Tafakari juu ya kijiji chenye mashine ya kusaga moja, bomba ya maji moja, duka la kijiji ni moja, hospitali au zahanati ni moja, basi linalounganisha miji na kijiji ni moja na pengine vyote hivyo ni mali ya mtu mmoja. Pengine nisieleweke sana kwa sasa, zamani kidogo ilikua kawaida, na kadri tulivyosogea ikawa ajabu tena ajabu sana.Katika mazingira yasiyo na ushindani huzaliwa mazoea katika kazi. Ni wakati huo ambapo, mtoa huduma huamka mda anao taka, atajibu apendavyo, na anaweza toa huduma mbovu lakini akashabikiwa na kubembelezwa kwa kuwa ni yeye tu.(iyena iyena). Pasipo ushindani, dhana ya “Mteja ni mfalme” haina maana. Mtoa huduma yeyote asiye na ushindani, haoni haja ya kuongeza ubunifu makini ili kuendelea kupata wateja wengi zaidi. Hujisahau na kufanya mambo kwa mazoea.
Hata hivyo wako watu wanaodhani wao wanapaswa kuwa tabaka la wateja tu na si watoa huduma. Dhana hii si sawa na ni mpango wa waliotangulia katika siasa na biashara kwa miaka mingi ili wengine wasijue tamu ya huko ndani. Akiulizwa biashara inaendeleaje, atajibu ngumu sana na.hali ukimtizama maisha yake yanaonesha ina mlipa. Vivyo katika siasa, waliotangulia hulithishana vizazi na vizazi na kuhadaa wengine kuwa siasa ni ngumu.
Ingawa kumekuwa na harakati za kumkwamua mteja na kumrejeshea hadhi yake. Harakati hizo zimeonesha nafuu ya kuzaa matunda walau mijini. Vijijini hali ni mbaya sana, wazee kwa vijana na wa jinsia zote ni kama wamekubali mteja kuwa lofa na hawataki kulipa gharama za wao kurudia hadhi yao ya asili.
Huendelea kushikilia msimamo wa zamani na wa kishabiki ambao huwaminya na kutweza utu wao. Ushabiki wa sura hii ni mithili ya uraibu. Uraibu huu, hupopolewa vikali na Mwana falsafa mmoja aliye wahi kusema “watu wanaopenda vitu vya zamani wako hatarini kukosa vizuri vya sasa na vya wakati unaokuja”.
Dhana hii imejidhihilisha wazi kwani wale waliokuwa wakisifia bidhaa za kielektroniki za kizamani mfano runinga za chogo, sasa wanakosa furahia wepesi wa runinga za sasa, uangavu wa picha, ubanaji wake wa matumizi ya umeme na zaidi, vile zinaweza kufanya mambo mengi kuliko hizo bidhaa za zamani.
Usisahau juu ya simu janja ambazo licha ya kubezwa sana wakati zikiingia hususani na wazee, sasa kila aliye anza kutumia simu hizi ameendelea na kuendelea na hakuna aliye rudi nyuma na zaidi kila mmoja amekua wakala mwema wa kujitolea kuzitangaza.
Katika jitihada za kumkwamua mteja na kumuamsha atambue hadhi yake, kuna changamoto ya uelewa. Mathalani mtizame mtu mwenye ukoma, mfumo wake wa fahamu huwa na changamoto katika kufikisha mawasiliano kwenye ubongo. Mbali na changamoto nyingi, anaweza shika kaa la moto na asisikie kuungua. Lakini wale ambao humuangalia na kwa kuwa mfumo wao wa fahamu uko sawa basi huumia juu ya asiyehisi kuumia.
Katika sura ya siasa ambayo ni mama wa utawala, ni jambo la afya kukawa na jukwaa sawa na lenye ushindani. Ni sawa na kusema, zama za kuwa na basi moja la kijiji zimepitwa sana. Wazee kwa vijana waamke na wajue tunaishi dunia ya ushindani.
