serikalini na idara zake, taasisi na mashirika ya Umma kwa hoja ya kwamba Wakristo ni wengi kuliko Waislam.
2. Takwimu za bandia zimetumika katika maamuzi mbali mbali ya kitaifa kwa lengo la kuwakwaza Waislam katika mambo ambayo yana maslahi na wao. Kwa mfano Waislam katika nchi hii kwa muda mrefu wamedai kujiunga na Umoja wa nchi za Kiislam (OIC) moja ya sababu ya kutosikilizwa madai yao kwamba Waislam katika nchi hii ni wachache. Haya yamesemwa na Professa Mwesega Baregu akijenga hoja kuhusu Tanzania kuzuiwa kujiunga na OIC alisema:
"Sharti la nchi kujiunga na umoja huo ni kuwa na idadi kubwa ya Waislam kuliko dini nyingine. Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa idadi ya Waislam Tanzania ni ndogo kulinganishwa na idadi ya dini nyingine. (Angalia gazeti la Mwananchi Jumatano 5 Novemba 2008 ukurasa 5).
Hii inaonyesha wazi kwamba madai mengi ya Waislam wa Tanzania yanapuuzwa kwa madai ya uchache wao kwa kuzingatia takwimu hizo za bandia.
Haitoshi kwa wakuu wa idara ya Takwimu ya Serikali kukanusha takwimu hizo tu si sahihi na hii limefanywa ni baada ya Waislam kulalamika, kabla ya hapo hakukuwa na makemeo yoyote. Inapaswa kwa sasa Serikali kuongeza kipengele cha dini ili kuukata mzizi wa fitna.
UDHAIFU WA HOJA ZA SERIKALI KATIKA KUKATAA KUINGIZA KIPENGELE CHA DINI KATIKA SENSA NA MAJIBU YAKE
1 Serikali haiwezi kurejesha kipengele hicho kwa kuwa ‘Baba wa Taifa' alikiondosha ili kujenga umoja wa Kitaifa. Haya yalisemwa na viongozi wa Serikali katika mkutano wake na viongozi uliofanyika Dodoma tarehe 11 Juni 2012.
2 Kuhesabiwa watu kwa msingi wa dini zao kutapekelekea uvunjifu wa amani na utulivu nchini.
3 Serikali haipangi maendeleo kwa kuangalia dini (haya yalisemwa na Waziri katika ofisi ya Rais Sera na Uhusiano, Stephen Wasira katika semina hiyo Dodoma na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kujibu maswali ya papo kwa papo bungeni tarehe 09 August 212.
4 Serikali ya Tanzania inafuata utaratibu wa Sensa wa Kimataifa ambao ni kuhesabiwa watu bila ya kuhusisha kabila wala dini zao.
MAJIBU
1. Anayotamka ‘Baba wa Taifa' si wahyi (ufunuo) kutoka mbinguni, ni yeye ndie alietuletea sera ya chama kimoja, na azimio la Arusha na siasa ya Ujamaa na kujitegemea. Sera sote hizo zimeshindwa na hili la kuondoa kipengele cha dini badala ya kuleta umoja wa kitaifa umeleta mtengano kwa sababu limeanza kuamsha hisia za dhulma na upendeleo dhidi ya Waislam na kuibuka takwimu zisizo sahihi. Na kwa hilo nalo Serikali ni lazima iweke pembeni fikra hizi za ‘Baba wa Taifa' ili kuokoa nchi na uvunjifu wa amani.
2. Kuacha kukitia kipengele cha dini katika takwimu ya kitaifa ndio ambako kunaweza kuvunja amani hasa pale ambapo baadhi ya raia kuhisi kwamba wanabaguliwa kwa madai kwamba wao ni wachache na wanadhulumiwa na kunyimwa haki zao nyingi. Hii ndio inaweza kuleta uvunjifu wa amani. Isitoshe nchi nyingi zikifanya takwimu zinaweka kipengele cha kujua dini za watu. Nchi kama Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, India, Kenya, Uganda n.k. zinafanya hivyo na hujasikia hata nchi moja duniani kumetokea uvunjifu wa amani kwa sababu hiyo.
3. Si kweli kwamba Serikali haipangi maendeleo yake kwa kuzingatia dini kwa sababu Serikali haina dini. Ukweli ni kwamba Serikali inapanga maendeleo yake kwa kuzingatia sana dini lakini ni ya kikristo. Mfano ni ule mkataba wa maelewano baina ya Serikali na Kanisa (MOU), ahadi ya Serikali ni "Kushirikiana na Makanisa kupanga sera na maendeleo ya sekta ya Elimu, Afya na huduma za Jamiii." Je hii si mipango ya maendeleo. Mkataba huo (MOU) umetoa mamlaka ya kuundwa kwa tume ya kikristo ya huduma ya Jamii (CSSC) kwa lengo la kuunda sera zinazofanana kwa huduma za makanisa na afya na elimu wa makubaliano na Serikali ya Tanzania.
