SoC04 Je, hatuhitaji nishati ya mkaa? Basi tutumie gesi yetu!

SoC04 Je, hatuhitaji nishati ya mkaa? Basi tutumie gesi yetu!

Tanzania Tuitakayo competition threads

Adili Utotole

Member
Joined
Jul 20, 2022
Posts
14
Reaction score
14
Tunapozungumzia ukuaji wa maendeleo hapa nchini,hatuwezi kusahau matumizi ya nishati mbadala ya gesi safi ya kupikia majumbani.

Inakadiriwa zaidi ya hekta 469,420 ya misitu huharibiwa kila mwaka kutokana na ukataji miti kwa ajili ya matumizi ya nishati ya mkaa na kuni. Zaidi ya asilimia 16 ya ardhi inakabiliwa na ukame unaosababisha jangwa katika maeneo mengi ya nchi.Hali hii inachangiwa na gharama kubwa ya upatikanaji wa nishati ya gesi ambayo wananchi wengi kwa sasa wanaona ndio suluhisho la kuondokana na matumizi ya nishati ya misitu ambayo ina gharama ndogo na rahisi kupatikana.

Lakini kwangu mimi ambaye nimetumia mkaa na kuni takribani miaka 25 sasa,naona gesi ndio mkombozi wa kweli ili tuweze kumaliza tatizo la ukataji wa miti ,ukizingatia gesi hupatikana chini ya ardhi na huhitaji utalaamu zaidi ili kuipata, hata hivyo pia kuni na mkaa kwa miaka ya hivi karibuni kwa upande wa mijini bei imezidi kupanda maradufu, kutokana na watu wa maliasili kuweka sheria kali na kukamata watu wanaojihusisha na Biashara hiyo.

Mara kadhaa nimeshuhudia wafanyabiashara wa mkaa na kuni wakiporwa vyombo vyao vya usafiri kama baiskeli na pikipiki lakini pia kutaifisha bidhaa zao.Hali hii imeenda mbali zaidi kupelekea kuwekeana uhasama na kusababisha vurugu kati ya askari misitu na wafanyabiashara hao. Siku moja niliwahi kuona askari wakitumia mabomu ya machozi kukimbizana na wauza mkaa na wao wakijihami kwa kurusha mawe ili kunusuru mali zao, hii nadhani ni hatari zaidi.

Katika mkutano uliofanyika Mei nane mwaka huu wa 2024 jijini Dar es salaam, katika uzinduzi wa mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia 2024--2034 , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ,aliagiza na kusisitiza Taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya mia moja, kutumia nishati t gesi kama njia nzuri ya kupunguza uharibifu wa misitu.

Je kama jamii tupo tayari kutumia nishati ya gesi badala ya mkaa au kuni? .Jibu ni NDIO tena kwa herufi kubwa. Mara nyingi tumekuwa tukiona wanaotumia Gesi kupikia kama watu fulani wenye kipato kikubwa kwa sababu , ukweli ni kwamba ukihitaji gesi ni lazima uwe na fedha tofauti na kuni ambazo unaweza kuzipata hata nyuma ya nyumba kwa waishio vijijini.

Nikiwa kama shuhuda ambaye nilianza kutumia nishati ya Gesi katika Biashara yangu ya chipsi kwa miezi sita sasa,nimeona kuna faida nyingi na mabadiliko makubwa kwenye Biashara yangu. Kiukweli hapo kabla nilipokuwa natumia mkaa ,nilitumia hadi shilingi 40,000 kila siku kuupata mkaa na mauzo yalikuwa ya wastani tofauti na sasa.

Kwanza gesi imerahisisha kazi yangu, mwanzo tena kipindi cha mvua mkaa ulitumia hadi dakika 40 au 50 kuwaka na karai la mafuta lilitumia dakika hata 10 kuchemka. Tofauti na sasa nawasha jiko la gesi halafu nakadiria moto uwake vipi, kwa spidi ya juu au kidogo kulingana na wateja. Pia nikiona chipsi zimejaa nazima jiko , tofauti na mkaa ukiwasha basi umewaka hadi uishe.

Pili nimeongeza zaidi idadi ya wateja kwa sababu hakuna tena mteja anayeweza kusubiri chipsi kwani zikauka haraka. Nina jiko lenye pande tatu ,ya kwanza natumia kukaanga tu, ya pili kupashia na ya tatu kukaangia chipsi mayai na kuchomea mishkaki.

