Wataalam wa lugha wanazigawa lugha zinazozungumzwa Afrika, hasa kusini mwa jangwa la Sahara, katika makundi manne.
Kuna lugha za Kibantu kama vile Kingoni, Kisukuma, Kinyakyusa, Kihaya, n. k. Halafu kuna lugha za Kikushi (Cushitic languages) kama Kiiraqw n.k. Zipo pia lugha za Kiniloti (Nilotic languages) kama Kimasai, na Kimang'ati. Mwisho kuna lugha za Khoisan, mfano mzuri ndio hao Wasandawe na pia Wahadzabe.
Hapa Tanzania lugha zote hizo zinazungumzwa. Hata hivyo Kibantu kinazungumzwa na wengi zaidi, na Khoisan zinazungumzwa na wachache sana. Kwa Afrika ya Kusini, Xhosa ni mfano mzuri wa Wabantu na mfano wa Khoisan ni Khoikhoi na San (Wazungu waliwaita Hotentots na Bushmen).
Kwa hiyo hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya Wasandawe (ambao kimsingi ni Khoisan) na Xhosa (ambao kimsingi ni Wabantu). Kufanana kwa lugha zao (zote zinatabia inayoitwa "click") ni kutokana na mwingiliano wa kijamii na kiutamaduni. Yaani Xhosa waliathiriwa na lugha ya majirani zao Khoikhoi.
Inaaminika kuwa Wabantu wa Afrika ya Kusini wanaasili ya eneo la maziwa makuu ya Afrika ya Mashariki. Kuhusu Wasandawe, michoro ya mapangoni inaonyesha kuwa walikuwepo eneo hili miaka mingi sana iliyopita.