Kite Munganga
Platinum Member
- Nov 19, 2006
- 1,773
- 952
Katika kupitia gazeti la Nipashe nimekumbana na habari yenye kichwa cha habari kinachosema-Jeshi sasa laanza biashara ya ulinzi, na baada ya hapo ilinikumbusha miaka ya 1979/80 hivi wakati Dar ilikuwa inalindwa na JKT pamoja na Polisi hata hivyo ilikuja gundulika kuwa hao hao walikuwa ama wanashirikiana na majambazi au wanaazimisha bunduki zao kwa majambazi, mwisho wake serikali ilisitisha mradi huo, sasa najaribu kuwaza kuwa vijana hawa watakuwa trained kijeshi na wataiva kisawasawa (kumbuka ghasia zote za JKT) na baada ya hapo umpe ajira akalinde mamilioni au mabillioni ya matajiri wetu, sasa swali kubwa ninalojiuliza ni kwa mshahara upi mali hiyo itakuwa salama? kwani hata kama watapewa mshahara unaolingana na JWTZ bado watakosa marupurupu wanayopata wakiwa kambini ambayo hulainisha ugumu wa maisha uraiani, je serikali haioni kuwa inatayarisha hatari kwa watu wake na yenyewe pia? Mfano kijana huyu umpeleke North Mara Barrick akalinde dhahabu ya wale jamaa na huku unamlipa KCC unategemea nini hapo kwa mtu aliyepitia JKT?
Na Lulu George na Godfrey Mushi, Handeni
Serikali imeridhia Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA- JKT), liongezewe nguvu kiutendaji na kuwa kampuni ya ulinzi itakayotoa ushindani kwa makampuni binafsi ya ulinzi yanayotoa huduma hiyo kwa kiwango kisichoridhisha.
Kwa sasa SUMA, imejikita katika ujenzi wa nyumba za serikali, barabara na kutengeneza samani.
Uamuzi wa JKT kuwa na kampuni ya ulinzi, una lengo la kuajiri vijana wanaohitimu mafunzo ya awali ya kijeshi.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Kanali Ayoub Mwakangata, alitoa taarifa hiyo jana wakati akihutubia katika kilele cha mafunzo ya Operesheni Uadilifu yaliyokuwa yakifanyika katika Kambi ya 835 JKT Mgambo wilayani Handeni.
Katika taarifa yake alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na Jeshi hilo wameridhia kampuni hiyo kuanza kazi rasmi mapema mwakani.
Kampuni hiyo imepanga kuboresha huduma za ulinzi kwa kuajiri askari waliopitia Jeshi hilo pekee na kuwasambaza katika maeneo mbalimbali nchini kote wakichuana na makampuni mengine yaliyoko sasa, lakini bila ya kuathiri utendaji wao.
``Suma JKT itakuwa kampuni ya ulinzi rasmi kuanzia mwakani na itachukua vijana waliohitimu mafunzo ya awali ya kijeshi na si askari wa akiba wa mgambo, mpango huu ni maalumu kwa ajili ya kuwasaidia vijana kama hawa kupata ajira za uhakika baada ya kuhitimu mafunzo haya na ukweli ni kwamba hatua hii itakuwa ni changamoto kwa vijana wengi wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne kujiunga JKT,``alisema.
Awali Ofisa Utumishi wa JKT Makao Makuu, Meja Elvis Massawe alipohojiwa kuhusiana na hatua iliyofikiwa hadi sasa na Kitengo hicho cha SUMA alikiri kwamba Ofisi hiyo imeshapokea maombi zaidi ya robo tatu ya vijana waliohitimu katika Jeshi hilo nchi nzima wakisubiri kuajiriwa rasmi.
Kwa mujibu wa Ofisa huyo ni kwamba Kampuni hiyo mbadala ya ulinzi itachukua askari wa rika mbalimbali bila kujali umri wao na kwamba bado jeshi hilo linapokea maombi ya yawanaotaka kujiunga na kampuni hiyo.
Katika hatua nyingine, Jeshi hilo limelaani vikali migomo ya wanafunzi wa elimu ya Juu nchini likidai kwamba vitendo hivyo vinatokana na kukosa mafunzo ya Jeshi la kujenga Taifa kwakuwa hawajafunzwa nidhamu ya kijeshi.
Mkuu wa Kikosi cha JKT Mgambo, Meja Nyiga Singu alimweleza, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Luteni Winfred Lugubi aliyekuwa mgeni rasmi katika kilele hicho kuwa ni vyema sasa serikali ikaona umuhimu wa kurejesha mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria ili vijana watakaopita jeshini na baadae kujiunga na vyuo vya elimu ya juu wasishiriki hata kidogo katika migomo inayoendelea kama ilivyo hivi sasa.
``Afande (Mkuu wa Wilaya) naomba nikueleze mbele ya bosi wangu ambaye ni Kiongozi wa Brigedi ya 303, Brigedia Jenerali Alex Chitenga, kuwa tunaishauri serikali irudishe haraka mafunzo yale kwa mujibu wa sheria kwa vile hii migomo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu itafikia ukomo.
Hii ni kutokana na nidhamu tutakayowafundisha wakati wa operesheni za kijeshi,``alisema Meja Singu.
Katika kilele hicho cha mafunzo ya operesheni uadilifu jumla ya vijana 835 walihitimu mafunzo hayo na walikula kiapo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba watalitumikia Taifa kwa uaminifu na uadilifu mkubwa.
Source: Nipashe