Je, hili nalo linahusiana na Karma?

Je, hili nalo linahusiana na Karma?

Al maktoum

JF-Expert Member
Joined
Nov 23, 2022
Posts
499
Reaction score
678
Sina uzoefu mwingi wa matumizi ya mitandao ya kijamii, bado mshamba kiasi, na neno KARMA nimelipata humuhumu jamii forums. Katika kutafutatafuta maana ya KARMA kwa kutumia kamusi za humuhumu mitandaoni nikaelewa kuwa KARMA ni malipo anayoyapata mtu kutokana na maovu aliyowafanyia wengine.

Katika kuzifikiria siasa na wanasiasa wa nchi hii nikakumbuka kisa cha msomi mmoja aliyepewa mamlaka ya kukagua na kudhibiti hesabu za serikali na mheshimiwa mmoja aliyepewa uenyekiti wa Baraza la uwakilishi wa kutunga sheria na kuishauri serikali.

Msomi huyu siku fulani akizungumza na moja ya vyombo vya habari vya kimataifa na kuulizwa ni kwanini ukaguzi wa mahesabu unaonyesha hesabu za serikali haziko sawa na hakuna hatua zinazochukuliwa, msomi huyo akasema kwamba "HUU NI UDHAIFU WA BUNGE!"

Yule mheshimiwa wa mjengoni alipopata habari za maneno ya msomi huyu aliyoyazungumza akiwa nje ya nchi hasira zikampanda! "Bunge kuanzia sasa linasitisha ushirikiano na msomi huyu, lazima ahojiwe na kamati ya maadili, asipokuja mwenyewe kwenye kamati TUTAMLETA HATA KWA PINGU, TUMUONYESHE KUWA BUNGE SIO DHAIFU!"

Kumbukumbu zangu kama hazijanidanganya hazionyeshi kuwa mtu huyu alifika kwenye kamati, ila ambalo nina uhakika nalo msomi huyu hakuwahi kuomba msamaha kwa maneno yake aliyoshutumiwa nayo ya kusema "BUNGE NI DHAIFU", na mwisho wa mgogoro huo ilikuwa ni kila mmoja kusimamia anachoona ni sawa kwa upande wake.

Muda si mrefu muda wa kutoa huduma kwenye ofisi ya ukaguzi wa mahesabu ukafika ukomo na msomi huyu akarudi kwao visiwani kupumzika na familia yake, na nafasi yake akapewa mtu mwingine ambaye hakuwa na mgogoro wowote na baraza.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba watumishi wote waliofanya kazi ya ukaguzi wa mahesabu ya nchi tangu tupate uhuru hadi sasa wote majina yao yalianza na Mr. Hakuna ambaye jina lake lilianza na Dr. au Prof. zaidi ya Proffesor Musa Juma Asadi, ndio maana namwita msomi.

Siku zikaenda. Waswahili wanasema bora ujikwae kidole kuliko kujikwaa ulimi!

Mheshimiwa mkuu wa baraza la kutunga sheria pamoja na ubabe wa kumtishia Proffesor kwamba atamleta mjengoni kwa PINGU akasahau kwamba KUNA WABABE ZAIDI YAKE!

Mara ulimi wa mheshimiwa ukajikwaa na kuingia ndani ya kumi na nane za AMIRI JESHI MKUU. Chawa wa mama wakapiga kelele kila kona ya nchi hata wale waliomo mjengoni.

Haiwezekani kumkosoa Amiri jeshi mkuu hadharani! Mwanzo mheshimiwa huyu alipodai kukutana na MKE WA YESU kule Bethelehemu, baada ya chawa wa Yesu kuja juu, katibu wake wa baraza alimsaidia bosi wake kusahihisha na kuomba radhi kwa niaba yake.

Lakini alivyoingia kumi na nane za Amiri jeshi mkuu watu wote wakamkimbia!

Ikabidi mwenyewe atoke hadharani na kuomba radhi.

"JAMANI NIMEKOSA MIMI, NIMEKOSA SANA, MUNGU ANISAMEHE, WATANZANIA NISAMEHENI, ASANTENI SANA"

Baada ya masiku machache aligundua kwamba kuomba kwake msamaha ni kazi bure!, hakujabadilika chochote katika fikra za watu aliowakosea na hapo hakuwa na njia nyingine ya kumaliza ugomvi zaidi ya kung'atuka na kuachia kiti cha uenyekiti wa baraza na baada ya hapo yeye na yule msomi aliyemtishia kumpeleka bungeni na PINGU MKONONI wakawa wanaitwa wastaafu.

Kule zenji kuna CAG MSTAAFU na Dodoma kuna SPIKA MSTAAFU na wote kwa sasa majina yao hayatajwitajwi tena na vyombo vya habari ukilinganisha na hali ilivyokuwa enzi za utumishi wao.

Ama kweli kila shetani ana mbuyu wake na KILA MBABE KUNA MBABE ZAIDI YAKE!

JE HADITHI HII INA UHUSIANO WOWOTE NA KARMA?
 
Kwa maoni yangu ni karma,na yule prof ni mtu wa ibada sana,ogopa mtu ambaye anajikurubisha kwa Mungu,halafu akamwachia Mungu aamue
 
Back
Top Bottom