Mausingizii
Member
- Jul 14, 2022
- 90
- 74
Awali mtoto wa kike hutakiwa kutokuondoa nywele zilizopo katika sehemu za siri kwa muda wa miezi mitatu, kisha huwekwa ndani kwa muda wa mwezi mmoja wakifanyiwa mambo ya kiutamaduni.
Baada ya hapo sherehe kubwa hufanyika ikiambatana na Unyoaji wa nywele hizo kwa mfumo wa unyonyoaji huku majivu ya moto yaliyochanganywa na dawa za kienyeji yakitumika.
Mashahidi walioyaondoa mavazi mwilini mwao huwazunguka wali hao, kisha ukeketaji hufanyika.
Baada ya tukio hilo wasichana waliokeketwa hutakiwa kurudi
kinyume nyume na kuigonga sehemu yenye jeraha katika tobo dogo lililotobolewa ukutani ili kukamilisha mila hiyo.
Utamaduni huu huambatana na vitendo vingi vya
kimila pamoja na mafunzo ya namna ya kumuhudumia mwanaume kingono na hata ndoa.
wakiamini kuwa kutokufanyiwa Ngoma hupelekea laana (wala wala) ambayo husababisha vifo vya watoto mara baada ya kuzaliwa kutokana na kugusa sehemu za uke ambazo hazikuondolewa.
Hii ni "NGOMA" utamaduni kutoka katika kabila la " wanguu" linalopatikana katika wilayani Mvomero, Tarafa ya Turiani , kijiji cha kibati chenye Sanduku la posta 67308 ,huko mkoani Morogoro .
Kabila hili limetapakaa pia katika vijiji vya Tunguri, vigereka, Diburuma mamboleo, masagalu ,kwevivu, sinya,kwesasu, mamboleo, Hoza, kwantembo n.k
Wakazi wa kijiji hiki hujishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula hasa mahindi, maharagwe na kilimo cha mazao ya bustani.
Ramani hapo chini, Inaonesha muonekano wa kijiji cha kibati kulingana na (Google Earth)
Mwanahamisi Ali (42) , Ni mkazi wa mtaa wa Difungo , amezungumza na muandishi juu ya mila hii.
Mabinti huchezwa mara tu baada ya kupevuka ridhaa yao.
Ngoma hufanyika mwishoni mwa mwezi wa saba hadi mwezi wa nane, Baada ya mavuno, ili kuweza kugharamia sherehe ambazo huambatana na zawadi mbali mbali.
Kutokana na suala hili ni wazi kuwa ustawi wa Afya ya mwanamke uko mashakani kutokana na madhara yatokanayo na ngoma hasa:
- Maambukizi ya magonjwa ya kuambukiza hasa UKIMWI na homa ya ini , kutokana na vitendo hivyo kutokufanyika pasipo kuzingatia tahadhari za kifya .
-Ndoa za utotoni , Ngono katika umri mdogo imepelekea ndoa na mimba za utotoni.
Jambo ambalo huwakosesha watoto haki ya elimu, kinyume na sera ya elimu ya mwaka 2014, inayolenga kuongeza idadi ya wananchi walioelimika kwa maendeleo ya uchumi wa kati, ifikapo mwaka 2025.
-Hali duni ya Maisha
Sherehe zinazofanyika wakati wa hutumia gharama kubwa, hivyo kupelekea Wanakijiji kuuza mazao mengi kwa gharama nafuu na kujikuta wakiishiwa akiba, hali inayopelekea kutopea katika lindi la umasikini.
Niwazi kuwa mambo haya yamekithiri kutokana na sababu mbali mbali
- Ukosefu wa hakimu wa mahakama ya mwanzo aliyehama mnamo mwaka 2012 hadi hivi sasa, hali iliyopelekea wenyekiti wa vijiji na wazee wa kimila kuwa waamuzi wa kesi za wanakijiji.
Uhaba wa maaskari polisi, kituo kidogo cha polisi kibati umepelekea kuundwa kwa polisi jamii, ambayo haiwezi kupambana na mila zao wenyewe, hivyo kupelekea wanawake na wasichana wanaokumbwa na matukio ya ukatili kukosa msaada wa kisheria.
-Ukosefu wa elimu kuhusu ukeketaji, uliopelekea kuwepo kwa ukinzani mkubwa baina ya wanakijiji na walimu wa shule za msingi wanaotoa elimu kuhusu athari za ukeketaji, Kama ilivyoripotiwa na waalimu hao . Hali hii inazidi kuchochea kukithiri kwa vitendo hivi.
-Utangamano duni baina ya wanguu na makabila mengine.
Utangamano huleta athari chanya ikiwemo kuzalisha mseto wa utamaduni, unaoweza kuzika mila za kizamani kupitia kujifunza baadhi ya mila kutoka katika makabila mengine. Utangamano hasi umepelekea mila na tamaduni za kizamani na zisizofaa, kuendelea kurithishwa kizazi hadi kizazi.
Pamoja na changamoto hizi bado sheria inashindwa kumlinda mtoto wa kike na ndoa za utotoni kufuatia,
sheria ya ndoa ya mwaka 1971 inayotoa ruhusa kwa mtoto wa Miaka 14 na kuendelea kuolewa ikiwa tu ni kwa ruhusa ya mzazi. Jambo hili linalowazuia watoto kupata haki ya elimu, malezi, huwasababishia mimba za utotoni na magonjwa kama fistula n.k
Sheria ya ukeketaji ya mwaka 1998 sura ya 2 kifungu 21 (169A) inapinga vitendo vya ukeketaji kwa watoto chini ya miaka 18 hivyo wanawake zaidi ya umri huo hukosa utetezi , kwamfano wajawazito walio na umri wa miaka 18 na kuendelea, wanaokeketwa pasipo ridhaa yao wakati wa kujifungua .
Ripoti ya mwaka 2022 iliyotolewa na shirika la haki za watoto duniani (UNICEF), inaonesha kuwa takriban watoto million 50 dunian kote, hukumbwa na matukio ya kikatili kila mwaka.
Kwa mwaka 2012 nchini Tanzania watoto wawili kati ya watano huozeshwa katika umri mdogo, huku mkoani morogoro ukeketaji ukifanyika kwa asilimia 42% (sauti ya siti: ukweli wa madai mwaka no 38 la mwaka 2012.)
Kwa mwaka 2015-2016 ripoti ya Ofisi ya taifa ya takimu imeonesha kuwa wanawake kati ya umri wa miaka 15 hadi 45 wamewahi kuendewa vitendo vya ukatili kwa asilimia 40, huku matukio 15,870 ya ukatili yakiripotiwa kwa mwaka 2020 na 11,499 kwa mwaka 2021 .
Ni wazi kuwa takwimu hizi bado haziridhishi.
Hivyo, Jamii, serikali, pamoja Na wadau wa maendeleo, wana wajibu wa kupinga vitendo vya ukeketaji, Ili kuwawezesha wanawake kupata elimu bora na kushiriki katika masomo ya sayansi, kushriki katika shughuli za maendeleo kama kilimo, ufugaji nakadhalika, vilevile kushiriki kikamilifu katika ngazi za maamuzi kama jinsi nyingine ili tuweze kutimiza mkakati wa Taifa wa kuufikia uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
Upvote
0