Kuna taarifa inadai kwamba IPTL imewasha mitambo na ishazalisha umeme na kuiuzia Kampuni ya kusambaza Umeme nchini (TANESCO). Aidha, taarifa hii inadai kuwa huu ni uhaba wa umeme ulikuwa unatengenezwa ili watu wapige pesa.
- Tunachokijua
- Baada ya kusambaa kwa uvumi huu Jamiiforums imetembelea Tegeta, Salasala ilipo mitambo ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na kukuta kuwa hakuna dalili yoyote ya mitambo ya IPTL kuwashwa au kuanza kazi (Tazama katika video hiyo hapo juu).
Aidha, mazingira ya eneo hilo yamejawa nyasi hadi getini, baadhi ya vyuma vina kutu ikiwa ni ishara ya kutotumika kwa muda.
Kuhusu IPTL
Katika miaka ya 1990, Tanzania ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji katika mabwawa ya kuzalisha umeme, hali iliyopelekea kuwepo kwa upungufu wa umeme na kuathiri shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Katika kutekeleza Sera ya Nishati na kutokana na upungufu Mkubwa wa Nishati uliosababishwa na uhaba wa maji kwenye mabwawa mbalimbali nchini, mwaka 1994 Serikali ilitoa kazi ya uwekezaji kwenye sekta ya Nishati kwa Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) iliyokuwa inamilikiwa na kampuni za VIP Engineering and Marketing Ltd ya Tanzania na Mechmar Corporation ya Malaysia (MECHMAR). MECHMAR ilikuwa na asilimia 70 na VIP asilimia 30 ya hisa katika IPTL.
Kampuni ya IPTL ilipewa leseni ya kujenga, kumiliki na kuendesha (Build-Own-Operate) mtambo wenye uwezo wa kuzalisha umeme wa MW 100 kwa kutumia mafuta mazito eneo la Tegeta-Salasala, Dar Es Salaam. Tarehe 26 Mei, 1995, TANESCO na IPTL walisaini Mkataba wa miaka ishirini (20), kwa ajili ya kununua umeme uliozalishwa na IPTL ( Power Purchase Agreeemnt - PPA).
Kwa mujibu wa Mkataba (PPA), IPTL ilitakiwa kuiuzia TANESCO umeme usiopungua asilimia 85% ya umeme unaozalishwa kila siku ( minimum off take).
Hata hivyo, IPTL ilianza kuzalisha umeme mwaka 2002 na hivyo, muda wa miaka 20 ya mkataba ulianza kuhesabiwa mwaka 2002.
Ndoa ya IPTL na Serikali ya awamu ya nne ya Jakaya Mrisho Kikwete, ilivunjwa rasmi na Serikali ya awamu ya tano, iliyokuwa ikiongozwa na Hayati Rais Dkt John Joseph Pombe Magufuli.
Mwaka 2017 JPM alivunja mkataba huo baada ya IPTL kutaka kuongeza mkataba mwingine wa miezi 55.