JamiiTalks
JF Advocacy Team
- Aug 7, 2018
- 685
- 1,124
SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI, 2016
Sheria ya Huduma za Habari inasimamia weledi katika tasnia ya habari, na inaunda Bodi ya Ithibati ya Wanahabari, Baraza Huru la Habari, kushugulikia masuala ya kashfa, makosa yanayohusiana na Habari na misingi mingine ya udhibiti wa tasnia ya habari.
Vipengele muhimu na athari zake kwa tasnia ya habari ni pamoja na:
Usajili na Ithibati:
Vyombo vya habari vya uchapishaji (magazeti) vinalazimika kupata leseni kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo. Kifungu cha 8-10 vinaeleza mchakato wa kuomba, kukataliwa, na kufutwa kwa maombi ya leseni.
Mamlaka ya rufaa dhidi ya maamuzi hayo yapo chini ya Waziri mwenye dhamana ya maudhui na rufaa inalazimika kuwasilishwa ndani ya siku thelethini baada ya kutolewa kwa uamuzi husika.
heria hii pia inaweka masharti ya mwandishi wa habari kuthibitishwa (kupata ithibati) ili kufanya kazi za uandishi. [Kifungu cha 19] Bodi inaweza kufuta uthibitisho wa mwanahabari kutokana na kukiuka kwa kiasi kikubwa maadili ya taaluma yaliyoainishwa katika kanuni za maadili ya taaluma ya uandishi wa habari, na kwa mwandishi wahabari asiye raia wa Tanzania, kutotekeleza lengo la uthibitisho wake. Bodi hutunza orodha ya wanahabari ikijumuisha majina na maelezo ya wanahabari waliothibitishwa.
Mwandishi ambaye jina lake limeondolewa kutoka kwenye Orodha ya Wanahabari au aliyesimamishwa kufanya kazi za uandishi wa habari hatofanya kazi hizo walau kwa muda wa miezi mitatu. Mamlaka ya rufaa dhidi ya maamuzi hayo yapo chini ya Waziri na Mahakama Kuu. [Kifungu cha 21]
Athari: Hitaji la kisheria la kusajili na kutoa ithibati kwa waandishi wa habari lina changamoto kubwa, kwa kuwa ni kikwazo kwa watu waaandishi wanaopenda ama kuhitaji kuingia kwenye taaluma hiyo.
Vigezo vya kutoa ithbati kwa waandishi wa habari havikuainishwa kwenye Sheria hii; hali inayotoa mwanya kwa Serikali kuweza kuwaengua bila kufuata utaratibu wowote waandishi wanaoikosoa kutoka kwenye tasnia hiyo, hasa kwa kuzingatia kwamba Waziri ndiye anayeteua wajumbe wa Bodi ya Ithibati ya Wanahabri.
Bodi ya Ithibati ya Wanahabari na Baraza Huru la Habari
Bodi ya Ithibati ya Wanahabari (wajumbe saba wanaoteuliwa na Waziri) itatoa ithibati na vitambulisho kwa waandishi wa habari, itasimamia kanuni za maadili ya uandishi wa habari, na itasimamia na kuendeleza misingi bora ya maadili na nidhamu kwenye tasnia ya habari. Bodi inaweza kusimamisha au kuondoa wanahabari kutoka kwenye orodha ya wanahabari waliothibitishwa, kutoa adhabu ya faini kwa kukiuka kanuni, na kuweka ada na tozo mbalimbali katika zoezi la kutoa ithibati. [Vifungu 11-14]
Kila mwandishi aliyethibitishwa atakuwa mwanachama wa Baraza, kwa mujibu wa Kifungu cha 24 cha Sheria hii. Kwa kushauriana na Bodi, Baraza litaweka kanuni za maadili kwa tasnia ya habari na litahimiza kufuatwa kwa misingi ya taaluma ya habari miongoni mwa wanahabari na vyombo vya habari. Baraza pia litafanya marejeo kuhusu utendaji wa vyombo vya habari, kushughulikia malalamiko mbalimbali yanayotokana na machapisho (magazeti), na kuhimiza uwajibikaji kwenye tasnia ya habari. [Kifungu cha 26]
Haki na Wajibu wa Waandishi kwa Habari
Vyombo vya habari vya umma na vya binafsi vinaweza kukusanya habari kutoka vyanzo mbalimbali; kuchambua na kuhariri taarifa zilizokusanywa kwa kuzingatia maadili ya kitaaluma; na kuchapisha au kutangaza habari. Serikali ina udhibiti mkubwa kwa vyombo binafsi vya habari kwa kuvitaka kuchapisha na kutangaza kuhusu masuala yenye umuhimu kwa taifa. [Vifungu 6-7]
Vyombo vya habari havitotoa au kusambaza taarifa: zitakazodhoofisha usalama wa nchi na upelelezi unaofanywa na vyombo vya sheria; zinazokwamisha taratibu za sheria na au kuhatarisha usalama wa maisha ya mtu yeyote; zinazoingilia faragha ya mtu yeyote; zinazozuia maslahi halali ya kibiashara ikiwemo haki miliki ya mmiliki, au zinazozuia au kusababisha madhara makubwa kwa Serikali katika kusimamia uchumi;
Mtu yeyote atakayekwazwa na maudhui yaliyochapishwa kwenye gazeti au chapisho lolote anaweza kupeleka malalamiko yake kwenye kamati ya malalamiko ya Baraza ndani ya miezi mitatu tangu kuchapishwa kwa maudhui husika; Mamlaka ya rufaa dhidi ya fidia iliyotolewa yapo chini ya Mahakama Kuu. [Vifungu vya 20-29]
Athari: Mamlaka mbalimbali zinapewa madaraka kubwa katika kudhibiti maudhui na shughuli za kila siku za vyombo vya habari. Nguvu hizo, hasa kwa vyombo binafsi vya habari, zinaingilia uhuru wao wa uhariri na hivyo kuathiri kwa upana uhuru wa vyombo vya habari, kutoa maoni na kujieleza. Zaidi ya hapo, jamii inanyimwa haki yake ya kupata taarifa kutoka vyanzo mbalimbali vya habari na maoni aina mbalimbali za maoni.
