SoC04 Jeshi la Kujenga Taifa liwe suluhisho la ajira kwa vijana

SoC04 Jeshi la Kujenga Taifa liwe suluhisho la ajira kwa vijana

Tanzania Tuitakayo competition threads

CLIFF SHEMELA

New Member
Joined
Jun 11, 2024
Posts
1
Reaction score
1
TANZANIA TUITAKAYO: JESHI LA KUJENGA TAIFA (JKT) LIWE SULUHISHO LA AJIRA KWA VIJANA

UTANGULIZI: Mfumo wetu wa elimu umekuwa na changamoto kubwa katika kutimiza ndoto za wahitimu wengi.Hii ni kwa sababu mfumo huu upo katika muundo wa msonge kwa maana kuwa katika ngazi za chini(Shule za Msingi na sekondari za kawaida) wanaosoma na kuhitimu ni wengi kuliko wanaohitimu katika ngazi za juu(kidato cha sita na vyuo).

KIELELEZO NA.1: Mfumo Msonge wa Elimu.
Hali hii hupelekea kuwa na kundi kubwa la vijana hapa katikati (wahitimu wa kidato Cha Nne waliofeli) ambao wanakosa uelekeo wa maisha baada ya kukosa fursa ya kuendelea na masomo kutokana na kuonekana kuwa na uwezo mdogo wa kitaaluma kwa upande mmoja, lakini pia kwa upande mwingine, uwezo mdogo wa serikali kuwachukua wahitimu wote kuendelea na ngazi ya elimu inayofuata. Mfano shule zenye sekondari za juu (A level) ni chache ukilinganisha na sekondari za kawaida (O level) ambazo zipo karibia kila kata nchini.
Mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa Sheria yanaweza kutumika kama suluhisho la ajira na uzalendo pamoja na kutimiza ndoto za vijana wetu.

Hali ilivyo Sasa ni kwamba mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria yanajumuisha vijana waliohitimu kidato Cha sita ambao wengi wao Wana uhakika na kuendelea na vyuo vikuu na vya kati.Hawa kwa mtazamo huo wanakuwa katika mfumo rasmi ambao unawatengenezea mazingira ya kuwa kwenye ajira katika sekta rasmi na zisizo rasmi.

Kwa Tanzania tunayoitaka,utaratibu huu wa kujiunga na JKT unatakiwa kuangaliwa upya. Utaratibu wenye tija kwa Taifa ni kuliangalia kundi kubwa la vijana wa kike na wa kiume ambao hawapati fursa ya kuendelea na masomo baada ya kuwa na matokeo yasiyoridhisha ya kidato Cha Nne. Hawa kwa mtazamo wangu ndio wanaotakiwa kuwa walengwa wa JKT kwa mujibu wa Sheria.

Utaratibu wa kuwachukua vijana ambao hawakupata fursa ya kuendelea na masomo (waliofeli mitihani ya Taifa ya kuhitimu kidato Cha Nne) utatupatia Tanzania tunayoitaka na kuwa na tija katika kutimiza ndoto za vijana wetu endapo utafanyika kwa kuzingatia mapendekezo yafuatayo:

i. Yaandaliwe makambi maalum na yaliopo yaboreshwe kulingana na mahitji. Makambi haya yatengwe kikanda za kiuchumi: Kilimo, ufugaji na uvuvi, Ujasiriamali na Biashara, Ufundi, TEHAMA, Sanaa na Michezo. Kuwepo na wataalam na vitendea kazi vya kutosha kwa fani husika( kwa ujumla mazingira yawe vutivu ili vijana hawa wasione kama ni adhabu kwenda huko)

ii. Baada ya matokeo ya kidato cha Nne kutangazwa, vijana wote wenye ufaulu mdogo na waliofeli (Divisheni IV na 0) wapangiwe kwenye makambi hayo kulingana na michepuo yao waliyosoma na uhitaji wa fani Kwa mlengwa. Kwa kufanya hivyo tutafanikiwa kuondoa wimbi la vijana waliokata tamaa mitaani na kujiingiza kwenye vitendo mbalimbali vya kihalifu na visivyo vya kizalendo ikiwemo kuzuia mimba na ndoa za utotoni.

iii. Serikali iweke muda maalum ( usipungue mwaka mmoja) wa mafunzo hayo, na baada ya hapo vijana hawa wawezeshwe mitaji na maeneo kwa ajili ya kuendeleza kile walichojifunza. Aidha, baadhi yao wanaweza kuandikishwa katika majeshi ya ulinzi na usalama ikiwemo JKT yenyewe kulingana na uwezo waliouonesha wakati wa mafunzo yao.

iv. Uwekwe utaratibu maalum wa kuwafuatilia vijana Hawa kuanzia wanapokuwa kwenye makambi hadi baada ya kuhitimu watakapokuwa wanatekeleza majukumu yao.Kwa kufanya hivyo serikali na mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali watapata watu sahihi wa kufanya nao kazi katika fursa mbalimbali zinazojitokeza.

v. Vijana waliohitimu mafunzo haya wapewe mwongozo wa kujiunga katika vikundi vya uzalishaji Mali.Kwa kufanya hivyo,mbali na kuwa vijana Hawa watakuwa wameshapata ajira lakini pia kwa upande mwingine itakuwa sekta nyingine ya ajira na wataweza kuwaajiri hata wenzao waliohitimu vyuo vikuu na vya kati kama wataalam wa kusimamia na kuendeleza miradi yao.Hivyo itasaidia katika kupunguza tatizo la ajira nchini.
Kwa upande wa wahitimu wa kidato Cha sita ambao hawakufanya vizuri, utaratibu huo wa kuwaita makambini unaweza pia ukawa na tija kwao na kwa Taifa kwa ujumla.wale waliofaulu vizuri utaratibu uliopo sasa unaweza ukaendelea isipokuwa mitaala ya vyuo iangaliwe upya ili kukidhi soko la ajira la nchini na kimataifa.

(Wafundishwe Stadi chache zinazoendana Moja kwa Moja na fani anayosomea) Mfano, Kuna baadhi ya vyuo wanawalazimisha wanachuo wote kujifunza lugha za kimataifa (mfano Kifaransa) wakati kwa fani anayosomea haimlazimu sana kutumia lugha hiyo, ni kumpotezea muda mwanachuo huyo na kumfanya awe anakariri tu ilimradi ahitimu au asirudie mitihani/kozi.Aidha wafundishwe jinsi ya kuanzisha, kusimamia na kuendeleza miradi ya wajasiriamali na vikundi vya ushirika sekta ambayo inaweza kuwaajiri wengi wao.

Kwa umakini na uzoefu wa JKT katika kusimamia na kuendesha mafunzo kama hayo, matokeo ya muda mfupi yanaweza kuonekana kuanzia miaka mitano tu na hivyo kweda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo ni maono ya Nchi yetu kwa miaka 25 ijayo.
 
Upvote 2
Back
Top Bottom