Analogia Malenga
JF-Expert Member
- Feb 24, 2012
- 5,108
- 10,191
Jenerali Ulimwengu aandika shairi kuwaasa walioko madarakani
MLIO MADARAKANI, JIFUNZENI KUCHELEA
MLIO MADARAKANI, JIFUNZENI KUCHELEA
| Nakuletea shairi, lino latoka moyoni Nakuomba likariri, ulitie maanani, Usije kulighairi, kuniona majinuni, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea | Uliye nazo akili, huna budi utambue, Mwenza wako ni adili, uendako mchukue, La, utakuwa batili, insi wasikutambue, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea |
| Jifunzeni kuchelea, mlio madarakani, Na sudi twawaombea, awalinde Rahmani, Na pindi mkikosea, basi radhi tuombeni Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea | Unapokuwa mkubwa, wako ukubwa ogopa, Hivyo si ulivyoumbwa, hadi ukafika hapa, Kwa bahati umekumbwa, wakati wewe ni kapa, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea |
| Kikataeni kiburi, na tambo za ufidhuli, Tutawapeni sufuri, mkijifanya ni nduli, Yenu ni ndefu safari, ya akili si misuli, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea | Epukeni kuwatisha, watu walio dhalili, Ogopa kudhalilisha, mtu aso na misuli, Ukitaka jaribisha, kwa mwamba alo kamili Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea |
| Madaraka nisemayo, si ya mmoja tu wengi, Kila mmoja anayo, kila mtu yake rangi, Kama hujui unayo, labda wavuta bangi, Mlio madarakani, Jifunzeni kuchelea | Jifunzeni lugha tamu, haiba inopendeza, Wajihi wa tabasamu, kila mkijieleza, Watu watieni hamu, kuja kuwasikiliza, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea |
| Ewe mkuu wa kaya, mwenye wake na uledi, Kisha umekosa haya, umewaacha stendi, Wakimbilia malaya, nyumbani katu huendi, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea | Mkikunja nyuso zenu, hovyo mwajiropokea, Watawacha mwende zenu, nyumbani watarejea, Wakumbuka nyuso zenu, mazimwi mlopotea, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea |
| Wake zako na watoto, nani atayewalea? Wafifiza zao ndoto, wakati ukibembea, Wajikalia kushoto, juha unachekelea, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea , | Msijeona muhali, kwa niliyojisemea, Wala hayana ukali, utaowaelemea, Yangu ni ya Kiswahili, lugha iliyotulea, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea |
| Kila siku u mkali, wana wanakuogopa, Wakiuliza maswali, huna jibu la kuwapa, Wanapokudai wali, wawatupia makopa, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea | Ki kitamu Kiswahili, na wageni waafiki, Yawaje hatukubali, nasi tukakipa tiki, Tukaionja asali, ya muruwa na mantiki, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea |
| Na mtemi wa kijiji, ama wewe mwenyekiti, Watu wanataka maji, wanazo zao risiti, Wanapokuita huji, kila siku vizingiti, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea | Kwa kujisemea hovyo, Kiswahili mwakitusi Hivyo msemavyo sivyo, mnatutia mikosi, Vyovote vile iwavyo, mu watu wenye nakisi, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea. |
| Pesa zao umekwiba, umeenda kuolea, Hujui wameza mwiba, tumboni utatoboa, Wajiletea msiba, usioutegemea Walio madarakani, jifunzeni kuchelea | Tamati natua nanga, kituoni napumua, Mtajaliona tanga, siku nitolifungua, Mawazo nitayapanga, mengi na yenye murua Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea |
| Ni mkuu wa wilaya, ama wako ni mkoa, Kubali kuwa na haya, watu wakikukosoa, Situtungie riwaya, majidai kutuboa, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea | Nakuombea salama, na maisha ya furaha, Uepushwe na zahama, na kila lenye karaha, Uzidishiwe karama, uongezewe staha, Mlio madarakani, jifunzeni kuchelea |