Mwanzo:3.8
Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone.
Mwanzo:3.9
Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi?
Mwanzo:3.10
Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.
Mwanzo:3.11
Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale?
Mwanzo:3.12
Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.
Mwanzo:3.13
Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.
Mwanzo:3.14
Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako;
Mwanzo:3.15
nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.
Mwanzo:3.16
Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.
Mwanzo:3.17
Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;
Mwanzo:3.18
michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni;
Mwanzo:3.19
kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.