Pia mkataba huo umelenga kuwa na utekelezaji sawa kwa Serikali na makanisa katika maendeleo ya jamii. Je, huu si mpango wa maendeleo baina ya Serikali na Wakristo.
Katika kifungu cha 11 cha mkataba huo kinasema:
"Serikali ni lazima itoe nafasi za ajira katika vyuo vyake vya Ualimu (TTC) kwa Wakufunzi wa kikristo kufundisha watu wataofuzu kama Walimu kwa ajili ya shule za Makanisa zilizoanzishwa."
Je, hii si mipango ya maendeleo kwa kuzingatia dini?
Kutokana na makubaliano hayo baina ya Serikali na kanisa, imelazimika Serikali kuyapa makanisa mabilioni ya fedha za wa-Tanzania kila mwaka katika utekelezaji wa mkataba huu. Mfano mwaka 2008 Serikali iliyapa makanisa jumla shilingi bilioni 170 (Gazeti la Jambo Leo la Jumapili 20/03/2011) liliandika hivi:
"Mwaka 2009 Serikali iliyapa makanisa shilingi bilioni 45. Mwaka 2010 iliyapa shilingi bilioni 61.9."
Kwa maana hiyo Serikali kuanzia 2008 hadi 2011 imeyapa makanisa na taasisi zake shilingi billioni 331. Jee Waislam na taasisi zake wamepewa nini?
Pia iweleweke kwamba zaidi ya asilimia 54 ya bajeti ya Wizara ya Afya inakwenda kwenye vituo vya Afya, zahanati, mahospitali na taasisi nyingine za afya za kikristo. Je fedha hizi zinaweza kutoka bila ya Serikali kuwa na mipango ya maendeleo?
4. Hoja ya kwamba Serikali inafuata mpango wa Sensa wa kimataifa unaiohusisha dini wala kabila si ya kweli kwa sababu utafiti unaonyesha kwamba Umoja wa Mataifa unataka Sensa iwe na kipengele cha dini, kabila, utaifa na lugha n.k. Hii inasaidia kuleta ufahamu na kujuana na hili limebainishwa katika Quran pale Allaam (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliposema:
يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنَّا خَلَقْنَاكُم مِّن ذَكَرٍ وَأُنثَىٰ وَجَعَلْنَاكُمْ شُعُوبًا وَقَبَائِلَ لِتَعَارَفُوا ۚ إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ
"Enyi watu Hakika Sisi tumewaumbeni kutoka na Mwanamme (Aadam) na Mwanamke (Hawaa) na tumewajaalieni mataifa na Makabila mbali mbali ili mpate kujuana hakika mbora wenu mbele ya Allaah ni Mchaji Allaah zaidi katika nyinyi." [Al-Hujuraat: 13].
Ili kupatikana Sensa iliyo sahihi kitengo cha Sensa cha Umoja wa mataifa kimetoa maelekezo yafutayo kwa nchi wanachama zinazotaka kufanya Sensa. Kipengelle nambari 2.109 hadi 2.111 chasema hivi:
"For the benefit of users of the data who may not be familiar with all of the religions or sects within the country as well as for the purposes of international comparability, the clasifications of the data should show each sect as a sub category of religion of which it forms a part. A brief statement of the tenets of releigions or sects that are not likely to be known beyond the country or region would also be helpful." (
www.unistats.un.org [5]).
Tafsiri
"Kwa faida ya watumiaji wa Takwimu ambao wanaweza wakawa hawafahamu dini zote na madhehebu yote yaliyopo katika nchi, vile vile kwa madhumuni ya ulinganishaji wa kimataifa, uchambuzi wa takwimu lazima uonyeshe kila dhehebu kama sehemu inayounda dini nzima kwa ujumla wake. Maelezo mafupi ya waumini wa dini au madhehebu ambayo yanawerza yakawa hayafahamiki nje ya nchi au ukanda yangeweza kuwa ni msaada. (Angalia tovuti
www.unistats.un.org [5]).
Hii inaonyesha wazi kwamba Umoja wa Mataifa wenyewe wanataka kipengele cha dini kuwepo kwenye Sensa kwa faida ya wote. Kwa nini basi Serikali ya Tanzania ikatae kuweka kipengele cha dini katika Sensa ilhali yenyewe ni mwanachama mwenye kufuata mikataba ya Umoja wa Mataifa?
WAISLAM KUTOKUWA NA IMANI NA IDARA YA TAKWIMU YA SENSA ILIYOPO HIVI SASA:
Waislam hawana imani na idara ya Takwimu na tume yake ya Sensa kwa kukaa kimya kwake juu ya takwimu zilizotolewa za bandia kwa lengo la kupotosha ulimwengu kwamba Wakristo nchi hii ni wengi kuliko Waislam ni dalili kwamba idara hii inashiriki kueneza propaganda hizo.
