Wizara ya Afya Tanzania
Official Account
- Oct 1, 2020
- 58
- 127
NA EMMANUEL MALEGI-MOROGORO
Shule zote nchini zimepigwa marufuku kuwapa wanafunzi (wasichana balehe) dawa aina ya Folic Acid badala yake zimesisitizwa kuhakikisha zinawajengea uwezo wa kulima maboga na mbogamboga katika bustani zao.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alipokuwa akihitimisha kilele cha Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki inayojumuisha Mikoa ya Dar
Es Salaam, Pwani, Tanga na Morogoro ambayo yalifanyika Mkoani Morogoro.
Waziri Ummy alisema ni marufuku kuwapa wanafunzi na wasichana balehe vidonge hivyo na kwamba fedha zinazotolewa kwa ajili ya kununua dawa hizo zitumike kuanzisha bustani shuleni ili kuzalisha vyakula vinavyotoa madini hayo.
“Mbali na kuanzishwa kwa bustani shuleni lakini pia fedha
hizo zinaweza kupelekwa kwa vijana ili waanzishe miradi ya bustani za mboga kwa ajili ya kuzalisha mazao yanayozalisha asidi hiyo yakiwemo maboga, matunda na hata karoti badala ya kutoa vidonge kwa wanafunzi,” alisema Ummy.
Pamoja na hayo, Waziri Ummy alisema utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonesha kila mtu anatakiwa kunywa nusu lita ya maziwa sawa na lita 180 kwa mwaka, lakini kwa sasa kila mtu anakunywa lita 40 kwa mwaka sawa na vijiko 10 vya chai kwa siku.
Akizungumzia hali ya udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano nchini, alisema umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2014 hadi asilimia 31.8 mwaka 2018 licha ya kuwa jitihada zinatakiwa kuendelea kuchukuliwa.
Aidha, aliupongeza Mkoa wa Morogoro kwa kuwa mwenyeji wa maonesho hayo ambayo yamekuwa chachu ya ukuaji wa kilimo, uvuvi na ufugaji pamoja na ujasiriamali nchini.
Aliwataka waratibu wake kutoishia hapo na badala yake ujuzi huo upelekwe vijijini
kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo muhimu ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia pato la taifa.
Jarida la Wizara ya Afya (Toleo la 2) sasa lipo mtandaoni. Pata nakala ya jarida hili ili uhabarike na taarifa mbali mbali za Sekta ya Afya nchini. Kwa kubofya link (https://afyablog.moh.go.tz/.../jarida-la-wizara-ya-afya... ) utaweza kupakua (download) moja kwa moja jarida hili na kuingia kwenye kifaa chako. Jarida hili pia linapatika kwenye mitandao yote ya Wizara ya Afya pamoja na tovuti kuu www.moh.go.tz
#TumekusogezaKaribu