Abou Twika
New Member
- Jul 13, 2022
- 4
- 18
By Abou Twika
0784327893
Awali ya yote, nianze kwa kuwasalimu kwa jina la jamhuri ya muungano wa Tanzania. Ni imani yangu mu kheri wa afya, na wale wote tuliye na maradhi inshallah, kwa neema zake rabuka atatupa mrejesho wa afya zetu.
Twendeni pamoja kwenye mada isemayo, ni jinsi gani kasumba ya kielimu inavyochangia baadhi ya watu kushindwa kufanikiwa kwenye vitu vilivyowaonesha kuwa na talanta navyo.
Kwanza, tufahamu nini maana ya neno kasumba?
Kasumba, ni mgando wa kidhana, ambao hupewa uhai wa kuendelea kuishi katika akili zetu. Suala la ukasumba limekuwa ni sumu inayotumaliza, na inafikia wakati wengi tumekuwa tukibatilisha hata vitu vyevye mitizamo chanya, kwa kuamini ya kwamba kitu fulani ni bora au ndicho kinastahili kupewa mashiko/ kipaumbele kuliko vingine. Kasumba ikiganda akilini, ni tatizo kubwa sana kimabadiliko, na hata kiunyumbulifu kimawazo.
Kipi nakimaanisha?
Siandiki andiko hili kubeza umuhimu wa elimu nchini kwetu, na dunia kwa ujumla wake. Lengo ni kutaka kuwayeyusha mawazo mgando yanayoendelea kupewa uhai kwenye bongo zetu.
Ni ukweli usiopingika ya kwamba, elimu ni moja ya sekta nyeti na uti katika maendeleo ya sekta nyinginezo, kama vile kilimo, viwanda, biashara, na hata nyanja ya kiutawala. Lakini, hilo halituhalalishi sisi kuamini kuwa elimu ni kitu pekee kinachopaswa kupewa mkazo kwa watoto wetu, kama daraja la kuwavusha na kuwaandalia kesho zao zilizo bora.
Kuna mambo yanapaswa kurekebishwa, upande wa serikali na upande wa wazazi/walezi.
Mosi, kwa upande wa serikali kuna ulazima wa kuanza kuangalia uwezekano wa kubadili mfumo wa kiuendeshaji katika sekta ya elimu.
Yawezekana ni kitu ambacho kinaweza kuigharimu serikali kwa kubadilisha mtaala wa kielimu, lakini gharama ya mabadiliko hayo haiwezi kuonekana kuelekea siku za usoni, kama serikali itatoa muda wa kimchakato. Nafikiria hata kauli ya serikali inayowasisitiza wasomi kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa, nadhani yote inatokana na zao kubwa la vijana kukosa kuajiriwa, baada ya kutamatisha masomo yao.
Hiki kinachojaribiwa kusemwa na serikali yetu ni kitu kizuri sana, ila tutakubaliana na mimi kwamba mpaka sasa serikali haijapata mwarobaini wa kutibu homa hii sugu tunayougua Watanzania.
Kwanini?
Katika siku za kisogoni serikali yetu ilishatuzoesha kutupikia vyakula vilivyojawa tui pamoja na viungo kadha wa kadha. Leo hii mambo yamebadilika, hivyo lazima kuangalia mifumo mingine ya kiuendeshaji itayotupatia tiba ya kudumu kwa gonjwa lililotukumba. Ni wakati sasa serikali ianze kufanya mchakato wa kimabadiliko, kwa kuupatia mtaala wetu wa elimu uhalisia wa vitendo badala ya kulishwa maarifa kinadharia.
Naimani kama kutakuwa na msingi mzuri katika kuwajenga wasomi wetu kuanzia ngazi ya awali ya elimu(primary school) hadi ngazi za juu (universities), tunaweza kuzalisha wabobevu katika fani mbalimbali kama vile Wahandisi, Wana sanaa (wasanifu lugha, Wasanii, Waigizaji), Wanamichezo n.k
Tukubali tukatae, Tanzania yetu ina wabobevu wachache, ila wengi ni wataalamu katika taaluma hizo.
