Jinsi ya kudhibiti matumizi ya biashara ili kupata faida kubwa

Jinsi ya kudhibiti matumizi ya biashara ili kupata faida kubwa

Makirita Amani

JF-Expert Member
Joined
Jun 6, 2012
Posts
1,915
Reaction score
3,422
Kwenye makala iliyopita tulijifunza jinsi ya kujua faida halisi ya biashara yako. Na tuliona kwamba faida halisi sio mauzo kutoa manunuzi, bali unahitaji kuweka na gharama za biashara pia. Kama hukusoma makala ile ni muhimu sana uisome.

Kama tayari umesoma makala hiyo, utakuwa umepata picha kwamba mauzo na manunuzi yanaweza yasibadilike sana. Hivyo faida yako kwa sehemu kubwa sana inaweza kuwa inategemea kwenye matumizi yako kwenye biashara unayofanya.

Gharama za biashara zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara wengi kuweza kuendelea. Hii imekuwa inawafanya wasione faida iko wapi na hivyo kuwa na imani kwamba huenda wanaibiwa. Lakini wao wenyewe ndio wanajiibia kwa kushindwa kudhibiti matumizi yao kupitia biashara ambazo wanafanya.

Leo kupitia mtandao huu wa NAPENDA BIASHARA, utajifunza njia za kudhibiti matumizi yako kwenye biashara ili uweze kupata faida kubwa kwenye biashara yako.

Andika matumizi yote.
Baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiandika matumizi makubwa tu, lakini madogo madogo wamekuwa hawayaandiki. Hii inawafanya waone matumizi hayo madogo hayana athari, ila ukweli ni kwamba yana athari kubwa sana.

Fedha yoyote ambayo utaitoa kwenye biashara yako, hata iwe ndogo kiasi gani, iandike. Kwa kitendo cha kuandika tu, kwanza unajijengea nidhamu kwamba huwezi kuondoa fedha kwenye biashara hovyo tu. Na kama matumizi unayotaka kufanya siyo ya msingi, utaona aibu kuandika na hivyo kuacha matumizi hayo.

Jilipe mshahara kutoka kwenye biashara yako.
Kosa kubwa ambalo wafanyabiashara wengi wamekuwa wanafanya kwenye kuendesha biashara zao ni kufikiri kwamba kwa sababu biashara ni yao basi wanaweza kuchukua fedha wakati wowote ambapo biashara inaendelea. Hiki ni chanzo kikubwa cha kupata hasara kwenye biashara.

Kuchukua fedha kwenye biashara bila mpangilio ni kuirudisha nyuma. Badala ya kufanya hivi, jiwekee kiwango cha mshahara ambao utakuwa unajilipa kutoka kwenye biashara yako. Inaweza kuwa ni kwa mwezi, wiki au hata siku. Heshimu kiwango hiko na kama hakikutoshi usikimbilie kuongeza kiasi unachojilipa, bali kuza biashara kwanza na kipato chako kitaongezeka.

Nunua vitu pale tu una matumizi navyo.
Baadhi ya wafanyabiashara hujikuta wakifanya manunuzi ambayo sio muhimu kwao, au hayahitajiki kwa wakati husika. Wengi hufikiri wamepata kwa gharama nzuri na labda wakati watakapohitaji hawatapata kwa urahisi. Huku ni kujidanganya, usinunue kitu chochote ambacho huna matumizi nacho kwa haraka. Ni bora fedha hiyo ukaiacha izunguke kwenye biashara na iongeze faida.

Tumia teknolojia kupunguza gharama.
Maendeleo ya teknolojia yamerahisisha sana uendeshaji wa biashara. Kama utaweza kutumia teknolojia vizuri unaweza kupunguza baadhi ya matumizi ya biashara. Kuna njia rahisi sana za kuwafikia wateja wako kupitia mtandao wa intaneti. Jifunze njia hizi na utaokoa gharama ambazo unatumia sasa na inawezekana hazileti majibu mazuri.

Anza kutumia njia hizi z akudhibiti matumizi yako ya biashara na muda sio mrefu utaanza kuona faida ya biashara yako. Kama tulivyosema kwenye makala iliyopita, hakuna chuma ulete kwenye biashara, chuma ulete ni wewe mwenyewe kwa kushindwa kuthibiti matumizi ya biashara yako. Anza sasa kudhibiti matumizi na utaona faida yako iko wapi.

Kwa ushauri zaidi wa biashara piga simu 0713 666 445 na utapewa ushauri na mwongozo mzuri wa kibiashara.

JIFUNZE BIASHARA, PENDA BIASHARA.
 
Back
Top Bottom