Mamlaka ya Polisi
Jeshi la Polisi limepewa mamlaka pana ya kufanya upekuzi kwenye chombo cha habari na kukamata kifaa chochote kilichoanzishwa, kuwekwa, au kuendeshwa kwa kukiuka matakwa ya Sheria hii. [Kifungu cha 60] Makosa chini ya Sheria Hii
Kifungu cha 50 cha Sheria hii kinaeleza makosa na adhabu kwa kuchapisha habari kwa makusudi, uzembe, ya kutungwa na ya uongo, yenye nia ovu au ya kutungwa na ya uongo; au taarifa iliyokatazwa inayoweza kuhatarisha maslahi ya jamii, na hadhi, haki au uhuru wa watu wengine. Makosa mengine ni pamoja na kuendesha chombo cha habari bila ya kuwa na leseni, kufanya kazi ya uandishi wa habari bila ya kuthibitishwa na mamlaka husika, au kusambaza taarifa za uongo na zisizothibitishwa.
Makosa yanayohusu kashfa pia yameainishwa kwenye Sheria hii. Hairuhusiwi kuchapisha ama kutangaza habari zenye kukashifu isipokuwa tu iwapo habari hizo ni za kweli na zinabeba maslahi ya umma. Sheria inaeleza mazingira ambayo kuchapisha habari au taarifa za kashfa hakutochukuliwa kama ni kuvunja sheria, na ambayo mwanahabari husika hatoadhibiwa – hasa pale ambapo habari au taarifa husika inachapishwa na mamlaka za Serikali. Kuchapisha au kutangaza habari zinazohusu kashfa unaruhusiwa katika mazingira mbalimbali, hasa iwapo kutangaza au kuchapisha habari hizo kunafanywa kwa nia njema. [Vifungu vya 35-39].
Athari: Kufanya kashfa kuwa kosa la jinai kunakiuka haki ya uhuru wa kujieleza, na adhabu kama vile kifungo si kikwazo kinachokubalika katika kudhibiti uhuru wa kujieleza kwa lengo la kulinda haki na hadhi za watu wengine. Ujinaishaji huo wa kashfa unaweza kusababisha hali ya wanahabari kujidhibiti wenye katika kutekeleza majukumu yao. Kuna hatari ya kinga zinazopewa mamlaka za Serikali kuweza kuzima sauti zinazokosoa utendaji wa Serikali. Taarifa hizo muhimu hazilazimiki kuwa za kweli au kutolewa kwa nia njema. Hali hii inatoa hiyari na wigo mpana kwa Serikali na vyombo vyake kufanya maamuzi yasiyofuata taratibu na kuchapisha habari za uongo au zenye kashfa bila ya kuhofia kuwajibika, kupata madhara au adhabu yoyote.
Vitu Vilivyopigwa Marufuku
Uingizaji, uchapishaji, uuzaji, usambazaji au uzalishaji wa vitu vilivyopigwa marufuku utachukuliwa kama makosa ya uchochezo kwa mujibu wa Kifungu cha 53. Chini ya Kifungu cha 58 cha Sheria hii, Waziri ana hiari ya kuzuia uingizaji wa machapisho ambayo kwa maoni yake yatakwenda kinyume na maslahi ya umma. Vile vile, Waziri anaweza kuzuia uchapishaji wa maudhui yanayoathiri usalama wa nchi au wa jamii. [Kifungu cha 59].
Athari: Maamuzi yasiyofuata sheria yanayotegemea busara za Waziri yana changamoto zake. Hiari hiyo ya Waziri inaweza kutumia vibaya kwa kuzuia uingizwaji na uchapishaji wa bidhaa au machapisho yenye taarifa zisizoipendeza Serikali. Pia, Sheria hii haielezi kuhusu aina ya bidhaa au machapisho yanayoweza kuingia kwenye kundi la bidhaa zinazozuiwa, ili kuwawezesha wanahabari kujidhibiti kama inavyopasa kwa kutokiuka matakwa ya Sheria hii.
Vile vile, vitendo vya uchochezi vimetakwa kwa ujumla mno kwenye Sheria hii, hali inayoleta mashaka na kusumbua wanahabari katika kutafuta namna bora ya kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria. Pamoja na adhabu kali zilizowekwa, ni vigumu kwa mtu kugundua chapisho au taarifa yenye uchochezi au kufahamu mtu anayeamua kwamba taarifa fulani ni ya uchochezi.
Mwandishi anaweza kuandika na kuchapisha taarifa inayodhaniwa kuwa ya uchochezi bila ya yeye kufahamu, au kuchapisha maudhui yasiyoipendeza Serikali na ambayo yanaweza kuonekana kuwa ni uchochezi baada ya kuchapishwa ama kutangazwa na chombo cha habari. Kuna hatari kwa vifungu vinavyoruhusu kunyang’anya vifaa vinavyohusishwa na uchapishaji wa taarifa za uchochezi kutumika kufanya vyombo vya habari kushindwa kutekeleza majukumu yake, hasa iwapo vitashindwa kuendelea kutangaza au kuchapisha habari.
SLF
Upvote
1