Ubora wa bidhaa/huduma ndiyo kivutio pekee cha ushawishi na hivyo hatuwez lazimishana kupanda basi chakavu eti kwa kuwa ni la jirani au ndugu yako, au kwa kuwa liko hilo hilo. Tufukuze hofu na ujinga tufurahie maisha wanayo furahia wao wenye mabasi.
Jambo hili linatengeneza kitu kibaya kwa kuwa wale watu ambao wamejaribu kupinga au kutoa mawazo mbadala kwa mfano maprofesa, madaktari, na wasomi wengine kwa ngazi mbali mbali baada ya kuona jitihada zao za kuwaambia wakoma wasishike moto zinagonga mwamba, wamehamishia juhudi pambe za kuchochea moto juu ya miili yetu mpaka au iteketee au mfumo wa fahamu upate hisia za maumivu.
Sasa wamejiweka sokoni tayari kwa teuzi na wakiteuliwa hawafanyi makosa. Wana tumia magari ya serikali na mafuta mpaka kwa kuchezea, mishahara yao haikatwi kodi, wana ofisi nzuri na wana uhakika wa elimu ndani na nje ya nchi kwa watoto na ndugu zao, achana na masuala ya uhakika wa tiba dhidi ya maladhi.
Utawala bora ni matokeo ya vitu vingi ikiwemo ushindani uliosawa. Leo hii tumeshuhudia kukosekana kwa ulinganifu katika kupatikana wawakilishi wa wananchi katani na majimboni. Jambo hilo limepelekea kuwa na watu wa mawazo ya namna moja katika nyumba za kufanya maamuzi ya umma. Matokeo yake ni kila mmoja kusema ndio kwa kila kitu. Je wateja wanaheshimiwa katika huu mfumo?
Je ni sahihi tuendelee kuwa na basi moja la kijiji? Je ina ifaa nini kuendelea kuvumilia kula ugali kila siku na hali wenzetu wanabadilisha vyakula kila uchao? Je kuna watu wameandikiwa wao tu kufanya jambo flani katika nchi hii?
Jambo la namna hii limepelekea watu wenye uwezo mdogo wa kiuongozi kuteka jamii na kuifanya kuwashabikia wakila na kunywa tena huku wakivimbiwa na kushauriwa wale kwa kiasi. Hakuna uwajibishwaji, hatma yake ni kukubaliana kuficha maovu ya watawala kwa umoja na huku jamii ikigharimika kwa kukosa huduma bora.
Ninatoa wito kwa kila mteja kupambania hadhi ya kuwa mfalme, mabasi yote yamesajiliwa na madereva wake wamefaulu mafunzo, tuondoe shaka kwao. Tuachane na propaganda za wafanya kazi wa basi kongwe la kijiji wanazo wazushia washindani ati ni magaidi, hawalipi kodi, wataleta vurugu, hawana uzoefu na mengine yote.
Ni wakati wa kubadili basi kwa kuwa yako mengi ili hata lile la zamani lianze kuheshimu wateja wake, si lazima kununua duka ambalo ni la anaye jinadi ni ndugu yako kwa maneno na hali kwa matendo anatunyonya.
Utawala bora utarejea kwa ushindani na kwa mteja pekee kutambua hadhi yake popote alipo. Kila jambo lililopo na lililo kuwapo, tujue hutokea kwa sababu na si bahati mbaya. Tuamke, tumeimbiwa nyimbo za dhihaka na kutweza sana lakini tumekaa kuwatukuza wanaochezea mali za umma ambazo kimsingi ni zetu sote.
Kila siku wanazidisha ugumu wa maisha kwa kuwa tuko kimya. Muangalie mtu anaye kuibia mpaka, huwa anachukua kidogo kidogo na kuona unafanya nini, akiona uko kimya huzidi mpaka atafika uwanjani pako/pangu. Basi likiwa moja hakuna mteja atakua mfalme, ila yakiwepo mengi ndipo mteja atarejeshewa hadhi yake.
Upvote
0