Isitoshe matokeo ya Sensa katika baadhi ya mikoa yenye Waislam wengi, kwamba idadi ya watu ni ndogo na haiongezeki. Mikoa yenye Wakristo wengi idadi ya watu ni kubwa sana.
Mfano mzuri ni katika Sensa iliyofanyika mwaka 1988, mkoa wa Tanga idadi ya wakazi wake ilikuwa 1,500,000 (milioni moja lako tano) na Sensa nyingine ilipofanyika mwaka 2002 idadi ya watu mkoani humo ilibaki kuwa hiyo hiyo yaani 1,500,000. (milioni moja laki tano).
Hii ina maana katika kipindi cha miaka 14 kutoka 1988 hadi 2012 hajaongezeka katika mkoa wa Tanga hata mtu mmoja na Serikali hadi leo haijaeleza sababu za kutoongezeka idadi ya watu katika mkoa huo, ni watu wanakufa sana au hawazaani. Hili ndio limeleta mashaka kwamba takwimu zinachakachuliwa kwa makusudi kwa lengo maalum.
Je, inafaa kisheria kushiriki katika zoezi la Sensa lisiloziingatia idadi ya watu kwa msingi ya dini yao?
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam)
(من رأى منكم منكرا فليغيره بيده فإن لم يستطع فبلسانه فإن لم يستطع فبقلبه وذلك أضعف الإيمان😉 رواه مسلم
"Anayeona ovu katika nyinyi alizuie kwa nguvu, akishindwa aseme, akishindwa achukie na huku kuchukia ni dalili uya udhaifu wa imani." [Imepokewa na Imaam Muslim].
Kususia ovu ni katika mafunzo adhimu aliyofundisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), hivyo basi endapo Waislam wamebainikiwa na lengo la Serikali kudhulumu, kudhalilisha Uislam na Waislam basi hatuna budi kususia zoezi hili katika njia ya kushinikiza Serikali ilinde maslahi ya Waislam.
Hili si jambo geni kwani kuna wakati Serikali ilitangaza nia yake ya kufuta misamaha ya kodi kwa mashirika na taasisi za kidini. Kanisa kwa sababu lilikhofia kuwa muathirika wa kwanza ni kanisa, liliweza kuishinikiza Serikali na kwa muda mfupi tu Serikali ilirejesha misamaha ya kodi pamoja na kwamba Taifa linakosa mapato makubwa kwa kuruhusu misamaha ya kodi.
Ni wazi kwamba Waislam ambao ni wengi nchi hii kwa pamoja wakiamua kususia zoezi hili la Sensa, basi hakutokuwa na takwimu sahihi na huku pia itakuwa ni kukiukwa kanuni za Umoja wa Mataifa ambazo zimetaka kila nchi mwanachama kuchukua idadi ya watu ikiwa ni pamoja na kujua dini zao na madhehebu yao.
Shime Waislam! Mashaykh wote wameunganika kuitaka Serikali iweke kipengele cha dini katika hili, la sivyo Waislam wote hawatoshiriki zoezi la kuhesabiwa. Na hili ni katika kutekeleza agizo la Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala).
فَلَا تُطِعِ الْكَافِرِينَ وَجَاهِدْهُم بِهِ جِهَادًا كَبِيرًا
"Wala msiwatii Makafiri na pambana nao kwa (Jihaad ya hoja ya Qur-aan) Jihaad kubwa." [Al-Furqaan: 52].
Tuachane na wale Mashekhe ambao wameweka maslahi ya matumbo yao mbele kuliko maslahi ya Dini. Pia tusiogope vitisho vinavyotolewa na baadhi ya Wakuu wa baadhi ya Waislam kwa hoja ya kwamba wanaleta uchochezi.
Waislam tujue kwamba hakuna sheria yoyote inayotaka mtu anayesusuia Sensa aadhibiwe, atakayeadhibiwa ni yule tu atakayezuia kwa mabavu kufanyika zoezi hili na haya yametamkwa na Mkurugenzi wa idara ya Takwimu nchini. (Rejea tamko la Mkurugenzi wa Idara ya Takwimu alilotoa katika Semina na Masheikh iliyofanyika Dodoma tarehe 30-07.2012).
Pia wito unatolewa kwa kila aliyekusudia kushiriki kwa njia ya yoyote ile, hata kwa njia ya ukarani wa kazi ya kuhesabu kwa kuweka maslahi ya tumbo mbele amche Mola wake juu ya hilo katika kutekeleza agizo la Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ
"Na msishirikiane katika dhambi na Uadui." [Al-Maaidah: 2].
Imekusanywa na:
Shaykh Saalim A. Barahiyaan. (LLB Shariah, LLM Sharia & Law)