Jengo la Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika

Jengo la Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
JENGO LA AL JAMIATUL ISLAMIYYA FI TANGANYIKA (UMOJA WA WAISLAM WA TANGANYIKA)

Historia ya Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika (Umoja wa Waislam wa Tanganyika) ni historia ya pekee sana.

Jana nimepita mtaa wa Max Mbwana na Lumumba Avenue.

Mitaa hii hapo zamani wakati Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika inaundwa mwaka wa 1933 mitaa hii miwili ilikuwa inajulikana kama Stanley Street na New Street.

Miaka mingi sana ilikuwa imepita sijafika maeneo haya na kilichonivutia ni kibao cha BAKWATA nilichokiona nje ya mlango wa pembeni wa kuingia ndani ya jengo la Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika.

Hakuna popote palipowekwa alama yeyote kuonyesha kuwa hili jengo ni la Waislam.

Jengo hili lango kuu lake liko Lumumba Avenue na Mtaa wa Max Mbwana kuna mlango wa pembeni ambako kuna hicho kibao cha BAKWATA kinachosema kuwa hiyo ni ofisi ya Shekhe wa Wilaya.

Lango kuu la jengo hili pameandikwa ukutani TAMISEMI (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa).

Waislam walijenga hili jengo kuwa shule kwa watoto wao wasomeshwe masoma ya sekula na Qur'an.

Mwaka wa 1968 baada ya serikali kuvunja East African Muslim Welfare Society (EAMWS) na kuunda BAKWATA mali zote za Waislam zilikabidhiwa BAKWATA na hivi ndivyo Waislam walivyopoteza jengo hili na historia yake.

Baba yangu, Abdul na Ally Sykes pamoja na watoto wengine wa miaka ile walisoma shule hii.

Shule ya Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika hivi sasa iko chini ya TAMISEMI na jengo hili ni mali ya serikali.

Juhudi za kuiomba serikali kurejesha jengo hilo na shule kwa Waislam hazijafanikiwa hadi sasa.

Ally Sykes wakati wa uhai wake alihangaika sana kujaribu kulipata jengo hili.

Wazee wa Dar es Salaam ya miaka hiyo ya 1920 baada ya kuunda African Association waliamua waunde na Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika 1929 ili kuepusha kuchanganya mambo yanayohusu dini yao na African Association ambayo hiki chama kilikusudiwa kuwa chama cha Waafrika wote bila kujali imani zao.

Kuliona jengo hili kwa karibu ikanijia hamu ya kuingia ndani.

Niliingia ofisi ya Shekhe wa Wilaya na baada ya kutoa salamu niliomba ruhusa ya kupiga picha majengo yale.

''Umenipa ombi gumu,'' alinijibu sheke niliyemkuta pale ndani ofisini.

''Sheikh usilifanye hili jambo kuwa kubwa sana ningeweza nikapiga picha bila ya kuomba ruksa na wale usingejua kama nimepiga picha.''

''Kwa nini sasa hukupiga?''

''Siwezi kufanya hivyo sheikh si katika ustaarabu wala adabu za Kiislam,'' nilijibu.

''Jengo hili limejengwa na babu zangu na baba zangu wamesoma shule hapa wakati huo ikiitwa Al Jamaitul Islamiyya Muslim School,'' nilimjibu sheikh.

''Nani babu yako?''

Nilifikiri nimtaje Mzee Ali Jumbe Kiro au Mzee bin Sudi lakini nilijua majina haya yeye pengine hajapata kuyasikia katika historia ya Tanganyika.

''Babu yangu Kleist Sykes.''
Sheikh alibakia kimya kama vile anafikiri la kujibu.

Nikaendelea kwa haraka, ''Sheikh mimi nimepita hapa na ni miaka mingi sijaingia humu ndani lakini majengo haya yana historia kubwa sana katika kupigania uhuru wa Tanganyika.

Mimi naona fahari kuwa waliyojenga hili jengo na jengo lile la TANU na kupigania uhuru ni babu zangu na ndiyo sababu kwa kuwa nimepita hapa nikaona niingie ndani nipige picha.''

Kulikuwa na sheikh mwingine mle ofisini kakaa mbali kidogo na mlango ambako sheikh ninaezungumzanae meza yake ipo, nikamuona kanyanua shingo kaacha kuandika ananisikiliza.

Hapa pana historia kubwa sana.

''Maalim Mattar kamsomesha Qur'an hapa baba yangu na Abdul Sykes.''

Nilikuwa namtupia sheikh haya majina Abdul Sykes, Maalim Mattar nikiamini anayajua ingawa pengine si katika historia ya jengo lile bali labda kwa kuyasikia yakitajwa.

''Basi bwana piga picha nakuruhusu,'' sheikh alinijibu.

Mtaa wa Makisi Mbwana una maduka na biashara ziepangwa hadi barabarani.

Biashara kubwa hapa ni vyombo vya nyumbani kama, masufuria, sahani, vikombe nk.

Nilisimama pale mtaani nikakumbuka siku za udogoni Maulid ya Mfungo Sita mchana watoto wote wa Karikaoo tulikuwa tunakusanyika hapo mchana kwa ajili ya karamu kwani barabara ile zilipowekwa meza za biashara palikuwa panatandikwa majamvi na maturubai yanafungwa kuzuia jua.

Halikadhalika jengo na mtaa mzima usiku zinawashwa taa za rangi.

Maulidi yalikuwa yanasomwa Mnazi Mmoja mbele ya jengo la Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika.

Jengo la Al Jamiatul Islamiyya si mali ya Waislam kwa zaidi ya nusu karne.
Sasa ni jengo hilo hatunalo kilichobaki ni historia, historia ambayo hata hao BAKWATA weyewe hawaijui.

Naamini wale masheikh wangu ningewashangaza kama ningewaeleza kuwa Secretary wa al Jamiatul Islamiyya Ali Mwinyi Tambwe na Abdul Sykes walisafari hadi Nansio kwenda kumshauri Hamza Mwapachu kuhusu kumtia Julius Nyerere katika uongozi wa juu kabisa wa TAA mwaka wa 1953.

Naamini wangeshangaa sana pia kama ningewaambia kuwa Iddi Faiz Mafungo Mweka Hazina wa Al Jamiatul Ilsamiyya fi Tanganyika ndiye alikuwa Mweka Hazina wa TANU pia.

Naamiini wangezidi kushangaa kama ningewaambia kuwa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika ilitoa fedha kuchangia safari ya kwanza ya Nyerere UNO mwaka wa 1955.

Nina hakika wangeshangaa ningewaambia kuwa dhifa ya kumuaga Nyerere kwa safari hii ilifanyika ndani ya jengo hili la Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika.

1655829165759.png
1655829294153.png
 
Back
Top Bottom