Je umechoshwa na unahitaji talaka ? Fuata hatua hizi

figganigga

JF-Expert Member
Joined
Oct 17, 2010
Posts
25,724
Reaction score
55,906
Kuomba talaka si dhambi. Kama lingekuwa dhambi sheria isingeruhusu jambo hilo kwakuwa si kawaida ya sheria kuhamasishi madhambi. Ni kwasababu hii nasema kuwa atakayeona amebanwa basi aombe talaka. Si kosa hata kidogo kufanya hivyo isipokuwa ndivyo tunavyoelekezwa na sheria zetu tunazozipenda na kuziheshimu sana.

1.KUVUNJIKA KWA NDOA.

Kuvunjika kwa ndoa kwa mujibu wa sheria zetu za Tanzania kuna mazingira mengi. Baadhi ya mazingira hayo ni yale yaliyoorodheshwa kifungu cha 12 (a-e) cha Sheria ya ndoa ambayo ni pamoja na kifo cha mmoja wa wanandoa, talaka ambayo tunaiongelea lakini pia yapo mazingira mengine mengi.

2. AINA ZA TALAKA

Talaka twaweza kuzigawa katika makundi mawili nayo ni, talaka itolewayo nje ya mahakama ambayo hutokana na ndoa zilizo katika mfumo wa kimila na nyingine ni talaka itolewayo mahakamani ambayo sisi hapa tutaiongelea.

3.UKITAKA TALAKA FUATA HATUA HIZI.

( a ) Hatua ya kwanza kabisa kwa anayehitaji kupata talaka ni kupeleka malalamiko yako kwenye kitengo maalum kijulikanacho kama Bodi ya usuluhishi wa ndoa ambayo imeanzishwa na Sheria ya ndoa kifungu cha 102(1).

Bodi itasikiliza malalamiko na kujaribu kufanya usuluhishi. Lengo la bodi ni kusuluhisha ambapo ikishindwa kusuluhisha itaandaa maelezo yanayohusiana na kilichojiri wakati wa usuluhishi ikiwa ni pamoja na kueleza namna ilivyoshindwa kusuluhisha. Sharti hili limewekwa ili kulinda ustawi wa familia kwa kuwa kupitia bodi wakati mwingine kunarejesha mahusiano ambayo yalikuwa tayari kuvunjika.

4.BODI YA USULUHISHI NI IPI NA IKO WAPI.

Kwa waislamu bodi ya usuluhishi ni Bakwata.Hautakiwi kufika mahakamani kudai talaka mahakamani mpaka una maelezo ya Bakwata kuwa umepitia kwao na suluhu imeshindikana.Ofisi za Bakwata zipo maeneo mbalimbali lakini haswaa ukiuliza misikitini watakuonesha.

Kwa wakiristo bodi ya usuluhishi iko ustawi wa jamii. Hautakiwi kufika mahakamani kudai talaka mpaka una maelezo kutoka ustawi wa jamii kuwa wamesuluhisha na imeshindikana. Ofisi za ustawi wa jamii zipo katika makao makuu ya kila wilaya ukifika hapo uliza utaoneshwa.

( b ) Hatua ya kwanza tumeona ni kupitia hizo bodi za suluhu sasa ni hatua ya pili ambayo ni mahakamani ambapo mwombaji atatakiwa kufika akiwa na kibali chake kutoka bodi kinachoonesha mwenendo wa usuluhishi na kushindwa kwa bodi kurejesha mahusiano. Ni katika mahakama ambapo mwombaji atatoa maelezo ya kuomba talaka huku akionesha sababu za kuishawishi mahakama hiyo ili ipitishe hukumu ya kuvunja ndoa. Kubwa zaidi atakalolionesha ni kuwa ndoa hiyo haiwezekani tena hata kwa namna gani.

Kwahiyo hatua ni mbili tu ile ya bodi ya usuluhishi na unamalizia na mahakamani.

5.SABABU ZA KISHERIA ZINAZOWEZA KUKUFANYA UOMBE TALAKA NI HIZI.

( a ) Kwanza ni zinaa. Inapotokea kuwa mmoja wa wanandoa amejamiiana na mtu mwingine ambaye si mme/mke wake na hali yupo katika ndoa ni sababu ya kubwa ya kuombea talaka.

( b ) Sababu nyingine ambayo mtu anaweza kuitoa akiwa anadai talaka ni kunyimwa unyumba kunakoendelea. Linatumika neno kunyimwa unyumba kunakoendelea kumaanisha kuwa haiwezekani mwanandoa akanyimwa unyumba maramoja au mara mbili halafu akaamkia mahakamani kudai talaka. Kunyimwa unyumba ili iwe sababu inabidi kiwe ni kitendo chenye kuendelea na si kitendo ambacho kimejitokeza maramoja au mara mbili.

( c ) Tatu , ukatili nao ni sababu anayotumiwa na mwombaji kuombea talaka. Tunaweza kusema kuwa ukatili ni matendo ambayo hayakubaliki yanayofanywa kwa makusudi na ambayo kimsingi yanaweza kusababisha hatari kwa afya ya mtu na maisha yake kwa ujumla kama kumpiga mtu mara kwa mara, kumtukana mtu mara kwa mara, kumuumiza kwa aina yoyote ile, kumwingilia mwenza wako kinyume na maumbile, ulevi wa kupindukia na wenye kuendelea, na mengine yote ambayo ni kinyume na ubinadamu.

( d ) Nne, talaka inaweza kutolewa iwapo mmoja wa wanandoa amethibitisha mahakamani kuwa mwenzake amemtelekeza . Kumtelekeza mtu katika ndoa kuna maana ya kujitoa katika mazingira ya uana ndoa bila sababu za msingi na bila ridhaa ya mwenzako hata kama mnaishi chini ya paa moja. Kwa hiyo kutelekezwa si tu kuondoka nyumbani mnakoishi na mwenza wako isipokuwa hata kuishi pamoja lakini bila kushirikiana katika mambo mbalimbali nako ni kutengwa.

( e ) Tano mtu anaweza kuomba talaka iwapo mwenzake amehukumiwa kifungo cha maisha au kwa kipindi kisichoshuka miaka mitano. Kama mtu amehukumiwa kifungo kama nilivyosema ni hiari ya mwanandoa kuamua kuivunja kwa talaka au kusubiri.

MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI MWANASHERIA NA MSHAURI WA SHERIA KUPITIA GAZETI LA SERIKALI LA HABARI LEO KILA JUMANNE , GAZETI JAMHURI KILA JUMANNE NA GAZETI NIPASHE KILA JUMATANO. 0784482959, 0714047241
bashiryakub@ymail.com

Chanzo: Sheriayakub
 
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…