Kipi kinachoweza kusaidia Tanzania kupata wabobevu katika fani hizo?
Mosi, kuongeza dhana ya vitendo kwenye chakula cha nadharia. Chakula cha nadharia ni kitamu mno, mbele ya macho ya kadamnasi, lakini ni chakula ambacho unaweza kutamani kukitapika ule wakati unapotamatisha kula.
Kamwe hatuwezi kupata wabobevu wengi wa fani, kwa kuendelea kuwaandalia watoto vyakula vya nadharia pasi na vitendo vyake. Tutaendelea kupata wataalamu wengi katika fani hizo, Kwani misingi ya kuwaandaa wabobevu si faafu.
Pili, ubobevu wa jambo lolote unachagizwa na vitu kadha. Ni rahisi kupata wabobevu kama watu wanaweza kujikita katika vile vitu pendwa, na chaguo ndani ya nyoyo zao. Mnato wa kasumba ni dhana hasi iliyoota mizizi miongoni mwa wazazi wa Kitanzania. Inafikia hatua kuwa na ufinyu wa kimtazamo, hata pindi wanapobaini watoto wao kuwa na vipaji fulani, mfano kuimba, kucheza mpira, ufundi n.k.
Kuna nyakati watoto huchapwa mijeledi, pindi wanapoonekana kujikita katika vile vitu wanavyovipenda, na baadhi ya wazazi husikika wakisema "huu si muda sahihi".
Swali la kujiuliza kwa wazazi, upi huo muda sahihi kwa watoto wetu kufanya vile wanavyovipenda?
Naomba nieleweke ya kwamba, siikani elimu. Nachotaka kukisisitiza kwa wazazi/walezi, tuanzeni tabia za kuwasimamia watoto wetu katika vitu chanya vinavyoonekana kupendwa kunako sakafu za nyoyo zao. Muda sahihi wa kuwaendeleza na kuwabobeza, ni pindi wakiwa wachanga, kwani kadri mtoto anavyokua anaweza kupoteza dira ya talanta yake kutokana na uchangamani wa vile vinavyomzunguka.
Nini ushauri wangu kwa wazazi/walezi.
Wazazi wengi wa Kitanzania, tunaamini kuwa malezi ya watoto hukamilika kwa kutimiza mahitaji muhimu ya chakula, mavazi na malazi, sivyo ilivyo. Hayo hayatoshi kwa wazazi/walezi kujipiga kifua na kujikuta tumemaliza kila kitu. Ni vyema wazazi tukatenga muda mwingi wa kuzungumza na kufanya tafiti za kutosha kwa watoto wetu, ili kubaini vitu gani wanavyovipenda toka sakafu zao za nyoyo.
Wazazi/walezi lazima tutambue, mfumo wetu wa elimu haujajikita katika kuendeleza kesho ya vipaji vya watoto wetu. Tatizo ninaloliona kwa wazazi wengi, tunapenda kutunishana vifua na kujiona wafahari kisa tu watoto wetu wamemaliza vidato fulani. Hiki ni chakula kitamu sana, kinachoendelea kuipa shibe hali ya ukasumba miongoni mwetu.
Mwisho
Tamati ya andiko langu, naomba niendelee kusisitiza ya kwamba, elimu ni kichachuo cha ukuaji wa maendeleo ya nyanja na sekta mbalimbali. Lakini, rai yangu kwa serikali na wazazi, sasa ni wakati sahihi wa kuyeyusha barafu ya kasumba iliyotuganda, ili tuanze mchakato wa kukuza na kuendeleza vipaji. Kwa kufanya hivyo, tunaweza kupata mwarobaini wa kuwaepusha wasomi wengi kuwa watumwa wa kusubiria ajira, badala yake wanaweza kujiajiri wenyewe kupitia fani au vipaji vyao.

Upvote
2