SoC04 Je, tunayo nia ya dhati kutokomeza vitendo vya rushwa na ufisadi?

SoC04 Je, tunayo nia ya dhati kutokomeza vitendo vya rushwa na ufisadi?

Tanzania Tuitakayo competition threads

allymaker

New Member
Joined
Apr 3, 2021
Posts
2
Reaction score
0
Rushwa ni kitu chochote Cha thamani kinachotolewa Kwa lengo la kumshawishi mtu afanye au asifanye jambo fulani kinyume na taratibu na Sheria. Aidha kwa mujibu wa benki ya Dunia rushwa ni matumizi mabaya ya madaraka kwa manufaa binafsi.

Sheria za Tanzania zimeharamisha vitendo vya rushwa chini ya Sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007. Rushwa inaathari mbaya zaidi kwa jamii kiuchumi, kisiasa na kijamii. Rushwa inapokithiri sekta zote muhimu hupoteza ufanisi na kuacha raia katika dimbwi la umasikini.

Kwa mujibu wa benki ya Dunia inakadiriwa kuwa takribani asilimia tano (5%) ya Pato la dunia hupotea Kila mwaka kutokana na vitendo vya rushwa. Pia inakadiriwa kuwa nchi za ulimwengu wa tatu hupoteza asilimia ishirini (20%) ya Pato lake la mwaka.

Hiki ni kiwango Cha juu Cha upotevu wa pesa ambazo kama zingetumika kama ilivyokusudiwa basi zingeweza kuleta mageuzi katika maisha ya watu. Kwa kutambua athari mbaya za rushwa na ufisadi Kwa ustawi wa taifa,nchi yetu imechukua hatua kadhaa kukabiliana na changamoto hii. Jitihada hizo zimeanza tangu tilipopata uhuru kutoka Kwa waingereza ambapo serikali iliendeleza mapambano dhidi ya rushwa Kwa kutumia Sheria ya kuzuia rushwa sura ya 400 ya mwaka 1958.

Baada ya uhuru ilitungwa Sheria ya kuzuia rushwa namba 16 ya mwaka 1971. Mwaka 1975 Serikali ilianzisha kikosi Cha wapinga rushwa (anti-corruption squad) kikosi hiki kilikuwa chini ya idara polisi. Mwaka 2007 Sheria ya kuzuia rushwa namba 16 ya mwaka 1971 ilifutwa na bunge na kutunga Sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Kutungwa Kwa Sheria hii iliashiria mageuzi na kutoa Imani kwa wadau katika kukabiliana na rushwa. Sheria hii ilianzisha Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) chini ya kifungu Cha 5 Cha Sheria hii. Pia Sheria hii ilitanua wigo wa makosa ya rushwa Hadi kufika makosa takribani ishirini ambayo yametajwa kuanzia katika kifungu cha 15 Hadi kifungu Cha 38.

TAKUKURU ilipewa majukumu makuu mawili ambayo ni kuzui rushwa pamoja na kupambana na rushwa. Majukumu hayo yameainishwa katika kifungu Cha 7. TAKUKURU katika utekelezaji wa majukumu yake haya itatumia njia mbalimbali zilizoainishwa katika Sheria hii ikiwa ni pamoja na kushauri taasisi za umma na binafsi namna ya kukabiliana na rushwa, kuelimisha jamii kutambua rushwa na athari zake, kuhamasisha jamii kushiriki vita dhidi ya rushwa pamoja na kushirikiana na asasi za kitaifa na kimataifa kuhakikisha rushwa inatokomezwa.

Katika kupambana TAKUKURU inajukumu la kupokea malalamiko kuhusu tuhuma za rushwa,kufanya uchunguzi Ili kukusanya ushahidi kuhusu tuhuma za rushwa pamoja na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa watakaobainika kutenda kosa la rushwa Kwa mujibu wa Sheria.

Licha ya jitihada zilizofanywa katika mapambano dhidi ya rushwa tatizo hili limeendelea kutafuna taifa letu katika maeneo tofauti tofauti. Ripoti za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali inaanika ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma Kila mwaka. Hii inaashiria kuwa kama taifa tumeshindwa kukabiliana na kadhia hii na tunahitaji kubadili namna ya kukabiliana na tatizo hili.

Mapambano dhidi ya rushwa Kwa kiasi kikubwa yamekuwa nadharia ambayo haijawekwa katika matendo. Kwa tafsiri rahisi ni kwamba tunataasisi zenye mamlaka ya kupambana na rushwa lakini hatuna nia ya dhati ya kutumia taasisi hizo kutokomeza rushwa.

Hata hivyo bado hatujachelewa na tunaweza kufanya mageuzi na kupunguza kama sio kutokomeza kabisa vitendo vya rushwa. Tunaweza kujisahihisha tulipokosea na kuendeleza mapambano Kwa kufanya yafuatayo;

Kubadili namna ya kuelimisha jamii.

PXL_20240414_112259797~2.jpg

Eimu ni silaha yenye nguvu katika mapambano dhidi ya rushwa. Hata hivyo silaha hii imekuwa haitumiki ipasavyo na badala yake inafanywa bila ufanisi na kwamazora. Wanajamii wengi hawatambui namna rushwa inavyoweza kuathiri maisha yao.

Pia hawana elimu ya kutosha kutambua matendo yanayotafsiriwa kisheria kuwa makosa ya rushwa. Kwakiwango kidogo sana elimu juu ya rushwa inatolewa Kwa wanafunzi walio kwenye klabu za wapinga rushwa katika taasisi za elimu na keakiwango kikochini tofauti na inavyotakiwa kwani inaweza pita hata mwaka wanaklabu hawajatembelewa na maafisa TAKUKURU kuelimishwa.