Tatu , ofisi yangu imekuwa katika hali ya usafi tofauti na mwanzo mkaa upisababisha sehemu nyingi kuwa nyeusi na kutokivutia weteja.

Pamoja na faida zote hizo lakini kikwazo kikubwa kwangu na kwa wananchi wengine ni kwamba gharama ya Gesi bado ipo juu sana na inazidi kupanda kila siku sio kupungua. Mtungi mkubwa wenye kilo 70 ,ambao ndani yake una kilo 38.5 za gesi katika kampuni ninayoagiza ,wanauza shilingi 108,000 kama ukienda kubadilisha na mtungi wako , lakini kama hauna kwa siku ya kwanza utatumia hadi shilingi 235,000 pamoja na vifaa vyake kama mpira wa kupitisha gesi na Regulator, na ninatumia hadi siku nne ndipo naenda tena kubadilisha kutokana na matumizi yangu.

Ukigawanya mahesabu hapo kilo moja ya gesi inagharimu hadi shilingi 2842 na pointi kadhaa, gharama inayokaribia na bei ya lita moja ya mafuta ya petroli na dizeli. Hata hivyo nimefanya uchunguzi kampuni hii ninayoagiza gesi nadhani ndio wanaouza bei rahisi kuliko wengine, wanaouza kuanzia shilingi 120,000 hadi 125,000 kwa mtungi wa kilo 70. Mitungi mingine ,kilo 30 shilingi 55,000, kilo 15 shilingi 24,000.

Kiukweli bei hizi za nishati ya gesi bado ni kubwa kulingana na kipato chetu na pia malengo ya serikali yetu inayoyahitaji. Siku moja nilimuuliza mzee mmoja kama yeye yupo tayari kutumia gesi ,alinijibu kwamba yeye anatamani sana familia yake iache kutumia mkaa sababu gesi inarahisisha sana muda na chakula kinaiva haraka, alisema anatamani watu wawe wanapikia hata maharage au nyama kwenye gesi, lakini uhalisia ni kwamba mtu anayepikia gesi ukizungumzia suala la kupika maharage au nyama kwenye gesi hakubaliani na wewe kutokana na bei yenyewe ya gesi na muda wa kupikia. Mzee huyu aliniambia anatamani sana huo mtungi wa kilo 15 uuzwe hata shilingi 6000, ili kila mwananchi atumie gesi .

Nchi yetu imebarikiwa na kuwepo kwa gesi katika eneo la Songosongo , lakini jambo lililonishangaza niliambiwa kuwa gesi tunayotumia kupikia inatoka nchi za nje. Mhudumu mkongwe katika kampuni hiyo wanayoniuzia gesi alisema kwamba gesi ya Songosongo inatumiwa zaidi viwandani. Ni kwa sababu tu haijafanyiwa uchakataji itumike majumbani hivyo ina nguvu sana.

Maoni yangu kwa serikali kupitia shirika la maendeleo ya petroli (TPDC) ,Je hatuhitaji matumizi ya nishati ya mkaa? basi tutumie gesi yetu kwa kufanya haya:

Kwanza kusomesha zaidi wataalamu watakaoweza kusaidia kufunga mitambo ya kisasa ya kuchakata gesi ya Songosongo ,ili wananchi waipate kwa bei rahisi, kama si hivyo basi tutafute kampuni shindani zinazoweza kuharakisha mchakato huu.

Pili kutafuta maeneo mengine zaidi ya kituo cha Songosongo ili kuongeza wingi wa bidhaa hii.

Tatu kama mambo yote hayo bado hatupo na utayari nayo ,basi serikali ipunguze kodi kama si kuondoa kabisa kwa makampuni yanayoagiza gesi kutoka nje,hii itasababisha kupungua zaidi kwa gharama ili tuondokane na kutumia mkaa na kuni.

Nadhani sasa wananchi tunaiihitaji zaidi nishati ya gesi kuliko nishati zingine kama umeme ambao sio wa uhakika kutokana na kukatika mara kwa mara.

Nalishukuru sana jukwaa la Jamii Forums kupitia kampeni hii ya Stories of change, kama sitofanikiwa kuwa mshindi basi naomba nakala ya andiko langu liifikie serikali kupitia shirika la maendeleo ya petroli TPDC.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom