Lycaon pictus
JF-Expert Member
- Jan 31, 2021
- 9,189
- 16,128
JINSI MPIGA BAO (RAMLI) ALIVYOTIWA NGUVUNI
Kutoka kitabu Masimulizi ya Mtawa Maporini kitabu cha pili. Unaweza kisoma bure ndani ya app ya Maktaba Sauti. Ipo Playstore.
Siku moja Juma aliniomba ruhusa ya kwenda kumtazama rafiki yake mwendo wa saa mbili kutoka pale kambini. Nikampa. Aliahidi kurudi kabla ya jua halijachwa. Jua lilipokuchwa, Juma hakurudi. Nikalala na wasiwasi usiku kucha. Wala sikuweza kuona sababu iliyomzuia asirudi kama alivyoahidi, maana alikuwa mtu wa mihadi sana.
Asubuhi na mapema akaja mtu kuniambia kuwa Juma amekutana na mchawi chini ya mbuyu, alikuwa akirudi kambini kiza kilipoanza kuingia. Juma akapatwa na ugonjwa mahututi hata asiweze kujisogeza. Ikawa amelala nyumbani kwa bwana aliyekuja kunipasha habari. Yule mtu akasema "Mgonjwa taabani, wala hajiwezi."
Nikamwambia yule mtu anisubiri kidogo tufuatane. Nilipomaliza kupika na kunywa chai yangu, nikafuatana naye. Tulipofika, nilimkuta Juma katika hali ya kuogofya. Ugonjwa wake hasa ulikuwa ni woga mtupu. Juma ni mtu anayeamini sana mambo ya uchawi. Kama angelitokea mtu na kumwambia kuwa maadam amekutana na mchawi chini ya mbuyu ule atakufa, naam angelikufa kweli kwa woga na kuamini kwake.
Nilipomwuliza yaliyompata, alihadithia kama mtu anayekata roho. Alisema kuwa alipokuwa akirudi, kiza kilikuwa kimekwisha anza kuingia. Alipofika penye mbuyu uliokuwa karibu na njia, aliliona jitu lililokuwa na macho yangarayo kama moto limebeba mifupa na vichwa vya watu waliokufa. Mara ile ile jitu likatoweka na kumwacha Juma mwili wote umemwisha nguvu na kumfanya nusu maiti hata asiweze kukumbuka jinsi alivyoweza kufika pale alipolala sasa. Akaniomba nimwitishe mpiga bao ili amwambie afanye nini apate kuepukana na maradhi yale. Sikuchelewa kutimiza maombi yake na mara mpiga bao akawasili.
Mpiga ramli alipofika tu, akaanza kazi yake bila ya kusema na mtu wala kuuliza asili ya kupiga bao na kwa nini au kwa sababu gani. Macho yalikuwa yamemtoka alipokuwa akitoa vitu vyake vya uganga na kututia woga sisi sote tuliokuwa pale. Akasemasema maneno ya kutisha ambayo hatukuweza kujua maana yake kwa sauti nene na ya kukwaruza. Kisha akaanza kusema kwa Kiswahili yafuatayo:- "Jana saa moja ya usiku ulikutana na mchawi chini ya mbuyu sivyo?" "Ndivyo!" Juma akajibu, "Mchawi huyu," yule mganga akaendelea "jina lake Nyambonde. Mchawi huyu ni mbaya sana. Macho yake yanang'ara safia. Ulipokutana naye alikuwa anatoka kufukua maiti ya watu aliowaua. Hakumwona amebeba maiti?" "Nimemwona, Juma akajibu, "Hmm." Mpiga ramali akaendelea. "Kama ungelichelewa kidogo tu, bila ya kuniagiza mimi, kucha mbili zisingepita bila kuiaga dunia."
Juma aliposikia maneno yale akapigwa na butaa. Lakini badala ya kuingiwa na woga zaidi alionekana na hali nzuri saa ile ile. Moyo wake ukajaa furaha kwa kuwa yule mpiga ramli alimtoa shaka kwa maneno yake. Juma akajitenga vizuri ili apate kusikia vizuri mashauri atakayosema mpiga ramli kwa kuepukana na kifo ambacho kama mpiga ramli yule asingelikuwapo pale, angekuwa maiti baada ya saa chache kupita. Kwa kuwa nilikuwa si mshirikina, sikuweza kuelewa lolote katika mambo yote yaliyopita pale.