Wanajamii ambao hawajapata fursa ya kwenda shule wanaendelea kuwa katika giza la maarifa kuhusu dhana ya rushwa na athari zake. Hii inapunguza nguvu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa kuondoa ushiriki wa raia katika mapambano haya muhimu.

Inapaswa kuwa na utaratibu wa mafunzo Kwa wanajamii na mafunzo haya yafanyike mara kwa mara na yasiwe Kwa wanafunzi pekee Bali yaguse wanajamii wote ikiwa ni pamoja na waishio vijijini. Tukilifanya Kwa ufanisi jukumu hili basi tunaweza kutokomeza rushwa. Je tuko tayari?

Kuchukua hatua Kwa wanaobainika. Kwa miaka kadhaa tumeshuhudia watu mashuhuri na taasisi mbalimbali zikitajwa kufanya ubadhirifu lakini hakuna anayewajibishwa. Napendekeza adhabu Kali zitolewe kama vile kifungo kirefu gerezani na kutaifishwa Mali zote Kwa wote wanaobainika kutenda kosa la rushwa ili iwe funzo Kwa wengine.

Pia taasisi zinzotajwa kufanya ubadhirifu zifumuliwe na viongozi waandamizi wote wa taasisi hizo wachukuliwe hatua. Adhabu hizi zitolewe bila kujali hadhi ya mtu kiuchumi Wala kisiasa. Tukiweza kutekeleza hili tutajenga nidhamu katika jamii na watu watahofia kujihusisha na vitendo vya rushwa ili kuepuka adhabu hizo. Je tuko tayari?

Utaratibu wa upatikanaji wa mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU ubadilishwe. Mkurugenzi mkuu wa TAKUKURU ndiye kiongozi mkuu wa taasisi hivyo anayo nafasi kubwa ya kuathiri mashauri yanayowasilishwa TAKUKURU. Kupatikana Kwa kuteuliwa na raisi kunapunguza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yake hasa linapowasilishwa shauri la rushwa linalogusa maslahi ya mamlaka yake ya uteuzi.

Ikiwa kweli tunania ya dhati kukabiliana na rushwa basi tunapaswa kufanya marekebisho ya Sheria ili mkurugenzi mkuu asipatikane kwa kuteuliwa Bali achaguliwe na watumishi wenzake ndani ya taasisi au ikiwezekana achaguliwe na raia ili kumpa uhuru zaidi katika utekelezaji was majukumu yake. Je tuko tayari?

Tuepuke kushughulikia tatizo la rushwa kwa manufaa ya kisiasa badala ya kushugulikiwa bila kufungamana na upande wowote. Kumekuwa na utamaduni wa kutumia rushwa kama silaha ya kisiasa kushambulia mpinzani was kisiasa.

Athari za utamaduni huu ni kuchagua tuhuma za kushughulikuia Kwa kutemeana na mlengo was mtuhumiwa kisiasa, kuelekeza nguvu kubwa kulaumu badala ya kuchukua hatua pamoja na kudhoofisha taasisi kwani wanasiasa wenye ushawishi wanaweza kuathiri maamuzi ya taasisi.

Msukumo was kisiasa unaweza kutumika kuwalinda wahalifu. Ikiwa tunalengo la dhati basi tunapaswa kushughulikia rushwa Kwa usawa bila kujali itikadi ya mtuhumiwa. Je tuko tayari?

Wizara ziondolewe fedha zinazotajwa kuwa za matumizi ya kawaida na badala yake waainishe matumizi hayo ili inapopitishwa bajeti ibainike fedha hizo zinatumika vipi. Kupitisha bajeti isiyo na uwazi wa mgawanyo wa matumizi ya pesa kwa kivuli Cha matumizi ya kawaida kunahalalisha matumizi mabaya ya fedha kwani hata kupima ufanisi wake ni vigumu.

Njia za kuripoti tuhuma za rushwa ziboreshwe. TAKUKURU imeainisha njia kadhaa za kuripoti matukio ya rushwa ikiwa ni pamoja na kupiga simu namba 113, kutumia TAKUKURU APP na kutumia barua pepe ya dgeneral@pccb.go.tz. Hata hivyo njia hizi kwasasa hazina ufanisi. App ya TAKUKURU imekosa ufanisi kumruhusu mtoa taarifa kwani haifanyi kazi.

Kwa upande wa barua pepe mtoa taarifa anaweza toa taarifa lakini asipate mrejesho wa shauri lake.Hii inavunja moyo na kuwafanya raia washindwe kutekeleza jukumu lao la kutoa taarifa. Ikiwa tunalengo la dhati kama taifa kukabiliana na rushwa basi hatunabudi kuboresha njia za utoaji taarifa na kutoa mrejesho wa mashauri yanayoripotiwa Kwa watu waliotoa taarifa ili wajue hatima ya taarifa wanazotoa.

Rushwa ni adui namba Moja wa maendeleo yetu hivyo tunapaswa kushughurika nayo kwa namna sawa na madhara yake. Kila mmoja Kwa nafasi yake anapaswa kushiriki mapambano haya muhimu kama mchango wake kwa taifa letu.

Aidha mapambano dhidi ya rushwa ni mapambano magumu zaidi ambayo yanaweza kugharimu uhai.Hata hivyo napambano haya ni mapambano ya lazima ambayo tunapaswa kuyashinda ili kuleta ustawi wa taifa letu kwa manufaa yetu na watakaokuja baada yetu.
 
Upvote 1
Back
Top Bottom