andrew kisanga
Member
- Apr 27, 2013
- 53
- 23
Mirathi ni utaratibu mzima unaotumika katika kugawa mali ya marehemu pale anapofariki.
Msimamizi wa mirathi ndiye mwenye jukumu kubwa la kuainisha mali iliyoachwa na marehemu, kutambua warithi halali, kugawa mali ya marehemu, kulipa madeni kama yapo na kuhakikisha mirathi inafungwa mara baada ya kukamilisha ugawaji. Kutokana na mila, desturi, tamaduni na mazoea yaliyopitwa na wakati mara nyingi mjane hujikuta katika hali ya manyanyaso mara anapofiwa na mumewe.
Mifano halisi imeshuhudiwa na taasisi zinazotoa huduma za kisheria kwa wanawake. Mifano hiyo ni pamoja na wajane kunyang’anywa mali na watoto, kufukuzwa katika nyumba, kunyimwa usimamizi wa mirathi, kutuhumiwa kuua waume zao kwa sababu mbalimbali na kulazimishwa kuolewa na ndugu wa marehemu.
Aina za Sheria za Mirathi TanzaniaTanzania ina sheria tatu tofauti za mirathi ambazo ni:
1. Sheria ya Kimila ya Mirathi,Tangazo la Serikali Namba 358 la Mwaka 1963.
2. Sheria ya Mirathi ya Kiislamu.
3. Sheria ya Serikali ya Mirathi ya Mwaka 1865 [ Indian Succession Act 1865].
MuhimuSheria hizi tatu (3) hutumika pale tu ambapo marehemu hakuacha wosia. Iwapo kuna wosia basi mali itagawanywa kwa kufuata wosia huo. Kwa muislamu hataweza kuhusia zaidi ya 1/3 ya mali yake.
Matumizi ya Sheria za Mirathi.Sheria itakayotumika kugawa mali ya marehemu itategemea aina ya maisha aliyoishi marehemu wakati wa uhai wake kama ifuatavyo:
Marehemu aliyekuwa akiamini na kufuata dini ya kiislamu, mirathi yake itagawanywa kwa taratibu za dini ya kiislamu.
Marehemu aliyekuwa mtanzania asiye na asili ya kihindi au kisomali aliyeishi kulingana na mila na desturi za kabila lake sheria itakayofuatwa ni ile ya kimila (Sheria ya Kimila ya 1963 ni kwa makabila ya mkondo wa baba pekee).
Marehemu aliyeachana na mila na desturi za kabila lake na ambaye hakuwa muislamu basi Sheria ya Serikali 1865 itatumika kugawa mali yake.
Sheria ya Kimila ya MirathiMsimamizi wa mirathi ni kaka mkubwa wa marehemu.Warithi wa mali za marehemu ni watoto wake ambao wamegawanywa katika madaraja matatu (3):
• Daraja la kwanza- Mtoto wa kiume wa kwanza.
• Daraja la pili- Watoto wa kiume wote waliobaki.
• Daraja la tatu- Watoto wote wa kike.Mjane mwenye watoto: Mjane hana fungu la urithi ila atarithi kupitia mgongoni kwa watoto na ataishi katika nyumba ya ndoa mpaka atakapoolewa au kufariki.
Mjane Mgumba: Sheria ya kimila inasema mjane mgumba atapata 1/20 ya mali iliyoachwana marehemu.
Muhimu
• Sheria hii inapingana na Katiba kwa kuwa inamnyanyasa mjane na watoto wa kike. Ni sheria inayohitaji kubadilishwa.
• Iwapo mjane ataweza kuthibitisha kuwa marehemu alikuwa ameachana na mila na desturi za kabila lake basi kuna uwezekano wa Sheria ya Serikali kutumika.Watoto wa nje ya ndoa hawatarithi ila kama tu wamehalalishwa kwa kufuata mila na desturi za kabila husika.Mfano:
• Kabila A: mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa atahalalishwa kwa kuchinja mbuzi na damu yake kupakwa katika sikio la mtoto huyo na baadaye kuingizwa katika nyumba ya familia.
• Kabila B: mtoto atahalalishwa kwa baba wa mtoto kutoa ng’ombe dume kwa familia ya mama wa mtoto.
• Kabila C: mtoto atahalalishwa kwa kutoa debe mbili za mtama, kiasi cha pesa kwa mama wa mtoto na nguo. Sheria ya Mirathi ya Kiislamu.Mjane/wajane kama kuna watoto atarithi/watarithi moja ya nane (1/8) ya mali ya marehemu.Mjane/wajane kama hakuna watoto atarithi/robo (1/4) ya mali.
Watoto wa kike hupata fungu moja na mafungu mawili huenda kwa watoto wa kiume.Mtoto wa nje ya ndoa kwa dini ya kiislamu hawezi kurithi
Sheria ya Kiserikali Warithi walioainishwa katika sheria ya Serikali ni mjane/mgane na watoto.Mjane atapata 1/3 ya mali na 2/3 iliyobaki kugawanywa sawa kwa watoto wote.Mjane asiye na watoto atapata ½ ya mali ya marehemu na ½ iliyosalia itakwenda kwa wazazi wa marehemu.