Mpiga ramli akasema, "Basi waambie nduguzo walete mbuzi mweupe, jogoo mweupe, njiwa manga mweupe na mayai saba kwa tiba ya ugonjwa wako. Vitu hivi ndivyo nitakavyotumia mimi kwa uganga wangu. Kisha itakubidi kutoa dhiraa sita za bendera (kitambaa chekundu), na sita bafta kwa kumfurahisha na kumwomba radhi Nyambonde kwa kuwa umeona alichochukua. Ada yangu ya uganga na kupiga ramli ni kama kawaida; yaani shilingi nne kupiga ramli na nne utabibu.
Tulipounga hesabu ya vitu vilivyotakiwa pamoja na gharama ya utabibu, tukaona kuwa zinatakiwa shilingi themanini na mbili kamili. Kwa kuwa fedha hii ilitoka mfukoni mwangu, ubongo ukachafuka. Juma akatibiwa, akawa mzima bukheri wa afya kama zamani. Mimi nikapatwa na ugonjwa wa mawazo kwa kumfikiri sana mpiga ramli. Ama kwa hakika alinishangaza jinsi alivyoweza kusimulia yaliyompata Juma bila ya kusikia wala kuona ingawa nafsi yangu haikukubali kumsadiki mpiga ramli yule, nilishindwa kuiona njia ya udanganyifu wake. Wenyeji wengi sana walikuwa wakimsadiki sana hata jina lake likavuma mbali. Watu wengi wakasema kuwa hakuna mganga awezaye kutibu mtu aliyekutana na mchawi yule aliyekutana na Juma isipokuwa yeye tu. Wakazidi kusema kuwa kweli yupo mchawi yule aliyekutana na Juma chini ya mbuyu; na watu wengi wamepata kukutana naye karibu na mbuyu ule ule. Ati ndiyo njia yake kuu chini ya mbuyu ule.
Baada ya masiku kupita, mambo yakanigeukia mwenyewe. Ilikuwa siku moja nilipokuwa nikirudi kutoka kuwinda nikapita pale mbuyuni kiasi cha saa moja u nusu za usiku. Pale mbuyuni nikasikia sauti kama paka atoapo ukali. Nilipotupa macho upande uliotoka sauti ile sikuona kitu. Nikaiweka bunduki yangu tayari kwa lolote lilitakalotokea. Nikaisikia sauti ile tena. Mara nikauona mwanga wa moto mkali sana wenye ukubwa wa kikombe ch chai. Nikapigwa na butaa nisijue la kufanya. Nikasimama kama jiwe na huku nywele zikinisisimka. Moto ule ukawa unazimika kila sauti ile inaponyamaza na kuwaka ikitokea. Sauti ile ilipotoea mara ya nne, ilikuwa na mwanga mwekundu sana kama wa chuma kilichookwa na muhunzi na katikati yake yakatokea meno makubwa ya kutisha bila ya mwanzo wala mwisho. Moto ule pamoja na meno yake vyote vikanisogelea. Mara kikatokeza kiwiliwili kilichokuwa na umbo la kutisha ajabu! Pande zote za kiwiliwili kile kulining'inia vichwa vya watu; vitatu kila upande. Vichwa hivi, vilikuwa vimefungwa kwa kamba toka shingoni mwa kiwiliwili. Nikajitia ujabali na kusema, "Nani we, sema upesi au nitakutia risasi !"
Lo! Si kishindo chake hicho kilichotokea. Lile jitu likageuka na kuanza kukimbia na huku vile vichwa vya wafu vikigongana ngongolo ngongolo. Nikamfukuza na huku nikisema, "Simama wee! Au nitakupiga risasi." Lile jitu likazidi kukimbia. Tukatokeza kwenye weupe, yaani mahali pasipokuwa na miti ya kutia kiza kwani mwezi ulikuwa mpevu. Hapa nikapiga risasi kwa juu ili apate kuogopa na kusimama. Lile jitu liliposikia sauti ya bunduki, likasimama na kusema, "Tafadhali sana usiniue. Nasimama."
Nikamwendea na kumkamata. Nikamchukua, nikampeleka mwizi mdanganyifu yule kwa Jumbe wa kijiji. Jinsi alivyohukumiwa kwa udanganyifu wake sikuambiwa. Nafikiri kule aliachiwa kwa kuogopa wasipatwe na baa. Sijui tena labda alihukumiwa vingine. Mchawi yule ni yule yule mpiga ramli. Juma alipopata habari alipigwa na butaa pevu kikweli kweli.
MWISHO